Bondia Francis Cheka (kulia) |
Msimamo huo wa Cheka unatofautiana na mkwara uliotolewa na Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO-Limited) iliyomtaka asidhubutu kucheza mechi yake isiyo na ubingwa dhidi la Mmalawi Chiotcha Chimwemwe.
TPBO kupitia Rais wake, Yasin Abdallah 'Ustaadh' ilionya kuwa Cheka hapaswi kupigana ndani ya siku 30 kabla ya pambano lake na Mmarekani Findley Derrick litakalokuwa la kuwania ubingwa wa WBF, litakalochezwa Agosti 30 jijini Dar.
Kabla ya pambano hilo Cheka alishasaini pigano jingine dhidi ya Mmalawi Chiotcha Chimwemwe litakalofanyika Agosti 10 kwenye uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro katika shamrashamra za sikukuu ya Idd el Fitri.
Hata hivyo akizungumza na MICHARAZO kwa njia ya simu jana toka kambini kwake mjini Morogoro, Cheka alisema hawezi kukacha kupigana na Mmalawi kwa madai ni sehemu ya maandalizi ya pambano lake dhidi ya Mmarekani.
Cheka alisema alishasaini mikataba na waratibu wa michezo hiyo na hivyo ni vigumu kusitisha pigano lake la Chimwemwe hata kama silo la ubingwa wowote.
"Mimi nitacheza mapambano yote, lile la Mmalawi ni kama sehemu ya maandalizi ya pigano lake dhidi ya Derrick, pia waratibu wa pambano la pili wenyewe ndiyo waliochelewa kumalizana nami na kujikuta nasaini mechi ya Chimwemwe," alisema Cheka.
Aliongeza haoni ubaya wa yeye kupigana na Mmalawi kabla ya kuvaana na Derrick, licha ya kukiri anapaswa kuwa makini ili asijeruhiwe kama ilivyotokea walipoumana na bondia huyo mjini Arusha na kutetea taji la IBF Afrika.
"Chimwemwe ni bondia nzuri na hatari ulingoni, hivyo nitacheza pambano langu la Idd Pili kwa umakini ili nisishindwe kupigana na Mmarekani, pia muda wa kujiandaa na pigano la pili unatosha kabisa sioni sababu ya kuibuka kwa malumbano wakati huu," alisema Cheka.
Hata hivyo TPBO-Limited kupitia rais wake, imeendelea kusisitiza kuwa Cheka anapaswa kuzingatia ushauri wake ili asije akavuruga pambano hilo la kimataifa la WBF ambalo litazidi kumjengea jina kuliko mechi ya 'ndondo' isiyo na tija.
Pia amesema taarifa walizonazo ni kwamba Chimwemwe ana pambano atakalopigana na Mkenya Agosti 10 na siyo Cheka na kudai huenda ni mbinu zinafanyika kulivuruga pambano hilo la Cheka na Mmarekani.
No comments:
Post a Comment