WACHEKESHAJI Robert Augustino 'Kiwewe' na Tumain Martin 'Matumaini' wameamua kugeukia muziki wa Injili wakijiandaa kuachia albamu yao iitwayo 'Nimepona'.
Akizungumza na MICHARAZO hili, Kiwewe anayetamba na kipindi cha 'Ze Comedy Show' alisema kuwa albamu hiyo itakuwa na nyimbo sita na imeshakamilika ikisubiri kuachiwa mtaani.
Kiwewe alisema wameamua kumtumikia Mungu kwa kuimba kama njia ya kumshukuru kwa yote aliyowatendea tangu walipoanza kujipatia umaarufu kupitia fani ya uigizaji.
"Tumeamua kumtumia Mungu kwa njia ya huduma ya nyimbo na tunaomba mashabiki wetu watuunge mkono mara albamu hiyo itakapoingia sokoni wakati wowote kuanza sasa," alisema.
Hata hivyo Kiwewe aliweka bayana kwamba pamoja na kuimba muziki wa Injili, yeye hajaokoka kama 'patna' wake Matumaini ambaye kwa sasa ni Mlokole akisali Mito ya Baraka.
"Sijaokoka kwa sababu siyo kila aimbaye muziki wa Injili ameokoka, ila Matumaini yeye kaokoka," alisema.
Matumaini mwenyewe alisema albam,u hiyo wameirekodia katika studuio za Levon, zilizopo Kibamba jijini Dar na kuzitaja nyimbo zilizopo katika albamu hiyo kuwa ni 'Nimepona', 'Amani ya Bwana', 'Msukule', 'Nitakutangaza Bwana', 'Mungu' na 'Anaweza Yesu' na amepanda kuiachia wiki mbili zijazo.
No comments:
Post a Comment