Kamanda Kihenya Kihenya. |
ABIRIA 13 wamekufa katika ajali baada ya gari aina ya Toyota Hiace kugonga gari la mizigo lililokuwa limeharibika
barabarani katika kijiji cha Ngogwa wilayani hapa.
Kaimu
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Kihenya Kihenya alisema jana
kuwa ajali hiyo ilitokea juzi saa 2 usiku ambapo Hiace hiyo namba T 756
CHX inayofanya safari zake Kahama na Ushirombo iligonga lori hilo namba T
999 AMS.Alisema katika ajali hiyo, watu 11 walikufa papo hapo na wawili katika hospitali ya wilaya ya Kahama wakati wakitibiwa. Kamanda alisema majina ya waliokufa hadi jana hayakuwa yamepatikana. Hata hivyo, alisema baadhi ya ndugu na jamaa walijitokeza jana jioni kutambua miili ya ndugu zao.
Kaimu Kihenya alishukuru wakazi wa kijiji cha Ngongwa kwa kutoa ushirikiano kwa Jeshi hilo baada ya ajali kutokea. Kamanda alitaka madereva kuwa makini wanapoendesha magari hasa usiku na wawe makini wakiwa na abiria.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Joseph Fwoma alithibitisha kupokea maiti 11 akiwamo dereva wa Hiace, Ezekiel Werema ambaye pia ndiye mmiliki wake. Alikiri majeruhi wawili pia kufia hospitalini hapo.
Katika hatua nyingine, Chama cha Wamiliki wa Mabasi ya Mikoani (TABOA) kimesema ajali nyingi za mabasi zinazotokea nchini, zinasababishwa na mamlaka husika, kutoa leseni kwa kampuni au wafanyabiashara bila utafiti wa kina na wao kutoshirikishwa.
Barua iliyoandikwa na chama hicho ikisainiwa na Katibu wake, Enea Mrutu kwenda wa Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe na nakala kusambazwa kwa vyombo vya habari, ikisema pamoja na uzembe wa madereva pia kwa kiasi fulani linachangiwa na utoaji wa leseni usiofuata utaratibu, ikiwamo kupewa leseni watu wasio na sifa.
“Uwepo wa ajali nyingi barabarani ni changamoto sugu katika sekta ya usafirishaji kwani tumejaribu mara nyingi kulikabili tatizo hili, lakini bado ajali zinaendelea kuwepo na hii inatokana na kampuni nyingi au watu wengi kupewa leseni bila utafiti wa kina,” alisema Mrutu.
Aliendelea kushauri kupitia barua hiyo: “Tunaomba uwepo utafiti wa kina wa kampuni mpya kabla ya utoaji wa leseni ya usafirishaji na Taboa makao makuu na matawi yake mikoani washirikishwe na ipewe nguvu kama wanavyofanya Chama cha Wasafirishaji wa Malori (TATOA) kwani hupewi leseni bila kupita kwao.”
Alisema Tatoa wameweza kusimamia ubora wa malori yanayoingizwa nchini, mwendo na kupunguza ajali za malori barabarani.
Aidha, chama hicho kilisema kilibaini uwepo wa mabasi mengi yaendayo mikoani na ndani ya mikoa yasiyo na leseni za usafirishaji, jambo alilosema kuwa ni hatari katika sekta ya usafirishaji hasa katika suala zima la kupunguza ajali za barabarani.
Alisema uwepo wa kampuni nyingi zinazomilikiwa na watu kutoka nje ya Afrika Mashariki zinazoingiza mabasi nchini na kupewa leseni ya biashara bila hata Taboa kupewa taarifa, unachangia kudhoofisha chama katika kusimamia taratibu za usafirishaji nchini.
No comments:
Post a Comment