STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, February 25, 2014

Tiko Hassan: Kimwana anayetaka mabadiliko, nidhamu Bongo Movie

Msanii Tiko Hassan katika pozi
"NAAMINI kama wasanii wa kike watajitambua na kutulia kwa kuepuka skendo na mambo ya upuuzi ni rahisi kwao kupata tenda zinazoweza kuwaingizia pato la ziada nje ya fani zao kama ilivyo kwa wanamichezo au wasanii wa kimataifa wanaotamba kwa utajiri duniani."
Ndivyo anavyosema Tiko Hassan 'Tiko' mmoja wa waigizaji nyota wa filamu nchini, akizungumzia namna anavyokerwa na baadhi ya wasanii wenzake wa kike wanavyojisahau na kujikita kwenye mambo ya ovyo kiasi cha kuchafua sifa ya sanaa na kuwafanya wasanii wote kuonekana wa ovyo.
"Kwa kweli hili jambo linakera kwa sababu jamii inatutazama kama watu tusiojiheshimu na hata wakati mwingine tunakosa nafasi ya kutumika kama mabalozi wa kutangaza bidhaa na huduma za taasisi kwa sababu ya mambo tunayofanya, imefika wakati wasanii tukabadilika," anasema.
Tiko anasema ingawa kila mtu ana uhuru wa kufanya atakalo, bado wasanii wanapaswa kuwa mstari wa kwanza kulinda maadili na nidhamu ya sanaa kwa sababu inawasaidia kuwaingizia kipato hata kama siyo cha kuridhisha, lakini bado ni ajira inayopaswa kuheshimiwa.
Mwanadada huyo aliyeanza kujihusisha na sanaa tangu akiwa Shule ya Msingi Mbagala Kizuiani kisha Al Haramain, anasema kuna haja vyombo vinavyosimamia sanaa kuwa wakali dhidi ya watu wachache wanaotaka kuwaharibia kazi.
Shabiki huyo wa Yanga, anasema anaamini vyombo kama Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) na hata Bongo Movie Unity wakiwa wakali wanaweza kufanya 'wavamizi' katika fani ya uigizaji kujiondoa wenyewe na kwenda kufanya upuuzi huo kwingine.

NANDIPHA
Tiko anayependa kula ugali kwa dagaa na bamia na wakati mwingine wali kwa kuku au kisamvu na maharage na kunywa juisi anasema licha ya kipaji cha kuzaliwa cha sanaa, lakini alijikuta akivutiwa na uigizaji kutokana na uigizaji wa Lesego Motsepe 'Nandipha' wa Isidingo the Need.
"Huyu dada ambaye kwa sasa ni marehemu alinifanya nami kuota kuja kuwa muigizaji kwa sababu nilikuwa navutiwa naye kupitia igizo lao la refu linaloendelea mpaka leo kwenye runinga la 'Isidingo the Need'," anasema.
Anasema baada ya kuonyesha makeke katika sanaa shuleni katikati ya miaka ya 2000 alijitosa jumla kwenye sanaa hiyo kupitia kundi la Shirikisho Msanii Afrika.
"Nakumbuka mwaka 2006 ndipo nilijitosa jumla kupitia Shirikisho Msanii Afrika na igizo langu la kwanza lilikuwa 'Chozi' kabla ya kufuatiwa na 'Darubini' kisha nikahamia kwenye filamu," anasema.
Anasema kazi ya kwanza kuicheza ilikuwa 'The Living Ghost' kisha kufuatiwa na utitiri wa filamu kama 'The Devil's Soul', 'Limbwata', 'Check in the Bible', 'My Son' , 'Melvin', Foolish Age na nyingine.
Mwanadada huyo anayefurahia sanaa kumbadilisha maisha yake kutoka kuwategemea wazazi mpaka kujitegemea mwenyewe na akiendesha biashara inayomuingizia pato la ziada anasema kati ya kazi zote alizocheza, filamu ya 'Limbwata' kwake ndiyo bomba  kwake.
"Limbwata, ndiyo filamu ambayo naamini nimeitendea haki, japo kazi nyingine ikiwamo  ya Melvin pia zinanisisimua," anasema.
Tiko anayeota kuja kuwa msanii wa kimataifa pamoja na kumiliki kampuni yake, mbali na uigizaji pia ni muimbaji na mjasiriamali akijihusisha na biashara ya urembo na nguo za wanawake.
Tiko Hassan
FURAHA
Tiko Hassan aliyezaliwa miaka kadhaa iliyopita jijini Dar es Salaam, anasema hakuna tukio la furaha kwake kama siku alipojifungua mwanae kipenzi aitwaye Aisha mwenye miaka nane, ambaye anadai ni kama rafiki na mfariji wake.
"Kwa kweli hili ndilo tukio la furaha kwangu. Aisha amenifanya nijisikie mwenye furaha na kwenye matukio ya huzuni hakuna linaloniliza kama nilipompoteza baba yangu mwaka 2005," anasema.
Msanii huyo aliyesomea kozi ya Uongozi ya Utalii katika Chuo cha African Tourism College, anasema kwa wasanii wa Bongo anamzimia na kumkubali sana Ahmed Salim maarufu kama 'Gabo' akidai akipewa sapoti kubwa anaweza kuwa 'nembo' ya Tanzania kwani ana kipaji na anajua kuigiza.
"Aah! Gabo hana mpinzani kwa sasa Tanzania, licha ya kuibuka siku za karibuni, lakini akiwezeshwa zaidi anaweza kuitoa kimasomaso Tanzania kwa kipaji alichoinacho na umahiri wake katika kuigiza," anasema Tiko ambaye hajaolewa ila ana mchumba anayetarajia kufunga naye ndoa.
Kuhusu sanaa ya Tanzania, Tiko anasema bado inahitaji mabadilkio makubwa, hasa wasanii wakongwe kujitolea kuwasaidia chipukizi badala ya kuwabania kwa kuamini watafunikwa.
"Pia ni lazima wasanii tupendane na kushirikiana bila kubaguana kwa nia ya kuendeleza mbele sanaa yetu na hasa katika kukabiliana na unyonyaji tunaofanyiwa," anasema.
Tiko anayependa kutumia muda wake wa mapumziko kuangalia movie, kuogelea, kulala na kupika anasema kama siyo sanaa huenda angekuwa 'Mama Ntilie' kwa sababu ya kupenda shughuli za jikoni na hasa kupikapika.
"Wallah, kama siyo kipaji cha sanaa naamini ningekuja kufanya kazi ya Mama Ntilie napenda sana kazi ya kupika," anasema.
Tiko anasema ukiondoa Mungu aliyemjalia kipaji na afya na kila kitu kinachomfanya amshukuru kila saa, pia anawashukuru mno wazazi wake, mchumba wake, wasanii wenzake, ndugu na jamaa wote waliomsaidia kwa namna moja au nyingine kumfikisha hapo alipo.
"Kwa kweli mbali na Mungu ninayemshukuru kila dakika kwani bila ya yeye nisingekuwa Tiko Hassan, pia nawashukuru mno wazazi wangu, mchumba wangu, marafiki na wote wanaoniunga mkono katika shughuli zangu ninazofanya kuanzia za sanaa na zile za ujasiriamali," anasema.

No comments:

Post a Comment