KATIKA kuhakikisha Watanzania wanakuwa na afya
bora, kinywaji kisicho na kilevi cha Vita Malt, kimeandaa bonanza maalumu
litakalowashirikisha wafanya mazoezi na litakalofanyika katika mikoa ya Dar es
Salaam, Mwanza, Arusha na Mbeya.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam jana, Meneja wa Vinywaji visivyo na Vileo katika Kampuni ya Bia Tanzania
(TBL), Consolata Adam alisema, wameamua kuandaa bonanza hilo ili kuwakutanisha
pamoja wafanya mazoezi wote, ambao mara nyingi wanafanyia katika vituo maalumu
(gym).
Consolata alisema, bonanza hilo la aina yake kwa
Dar es Salaam litafanyika katika Viwanja vya Posta vilivyopo Kijitonyama
kuanzia saa 12 asubuhi hapo kesho (Jumamosi).
“Tumeamua kuandaa bonanza linalowakutanisha
wanamichezo mbalimbali hasa wafanya mazoezi ili kuweza kukutana na kufanya
mazoezi kwa pamoja.
“Siku hiyo katika Viwanja vya Posta kutakuwa na gym
kumi na mbili zilizo maarufu ambazo zitashiriki na kutakuwa na wakufunzi kumi
ambao wataongozwa na mkufunzi wa kimataifa SAAS,” alisema, huku akidai mtu
anatakiwa kwenda tu kwani mazoezi hayo yatakuwa bure.
Alisema, lengo kuu kuu la bonanza ni kuhamasisha jamii nzima kutambua umuhimu wa
kufanya mazoezi ili kujenga afya bora za miili yao na pia kujenga umoja imara
wa gym zilizopo nchini.
Consolata alisema, katika kuhakikisha bonanza hilo
linakuwa bora na la kufana jumla ya gym kumi na mbili zitashiriki ambazo ni
Better Life, Genessis ya Kijitonyama, Segerea Gym, Rio Gym,Genessis ya Kimara,
Azula ya Mikocheni na Serena Gym.
Alisema pia baa zilizoshinda katika kuchoma nyama
katika mashindano yaliyofanyika hivi karibuni za Fyatanga ya Tegeta na Kisuma
Bar ya Temeke, zitaonyeshana umwamba kwa kuchoma nyama bomba kwa kipindi chote
hicho.
“Tumeweka burudani za kila aina kwani kutakuwa na
michezo mbalimbali ya kufurahisha kama soka, netiboli, kuvuta kamba, kukimbiza
kuku, Sehemu za watoto kuchezea pia na zawadi nyingi toka Vita Malt zitakuwepo.”
Naye Meneja Mawasiliano na Mahusiano wa TBL, Edith
Mushi alisema mbali na hayo kutakuwa na burudani mbalimbali toka kwa bendi African
Stars ‘Twanga Pepeta’ na msanii mkali wa Hip hop, Roma Mkatoliki sambamba na
burudani nyingine nyingi kwa kipindi chote cha tamasha.
“Hii ni siku ya familia napenda kuwajulisha
watanzania wote na wapenda michezo kote nchini kuwa waje mapema na familia zao
siku ya Jumamosi, hakutakuwa na kiingilio chochote na vinywaji vyote toka TBL
vitakuwepo.
“Lakini pia watu wa kawaida na wa rika zote siku
hiyo hakutakuwa na kikwazo chochote cha kufanya mazoezi, kwani ni bure kabisa,
hivyo nawashauri tufike kwa pamoja ili tuweze kupata pia ushauri mbalimbali juu
ya kupunguza uzito na aina ya mazoezi yanayotakiwa,” alisema.
Vita Malt ni kinyaji kinachozalishwa na kusambazwa
na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
No comments:
Post a Comment