Waziri Mkuu wa zamani, Mhe. Fredrick Sumaye |
WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, ameibuka tena na kusema, wanaokerwa na karipio lake kuhusu rushwa, wanapaswa kuachana na vitendo hivyo viovu.
Hivi karibuni, Sumaye, alitoa karipio kwa
viongozi wa dini hususani ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT), akionya kuhusu kasi ya wanasiasa kutumika katika
harambee zake.
Sumaye, alikaririwa akisema miongoni mwa
wanasiasa hao, wanatumia mwanya huo kama njia ya kuungwa mkono
watakapotangaza kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Ingawa hakuwataja wanasiasa hao kwa
majini, kauli yake ilitafsiriwa kumgusa Waziri Mkuu ‘aliyemrithi’ na
baadaye kujiuzulu, Edward Lowassa.
Lowassa ameshiriki harambee mbalimbali
nchini, hali inayoelezwa na baadhi ya wachunguzi wa mambo ya siasa kuwa
ina lengo la ‘kujisafishia’ njia kuelekea urais wa 2015.
Lakini Lowassa amekanusha kushiriki
harambee hizo kwa nia ya kutafuta urais, badala yake akasisitiza kwamba
ana karama ya ushawishi inayomfanya afanikishe shughuli hizo kwa kupata
fedha nyingi.
Jana, Sumaye alizungumza na vijana wa
klabu za Jogging za Ukwamani na Islamic katika uwanja wa Tanganyika
Packers jijini Dar es Salaam jana.
Alisema kama mtu anaumizwa na karipio lake
dhidi ya vitendo vinavyoashiria rushwa, anapaswa kuachana navyo na si
kumjibu kwa kejeli.
Sumaye alisema ushiriki wake katika vita
dhidi ya vitendo viovu kama rushwa, umeanza muda mrefu na kwamba hata
karipio lake kwa wanaousaka uongozi kwa njia zisizo sahihi ni sehemu ya
kuisimamia imani na dhamira yake.
Alisema, “kama kuna mtu anayeumizwa kwa
kauli zangu ninapokaripia uovu, nikipinga rushwa basi watoaji na walaji
rushwa waache kujihusisha na vitendo hivyo, na kama hawataki kusemwa
basi wapasuke.”
Sumaye alisema si rahisi akaacha kukemea
vitendo viovu hasa vinavyofanywa na viongozi kwa sababu, ukimya ni
sehemu ya kishawishi kwa waovu kuendeleza vitendo viovu.
Akimnukuu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliposema, serikali ya wala rushwa haiwezi kuleta maendeleo kwa wananchi wake.
Sumaye rushwa ikiachwa ishamiri, itakuwa vigumu kujenga nchi yenye usawa, hivyo kuifanya nchi kuwa katika hatari ya kuangamia.
“Hivi sasa imebaki miaka miwili ya kuingia
katika Uchaguzi Mkuu, hivyo tutaanza kushuhudia namna kanga, kofia,
fedha na vitu vingine vitakavyotembezwa kwa ajili ya kutafuta uongozi.
Tusipolisema sasa, tutaangamia,” alisema.
Alisema wananchi wanapaswa kuwa makini na viongozi wanaotumia ushawishi wa fedha na rushwa, kwani hawafai kuongoza.
Alisema viongozi wa aina hiyo wana kundi
la watu nyuma yao, wanaowafadhili hivyo pindi watakapopata uongozi,
watalazimika kuwatumikia waliomo katika ufadhili huo.
Alipinga dhana kuwa vijana ni kama bomu
linalongoja kulipuka, badala yake ameitaka serikali kuhakikisha wanapata
fursa ili wazitumie kuliko kuwaita kwa majina hatarishi.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment