STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, February 26, 2015

Kili Marathon kufunga barabara J'pili Moshi

http://www.blackmarathoners.org/wp-content/uploads/2013/11/Mt-Kilimanjaro-Marathon-Logo-WP.jpgNa Tariq Ticotico, Moshi
BAADHI ya barabara za mji wa Moshi zitafungwa ili kuhakikisha usalama wa wanariadha wataoshiriki mbio za kimataifa za Kilimanjaro Marathon 2015 zitakazofanyika Jumapili hii.
Mkurugenzi wa Wild Frontiers, waandaaji wa mbio hizo, John Addison, amesema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kwamba Halmashauri ya Manispaa ya Moshi imetoa kibali cha kufunga na takribani kilometa kumi za barabara kuu iendayo Dar es Salaam zitafungwa kuanzia saa 12.15 asubuhi hadi saa 2.00 asubuhi.
Barabara ya Sokoine kutokea Chuo Kikuu cha Ushirika na Biashara, (MOCU) hadi KCMC na kona barabara ya Kibosho na kutoka barabara ya Lema hadi Chuo Kikuu cha Ushirika, kupitia barabara ya Kilimanjaro, zitafunguwa kuanzia saa 12.30 asubuhi hadi saa 2.00 asubuhi.
Addison alisema kutakuwa na udhibiti utakaofanywa na askari wa usalama barabarani kwenye barabara ya kutoka YMCA hadi Mnara wa Saa, Barabara ya Boma, mzunguko wa barabara ya Arusha, Barabara ya Uru hadi ile ya Chuo Kikuu cha Ushirika, zitafungwa kuanzia saa 1.30 asubuhi hadi za 2.15 asubuhi.
“Madereva wote watakaotumia barabara hizi punde zitakapofunguliwa wanaombwa kuendesha magari yao kwa uangalifu na tahadhari kubwa kwa ajili ya usalama wa wale wanariadha ambao bado watakuwa wanaendelea na mbio hizo,” alisema.
Kampuni za kusafirisha na kuongoza watalii watakaokuwa na makujukumu ya kuwasafirisha wateja wao kutokea Mweka, zinashauriwa kuanza safari zao baada ya saa 3.00 asubuhi kwa kupitia barabara za Mweka na Sokoine kwa vile wanariadha watakuwa washapita maeneo hayo.
Waendesha magari na wale wa vyombo vingine vya moto wanashauriwa kuepuka kutumia barabara za Lema, Kilimanjaro na ile ya lango kuu la kuingilia Chuo Kikuu cha Ushirika na Biashara kadiri itakavyowezekana ili kuepuka usumbufu.
Alisema mabasi ya mikoani yanashauriwa kuanza safari zao za kutoka Moshi kuelekea Dar es Salaam baada ya saa 2.00 asubuhi, hata hivyo aliongeza kuwa yale ya kutoka Moshi kuelekea Arusha yanaweza kufanya hivyo kwa kupitia barabara ile ya mzunguko wa barabara ya kwenda Arusha.

No comments:

Post a Comment