Madam Ritha akiwa na mshindi wa mwaka jana Walter Chilambo |
FAINALI za mashindano ya kusaka vipaji vya kuimba ya Epiq Bongo Star Search (EBSS) mwaka huu zitafanyika Novemba 17 jijini Dar es Salaam, waandaaji walisema jana.
Mkurugenzi wa kampuni ya Benchmark Productions, Ritha Poulsen, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa wamejipanga kuboresha mashindano hayo na wadau watarajie kushuhudia fainali zilizoandaliwa katika kiwango cha kimataifa.
Alisema kuwa awali walipata washiriki 50 lakini sasa baada ya kuwachuja wamebaki 20 ambao wataingia kambini na kupewa mafunzo mbalimbali ya muziki kabla ya kuwachuja na kubaki wanane watakaoingia fainali.
“Lengo la kuanza kambini mapema ni kuwapa fursa washiriki kujifunza zaidi vitu muhimu katika muziki na hii itawasaidia kuboresha vipaji vyao," alisema mratibu huyo.
Alisema kuwa washiriki hao waliopatikana wametoka katika mikoa sita ya Arusha, Mbeya, Mwanza, Dodoma, Dar es Salaam na Zanzibar.
Naye mshindi wa shindano hilo kwa mwaka jana, Walter Chilambo, aliwataka vijana kuondoa aibu ili wajiandae kutimiza ndoto zao za maisha.
“Vijana wengi wamejitokeza msimu huu ila wameonekana kuwa na aibu baada ya kuwaona majaji, hali hii si nzuri na huwezi kufikia malengo," alisema mshindi huyo.
Naye Ofisa Biashara Mkuu wa Zantel, Sajid Khan, alisema wamejipanga kuhakikisha shindano hilo linakuwa la aina yake mwaka huu kupitia udhamini wa kampuni yake.
Alisema pia bado washiriki wanaendelea kusailiwa kupitia namba ya simu 0901551000 au kutuma ujumbe mfupi kwenda 15530 kama ilivyokuwa kwa mshiriki Meninah Abdulkarim aliyepatikana kwa njia huyo wakati wa mchakato wa mwaka jana.
No comments:
Post a Comment