STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, November 26, 2013

Hapatoshi Ligi ya Mabingwa Ulaya

Arsenal watakaokuwa nyumbani Ligi ya Mabingwa Ulaya
KIVUMBI cha Ligi ya Mabingwa Ulaya kinatrajiwa kuendelea tena leo, huku kivumbi kikiwa katika pambano kati ya Borussia Dortmund itakapoikaribisha Napoli ya Italia, hiyo ikiwa ni nafasi pekee kwao kujua kama itakuwa na nafasi ya kusonga hatua ya mtoano ama la.
Kwanza inakabiliwa na majeruhi kutokana na kipigo cha 3-0 ilichokipata Jumamosi kwenye Bundesliga dhidi ya wapinzani wao wakubwa Bayern Munich, timu hiyo ya Kocha Juergen Klopp inahitaji kushinda mechi zake mbili za mwisho katika Kundi F, dhidi ya Napoli na Olympique Marseille ili kutinga hatua ya mtoano.
Matokeo yoyote kinyume na ushindi, yatamaanisha timu hiyo ambayo ilitinga fainali msimu uliopita, itakuwa imeshindwa kufikia malengo hayo.
"Tunakosa umakini na malengo," alisema kipa wa Dortmund, Roman Weidenfeller. "Tunachukua muda mrefu kumalizia gonga zetu. Tunapasiana badala ya kwenda moja kwa moja langoni."
"Bado hakuna lolote ambalo limefanyika, iwe kwenye ligi ya nyumbani ama Ulaya. Lakini mechi ya Jumanne (leo) ni muhimu sana kuliko hii dhidi ya Bayern. Tunahitaji kushinda mechi hii ya nyumbani na tunahitaji kutumia nafasi zetu kwa sababu mchezo ni kushinda kwa kufunga mabao."
Dortmund inashika nafasi ya tatu katika kundi lao ikiwa na pointi sita, tatu nyuma ya kinara Arsenal na  Napoli ambazo zina pointi tisa zikitofautiana kwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa. Marseille haina pointi yoyote baada ya kupoteza mecho zote. Napoli iliichapa timu hiyo ya Ujerumani kwa mabao 2-1 katika mechi ya kwanza iliyopigwa Septemba mwaka huu.
"Niliiambia timu yangu baada ya mechi ya Bayern kuwa ina dakika tano za kusahau machungu na kisha kujipanga upya," alisema Klopp, ambaye timu yake ipo pointi saba nyuma ya vinara Bayern katika Bundesliga.
"Tunapaswa kufikiri kuhusu mechi ijayo, kutoa maamuzi sahihi na kuwa na utayari kimichezo. Tunahitaji kujua mustakabali wa yote katika mechi na Marseille (katika mechi yetu ya mwisho)."

Majeruhi
Klopp atahitaji kufanya mabadiliko katika safu yake ya ulinzi kwa mara nyingine tena baada ya Manuel Friedrich kuwa mbadala pekee wiki iliyopita kutokana na Mats Hummels, Neven Subotic na Marcel Schmelzer, kuwa majeruhi na kuenguliwa katika michuano hiyo ya Ulaya.
Hata hivyo, kuna habari njema kutokana na beki wa kulia Lukasz Piszczek Jumamosi kurejea uwanjani baada ya kupona majeraha yaliyokuwa yakimkabili majira ya joto.

Napoli nayo yashikwa
Napoli nayo kimatokeo haikufanya vizuri baada ya kupoteza mechi zao mbili zilizopita za Serie A tena bila kufunga, awali ilikubali kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Juventus wiki mbili zilizopita na kisha Jumamosi ikanyukwa nyumbani bao 1-0 dhidi ya Parma.
Kocha Rafael Benitez alibadili kikosi chake dhidi ya Parma, sera ambazo zilizua maswali mengi katika vyombo vya habari, hivyo kushuhudia timu yake ikilala kwa bao la usiku la Antonio Cassano.
Hofu kubwa ni mshambuliaji Marek Hamsik, ambaye aliingia dakika 10 za mwisho na kuumia unyayo, hivyo ataikosa Dortmund leo.
Benitez alilalamikia mapumziko ya mechi za kimataifa. "Tumefanya makosa mengi, lakini ni vigumu kufanya vizuri kwa muda mfupi kama huo," alisema.
"Tunapoteza mipira kirahisi, tunaruhusu nafasi nyingi za kuchezewa mashambulizi ya kushtukiza na kupoteza nafasi chache za kusonga mbele kwa  Gonzalo Higuain na Goran Pandev.
"Sishangai kwa Borussia kufungwa na Bayern. Ninayaangalia zaidi matokeo yetu kuliko Borussia. Tayari tunaelekeza akili zetu katika mechi inayofuata."

Cazorla aionya Arsenal kwa Marseille
Licha ya Arsenal leo kuwa nyumbani kwenye dimba lao la Emirates ikicheza dhidi ya vibonde Olympique Marseille, haitahitaji kulala kwenye mchezo huo.
Miamba hiyo inayoongoza Kundi F ikiwa juu ya Napoli kwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa huku ikiizidi Borussia Dortmund kwa pointi sita, kama itafanikiwa kuifunga Marseille na Wajerumani hao wakashindwa kuifunga Napoli, kikosi hicho cha Arsene Wenger kitakuwa kimejihakikishia nafasi ya kucheza hatua ya mtoano.
Kiungo Santi Cazorla ameonya kutobweteka katika mechi hiyo wakati huu wakiwa bado wana safari ya kwenda Napoli, kuhitimisha safari yao ya hatua ya makundi.
"Tatizo kubwa ni kwamba, kila mmoja anafikiri itakuwa mechi rahisi kwetu kushinda," Mhispania huyo aliiambia tovuti ya Arsenal (www.arsenal.com) baada ya ushindi wa 2-0 walioupata Jumamosi dhidi ya Southampton, uliowafanya kuendelea kukaa kileleni mwa Ligi Kuu England.
"Hakuna wanalolitarajia Marseille kwa sababu hawana pointi yoyote, lakini watafanya mambo kuwa magumu kwetu. Itakuwa mechi ngumu na kama hatutakuwa makini tutashindwa kupata nafasi ya kusonga mbele.
"Tunapaswa kutambua kwamba ni mechi muhimu," alisema Cazorla. "Kama hatutapata matokeo mazuri, yatafanya mambo kuwa magumu kwetu kwani tutakapokwenda Napoli tutalazimika kushinda."
Marseille ililazimisha suluhu dhidi ya Arsenal zilipokutana Emirates miaka miwili iliyopita, lakini Klabu hiyo ya Ufaransa ina rekodi mbaya ikiwa England.
Ushindi pekee iliyopata katika mechi 11 za mashindano ilizocheza England, ulikuwa wa bao 1-0 dhidi ya Liverpool msimu wa 2007-08 katika mechi ya Ligi ya Mabingwam Ulaya hatua ya makundi na imepoteza mara sita.
Hata hivyo, Marseille itamtegemea Andre-Pierre Gignac baada ya mshambuliaji Dimitri Payet kuwa majeruhi wa goti. Mabingwa hao wa Ulaya wa 1993, pia watamkosa mshambuliaji Mghana Andre Ayew anayesumbuliwa na goti.

Basel v Chelsea, Barca na Ajax
Katika mechi nyingine itakayopigwa leo, Kundi E, Basel  itakuwa mwenyeji wa Chelsea wakati huo Steaua Bucharest ikiialika Schalke 04. Kundi G, Zenit St Petersburg itaialika Atletico Madrid  huku
FC Porto ikiwa nyumbani kuisubiri Austria Vienna.
Kundi H, Ajax Amsterdam itaisubiri  Barcelona wakati  Celtic ikiwa mwenyeji wa  AC Milan.

NIPASHE

No comments:

Post a Comment