Simba watapona kwa Coastal |
Yusuf Chippo, Kocha wa Coastal Union (mwenye kofia) ataendeleza ubabe kwa vijana wake dhidi ya Simba leo Taifa? |
Ndanda Fc waliokaa kileleni baada ya ushindi wake wa kishindo jana dhidi ya Stand Utd |
Ushindi wa mabao 4-1 iliyopata ugenini dhidi ya Stand United ya Shinyanga imeiweka Ndanda kileleni ikiwazxidi mabingwa watetezi Azam kwa uwiano wa bao moja la kufunga.
Azam wanakamata nafasi ya pili na kufuatiwa na Mtibwa Sugar waliowatoa nishai Yanga na Marcio Maximo wao pamoja na Jaja, kisha Prisons waliowakong'ota maafande wa Ruvu Shooting wakifuatia mbele ya Mgambo JKT walioshinda jana nyumbani mjini Tanga.
Ingawa ni mapema mno kuijadili ligi kwa sasa, lakini kwa kuwa asubuhi njema huonekana asubuhi, Ndanda, Azam, Mtibwa na Prisons zimesafisha 'nyota' kwa ushindi katika mechi zao za ufunguzi, huku Mbeya City na JKT Ruvu wenyewe wakikusanya pointi moja moja.
Raundi ya kwanza ya mechi hizo za ufunguzi itakamilika leo wakati Simba na Coastal Union zitakazpovaana kwenye dimba la Taifa, huku Simba ikitaka kulipa kisasi na Coastal wakitafuta rekodi ya kuendeleza ubabe kwa vijana wa Msimbazi.
Katika mechi ya mwisho ya msimu uliopita baina ya timu hizo, Simba ilikubali kipigo cha bao 1-0, goli lililofungwa na beki kinda wa Coastal Hamad Juma dakika chache kabla ya mapumziko na kulizamisha jahazi la Wekundu wa Msimbazi waliokuwa chini ya Kocha Zdravkov Logarusic ambaye kwa sasa hayupo na timu hiyo.
Simba itawakabili Coastal wakiwa chini ya Mzambia Patrick Phiri na ikiundwa na kikosi imara, hali inayofanya pambano hilo kuwa la kusubiriwa kwa hamu kwani hata Coastal nao siyo ya kubezwa kwa usajili iliyofanywa chini ya kocha Mkenya, Yusuf Chippo.
Je ni Simba itakayolipa kisasi au Coastal itakayoendeleza ubabe katika mechi ya leo? Jibu ni baada ya dakika 90 ya mchezo huo. Tusubiri tuone.
No comments:
Post a Comment