STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, October 22, 2013

Wafuasi wa Sheikh Ponda kidedea


Sheikh Ponda Issa Ponda katika harakati zake

MAHAKAMA Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam imewaachia huru watu 52 wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, baada ya kuona kwamba sheria ilikosewa kwa kuwafunga kifungo cha mwaka mmoja.
Mahakama hiyo imesema kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilipaswa kuwahukumu kifungo cha miezi mitatu tu.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Salvatory Bongole baada ya kusikiliza hoja za rufaa iliyokatwa na wafuasi hao kupitia wakili wa utetezi, Mohammed Tibanyendera.

“Mahakama hii imeona kwamba washtakiwa kukutwa na hatia ya kosa la kula njama adhabu yake siyo sahihi, nimeifutilia mbali, lakini nakubaliana na kosa la pili na la tatu wana hatia,” alisema na kuongeza:

“Adhabu ya mwaka mmoja mliyopewa naibatilisha, mtakwenda jela miezi mitatu kama sheria ya Jeshi la Polisi inavyosema au faini Shilingi  50,000.”

Jaji Bongole alisema washtakiwa hao walihukumiwa kwenda jela kutumikia kifungo cha mwaka mmoja Machi 21, 2013 mpaka sasa wametumikia zaidi ya miezi mitatu.
“Kwa kuwa wameshatumikia zaidi ya miezi mitatu, natamka kwamba nawaachia huru wote, kwa sababu adhabu yenu mmeitumikia na zaidi,” alisema Jaji Bongole.

Jaji Bongole alisema washtakiwa waliotiwa hatiani na kufungwa mwaka mmoja jela kwa makosa ya kula njama, kufanya mkusanyiko usio halali na kukaidi amri ya Polisi iliyokuwa ikiwazuia kufanya maandamano kuelekea katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kushinikiza Sheikh Ponda kuachiwa kwa dhamana ni Salum Makame na wenzake 51.

“Warufani mlipewa adhabu mbili katika kosa moja, mtu anapokula njama na kuiba, akitiwa hatiani kwa kosa la kuiba, kosa la kula njama linakufa,” alisema Jaji Bongole na kuongeza:

“Adhabu mliyopewa kwa kosa la kula njama na kukaidi amri ya Polisi haikuwa sahihi, kosa la pili nilipopitia ushahidi limethibitishwa kwamba mliandamana kwa kukaidi amri ya RPC (Kamanda wa Polisi wa Mkoa) iliyowakataza  kufanyahivyo.

“Kosa la pili na tatu nakubaliana na uamuzi wa Mahakama ya Kisutu uliowatia hatiani, kifungu namba 46 cha sheria za Polisi kilichotakiwa kutumika kuwapa adhabu hakikutumika, kifungu hicho kinatamka adhabu kwa makosa hayo ni kwenda jela miezi mitatu au faini ya Sh. 50,000.

“Kutiwa hatiani kwa kosa la kula njama na adhabu yake siyo sahihi, nimeifutilia mbali, kosa la pili na tatu nakubaliana na kutiwa hatiani, adhabu ya mwaka mmoja mliyopewa naibatilisha, mtakwenda jela miezi mitatu kama sheria ya Polisi inavyosema au faini Sh. 50,000.”

Jaji alisema: “Mlifungwa Machi 21, 2013 na Hakimu Mkazi Sundi Fimbo, mpaka sasa ni zaidi ya miezi mitatu, natamka kwamba nawaachia huru wote, mtoke gerezani sababu adhabu yenu mmeitumikia zaidi.”

Wafuasi hao walidaiwa kufanya maandamano Februari 15, mwaka huu wakishinikiza Sheikh Ponda kuachiwa kwa dhamana katika kesi ya uchochezi iliyokuwa ikimkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Victoria Nongwa.

Machi 21, mwaka huu, Mahakama hiyo iliwahukumu kwenda jela mwaka mmoja kwa makosa hayo matatu waliyokuwa wakikabiliwa likiwamo la kukaidi amri ya Polisi iliyokuwa ikiwazuia kufanya maandamano kuelekea kwa DPP ili kushinikiza kiongozi wao apewe dhamana.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Fimbo alisema kuwa katika shtaka la kula njama upande wa mashtaka ulithibitisha bila kuacha shaka kwamba washtakiwa walikutana, wakakubaliana kufanya maandamano hivyo mahakama inawatia hatiani kwa kosa hilo.

Katika shtaka la kukusanyika na kuandamana, alisema mahakama inawatia hatiani.

Kuhusu kosa la kukaidi amri halali ya polisi alisema mahakama inawatia hatiani kwa kuwa  washtakiwa walipeleka maombi ya kufanya maandamano ya amani na Polisi waliyazuia kwa sababu hawakuwa na askari wa kutosha, lakini maandamano hayo yalifanyika baada ya kutoka msikitini.

Katika kosa la kwanza aliwahukumu washitakiwa kwenda jela mwaka mmoja. Katika shtaka la pili pia aliwahukumu mwaka mmoja jela huku kosa la tatu wakihukumiwa tena kifungo cha mwaka mmoja jela.

Hakimu Fimbo alisema adhabu hizo zinatumikiwa kwa pamoja hivyo aliwahukumu washtakiwa kifungo cha mwaka mmoja jela kila mmoja.
 

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment