STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, September 26, 2013

Simba 'kamili gado' kuiua JKT Ruvu


KLABU ya soka ya Simba imetamba kuwa wapo kamili gado kwa ajili ya 'kuiua' JKT Ruvu watakaokutana nao kwenye pambano la Ligi Kuu Tanzania Bara siku ya Jumapili, licha ya kukiri wanatarajia kupata upinzani mkali kwa wapinzani wao hao.
Simba wanaoongoza msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 11 na JKT Ruvu waliopo nafasi ya pili wakiwa na poini zao 9 watavaana kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam katika mfululizo wa ligi hiyo iliyopo raundi ya sita.
Benchi la ufundi la Simba limekiri kutambua ugumu wa pambano hilo dhidi ya JKT Ruvu, lakini limetamba kuwa hawana hofu yoyote kwa vile kikosi chao kipo fiti ikiwamo kuendelea vyema kwa baadhi ya wachezaji waliokuwa majeruhi.
Kocha Msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelu 'Julio', aliiambia MICHARAZO kwa njia ya simu jana akiwa kwenye kambi ya timu hiyo iliyopo Bamba Beach, Kigamboni kuwa, kikosi chao kipo tayari kwa vita ya Jumapili ili kuimarisha uongozi wao.
Julio alisema wanajua wanakutana na timu ngumu, lakini wanajipanga ili kuweza kuvuna pointi zote tatu na kuendelea kujikita kileleni baada ya mechi yao iliyopita kupata sare ya mabao 2-2 mbele ya 'wageni' Mbeya City ya Mbeya.
Kocha huyo mwenye maneno mengi alisema kwa kuwa lengo la Simba msimu huu ni kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu baada ya kuupoteza msimu uliopita kwa watani zao Yanga, hawatafanya makosa kwa JKT au klabu yoyote watakayokutana nao.
"Kambi yetu inaendelea vyema ikiwamo wachezaji waliokuwa majeruhi wakiendelea vyema na imani yetu tutapata ushindi kwa JKT Ruvu ili kuendelea kukaa kileleni, japo tunajua litakuwa pambano gumu mno," alisema Julio.
Julio aliongeza pamoja na kukiamini kikosi chao, hawaidharau timu yoyote katika ligi hiyo na badala yake watakuwa wakishuka dimbani kama wanacheza fainali muhimu kuvuna pointi zitakazowasaidia mbele ya safari.

No comments:

Post a Comment