STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, July 15, 2014

Brazili yamtimua 'Big Phil' ni baada ya aibu aliyowapa nyumbani


Scolari katika picha tofauti kabla ya kutimuliwa kocha wa Brazil
BRAZIL imemtimua kocha Luiz Felipe Scolari saa chache tu baada ya kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia ambalo walikumbana na vipigo vyao viwili vibaya zaidi katika historia yao ya michuano hiyo, moja ya magazeti yanayoongoza Brazil liliripoti jana.
Kikosi cha kocha Scolari cha Brazil kilikuwa kikipewa nafasi ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo lakini kilikumbana na kipigo cha aibu cha magoli 7-1 katika nusu fainali dhidi ya waliokuja kuwa mabingwa Ujerumani. Katika kukamilisha mwisho wao mbaya, walikumbana na kipigo kingine cha 3-0 dhidi ya Uholanzi katika mechi ya kusaka mshindi wa tatu.
Scolari, ambaye aliiongoza Brazil kutwaa taji lao la tano na la mwisho la Kombe la Dunia 2002, alisema baada ya mechi hiyo kwamba atawasilisha ripoti kwa mabosi wake katika Shirikisho la Soka la Brazil (CBF) na ni wakati huo tu hatima yake itaamuliwa.
Lakini gazeti la O Globo liliripoti jana kwamba Scolari alitimuliwa Jumapili usiku. Gazeti hilo lilisema taarifa rasmi ingetoka baadaye jana.
Hapakuwa na uthibitisho kutoka CBF, wala mshauri wa habari wa Scolari.
Scolari aliichukua timu hiyo Novemba 2012 na amepoteza mechi tano tu kati ya 29 alizokuwa madarakani. Aliiongoza Brazil kutwaa Kombe la Mabingwa wa Mabara mwaka jana kwa ushindi wa kukumbukwa wa 3-0 dhidi ya mabingwa wa dunia wa wakati huo Hispania katika mechi ya fainali.
Alikuwa ni mtu anayependwa sana Brazil kwa ucheshi wake na pia kwa wachezaji ambao humchukulia kama baba yao.
Alikuwa na sapoti ya taifa kuelekea kwenye Kombe la Dunia na kulikuwa na upinzani mdogo kwa kikosi alichoteua, jambo ambalo ni nadra sana nchini Brazil, kunakofahamika kama "taifa la makocha milioni 200."
Kama kuondoka kwake kutathibitishwa, makocha wanaopewa nafasi ya mapema kama warithi wake watakuwa ni Tite, kocha ambaye aliiongoza Corinthians kutwaa Kombe la Ligi ya Klabu Bingwa Amerika Kusini (Copa Libertadores) na Kombe la Dunia la Klabu 2012, na Muricy Ramalho, ambaye ni kocha wa sasa wa klabu ya Sao Paulo.

No comments:

Post a Comment