Husseni Javu |
Javu amekuwa akitajwa kuwa ameshasaini mkataba wa miaka miwili wa kuichezea Yanga kwa msimu ujao, lakini uongozi wa Mtibwa Sugar umesema taarifa hizo siyo za kweli kwa sababu hakuna maafikiano yoyote yaliyofanyika.
Mkurugenzi wa klabu hiyo, Jamal Bayser aliiambia MICHARAZO kuwa, ni kweli Yanga waliwafuata wakionyesha nia ya kumsajili mfungaji wao huyo hodari, lakini baada ya kuwapa masharti yao hawakurejea tena kwao.
Bayser alisema kutokana na ukimya huo wa mabingwa hao wa soka nchini, ni wazi huenda wameachana na wazo la kumsajili mchezaji huyo ambaye bado wana mkataba naye wa kuichezea klabu hiyo mpaka mwakani.
"Javu bali ni mali yetu tuna mkataba naye, pia tangu Yanga walipokuwa kwa mara ya kwanza wakionyesha nia ya kutaka kumsajili hawajarudi tena, na kunashangaa kwamba mchezaji huyo akielezwa kasajiliwa Jangwani," anasema.
Anasema anadhani taarifa za Javu kutua Jangwani ni za kuuzia magazeti tu kwa vile hakuna makubaliano yoyote na wenzao wa Yanga, akiamini pia nyota huyo aliyeanza kuichezea Mtibwa kupitia timu ya vijana tangu mwaka 2007 atasalia Manungu kwa msimu ujao.
Javu mwenyewe aliliambia MICHARAZO kwamba bado anajitambua ni mchezaji wa Mtibwa Sugar, licha ya kukiri kuwahi kufuatwa na viongozi wa Simba na Yanga kwa nia ya kumshawishi kujiunga na klabu zao.
"Walinifuata kwa nyakati tofauti ili kunishawishi nitue katika klabu zao, ila niliwaeleza mimi bado nina mkataba na Mtibwa hivyo wakazungumze na mabosi wangu wakiafikiana sintakuwa na tatizo, ila mpaka sasa sijui kinachoendelea," alisema Javu aliyepo pia kwenye kikosi cha pili ya taifa 'Young Taifa Stars.
Mwisho
No comments:
Post a Comment