STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, February 26, 2015

Nyambui ataka riadha ianzie shuleni

http://www.ippmedia.com/media/picture/large/NyambuiMbio(1).jpg 
Na Rahim Junior, Morogoro
MAOFISA michezo na maofisa elimu wa mikoa ya Tanzania wameombwa kushirikiana na wenyeviti wa mchezo wa riadha kufufua mchezo huo kutoka ngazi ya shule za msingi na sekondari.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Suleiman Nyambui, alisema hayo wakati akizungumza katika mkutano Mkuu wa Mwaka wa tathmini wa mashindano ya Shule za Msingi (UMITASHUMTA) na Shule za Sekondari (UMISSETA) yanayosimamiwa na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) .
Alisema mchezo huo ambao zamani uliitangaza Tanzania duniani unazidi kupoteza umaarufu kwa sababu hakuna mikakati madhubuti ya kufuatilia wanamichezo wenye vipaji kutoka ngazi ya shule za msingi hadi vyuo vikuu.
Nyambui alisema kwa mara ya mwisho mwaka jana Tanzania ilishiriki mashindano ya Jumuiya ya Madola yaliyofanyika Scotland ikiwa ni baada ya miaka 40 tangu mkimbiaji Basil John aliposhika nafasi ya nane kati ya 12 walioingia fainali za mbio za mita 1,500.
Alisema mchezo wa riadha hauna wafadhili kama ilivyo michezo ya soka lakini amejitahidi kuishawishi kampuni ya Isere Sports isaidie kuwauzia wachezaji wa riadha vifaa kwa bei ya chini.
"Tumekubaliana na Kampuni ya Isere Sports iagize na kuwauzia wetu vifaa vya michezo kwa bei ya kawaida ili wamudu kununua viatu na jezi," alisema Nyambui.
Meneja Masoko wa Isere Sports, Abbas Ally Isere, alisema ni kweli wamefikia makubaliano hayo na yeye kama Mtanzania anayehitaji vipaji vionekane atajitahidi kuhakikisha vifaa vya riadha anaviagiza na kuviuza kwa bei ya chini.
Mikoa inayotamba kutoa wanariadha wengi ni Manyara, Arusha, Mara, Mtwara, Dodoma, Mbeya, Kanda ya Ziwa na mikoa nyingine.

No comments:

Post a Comment