STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, April 9, 2014

Roho Mkononi VPL, Azam kutawazwa mabingwa leo?


Azam wanaoweza kutawazwa kuwa mabingwa leo
Yanga kukubali kulitema taji kilaini kwa Azam leo dhidi ya Kagera Sugar
ROHO Mkononi kwenye viwanja viwili vya Ligi Kuu Tanzania Bara zitakavyozihusisha timu mbili zinazowania ubingwa wa msimu wa 2013-2014, watetezi Yanga na Azam Fc.
Yanga watakuwa uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuwakaribisha Kagera Sugar, huku wapinzani wao watakuwa uwanja wa Mabatini Mlandizi kuvaana na wenyeji wao Ruvu Shooting.
Matokeo ya aina yoyote leo yanaweza kumtangaza bingwa mpya na hasa kama Yanga ikapoteza ubingwa na Azam kushinda dhidi ya Ruvu Shooting kutokana na mahesabu ya pointi zilivyo.
Yanga wenyewe wana pointi 49, nne nyuma ya Azam wenye pointi 53 zote zikiwa zimeshacheza mechi 23 na leo zinashuka kuhitimisha raundi ya 24.
Iwapo Azam itaendeleza rekodi ya kutopoteza mechi katika ligi hiyo kwa kuwazabua Ruvu watafikisha pointi 56 ambapo kama Yanga itapoteza mechi yake ya jiji haitaweza kuzifikia hata iweje.
Kwa maana hiyo mechi hizo mbili kwa timu hizo ni kama mtu kuishikilia roho mkononi isiweze kuitoka kutokana na umuhimu wake na presha kubwa waliyonayo Yanga kuliko Azam.
Yanga waliotoka kuvuna ushindi mnono wa mabao 5-1 dhidi ya JKT Ruvu, itakuwa na kila ulazima wa kuishinda Kagera Sugar iliyoikomalia Simba katika mechi yao iliyopita mjini Bukoba.
Kupoteza ina maana kwamba wamewavisha Azam taji hilo kwa mara ya kwanza katika historia yao tangu walipopanda Ligi Kuu mwaka 2008.
Kushinda na kisha Azam kushinda Mlandizi itaamaanisha watasubiri mechi ya Jumapili Azam wakiwafuata Mbeya City na Yanga kuifuata Oljoro mjini Arusha kuchanga tena karata zao.
Akizungumzia jana juu ya mechi hiyo, Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kiziguto, alisema wanatarajia kupata ushindani mkubwa kutoka kwa Kagera Sugar, lakini wamejipanga kupambana.
“Kagera ni timu nzuri, ila tumejipanga kupambana kushinda mechi hiyo na nyinginezo zilizobaki kwani hatuwezi kutetea ubingwa bila kwanza kushinda mechi zote,” alisema.
Alisema kutokana na ugumu wa mechi hiyo, ni muhimu mashabiki wao wakajitokeza kwa wingi kuisapoti timu yao pamoja na kuwa watulivu wanapokuwa uwanjani kuepuka vitendo vya vurugu.
Kwa upande wa Azam, Kocha Msaidizi, Kali Ongala, alisema pointi tatu ni muhimu kwao katika mechi ya leo kuendelea kubaki kileleni hadi mwisho wa ligi hiyo, hivyo kubeba taji kwa mara ya kwanza.
“Kiukweli timu ipo vizuri na tuna uhakika tutashinda mchezo huo kutokana na maandalizi tuliyofanya, wachezaji wenyewe wanajua ni kitu gani tunataka, muhimu ni kuomba Mungu," alisema.
Hata hivyo Afisa Habari wa Ruvu, Masau Bwire ametamba kwamba kikosi chao kipo tayari kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza msimu huu kuitungua Azam baada ya Simba na Yanga kushindwa.
"Tupo vyema na tunataka kuweka rekodi ya kuwa wa kwanza kuwafunga Azam, nadhani rekodi yetu kwenye uwanja wa nyumbani ipo wazi hatujapoteza mchezo Mabatini," alisema Bwire.
Naye kocha wa timu hiyo, Tom Olaba alitamba kuwa anaawaamini vijana wake watapambana dakika zote 90 kuhakikisha Ruvu wanapata ushindi ili kuzidi kusogea kwenye nafasi za juu.

No comments:

Post a Comment