STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, August 19, 2016

Mtamkoma! Kessy ruksa kukipiga Jangwani msimu huu

Kessy akiwajibika kwenye mechi ya Ngao ya jamii dhidi ya Azam
Na Rahma Kimwaga
YANGA inayojiandaa kupaa kwenda zao DR Congo huenda ikawa inatabasamu kwa furaha baada ya beki waliyekuwa wakimpigania kutoka Simba, Hassan Kessy kupewa uhalali wa kuanza kuitumikia timu hiyo katika Ligi Kuu Bara msimu huu.
Kessy aliyekuwa akiwekewa zengwe na Simba, licha ya ukweli ilishamaliza naye mkataba na ilionyesha wazi kutomhitaji baada ya kumfungia mechi tano za mwishoni mwa msimu uliopita kwa kitendo cha kunmchezea rafu Edward 'Rddo' Christopher aliyekuwa akiichezea Toto Africans aliyesajiliwa Kagera Sugar kwa sasa.
Kamati ya Sheria na Haki za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)  lilipitisha jina la Kessy kuichezea Yanga sambamba na usajili wa klabu nyingine kwa msimu wa 2016-2017.
Kamati hiyo imepitisha jina la Hassan Ramadhani ‘Kesi’ kuitumikia Yanga kuanzia msimu huu 2016/17 baada ya kuona kuwa hana tatizo katika usajili badala yake madai ambayo pande husika zinaweza kudaiana wakati mchezaji anaendeleza kipaji chake.
Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Richard Sinamtwa imepitia usajili wa timu zote na kujiridhisha kwamba suala la mchezaji Hassan Kessy limeegemea kwenye madai na si usajili ambako Simba ndiye mdai kwa kumtuhumu mchezaji huyo kuwa alianza kuitumikia Young Africans kabla ya kumaliza mkataba wake Simba SC. Mkataba wake ulifika mwisho, Juni 15, 2016.
Kama ni madai Simba inaweza kuendelea kumdai Kessy au Young Africans wakati mchezaji huyo anatumika uwanjani kwa mwajiri mpya. TFF inafuatilia na kuangalia haki ya Simba namna ya kupata haki yake baada ya kuwasilisha madai kuhusu kuvunja mkataba na mwajiri wake wa zamani.
Kanuni hazimzuii mchezaji kuendelea kucheza kwa hoja ya madai badala yake suala hilo linaweza kumalizwa wakati mashindano yanaendelea. Kamati inaendelea kupitia malalamiko na pingamizi za wachezaji wengine na inatarajiwa kutoa taarifa rasmi kuhusu wachezaji wote wakati wowote kuanzia sasa.
Katika hatua nyingine Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limezionya timu shiriki za ligi hiyo kutochezesha wachezaji wa kigeni kama hawana vibali vya kuishi, kufanya kazi na leseni inayomruhusu kucheza ligi husika kwa mujibu wa sheria za nchi na kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Vibali vya kuishi na kufanya kazi vinatolewa na Idara ya Uhamiaji Tanzania (Uhamiaji) wakati leseni ya kucheza inatolewa na TFF.
Vilevile TFF imeziagiza klabu kulipia ada za ushiriki kwa kila timu; leseni za wachezaji, ada za wachezaji na ada za mikataba.
Mchezaji hatapewa leseni ya kucheza kama uongozi wa timu hautakamilisha taratibu za malipo.
TFF pia imezikumbusha timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwamba hazitapewa leseni ya mchezaji yeyote ambaye timu haikuleta mkataba wakati wa maombi ya usajili, hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 68 vipengele vya 1, 2, 3 na 8 ya Ligi Kuu ya Tanzania toleo la 2016/2017.
Kila timu inatakiwa kuleta nakala tatu za mkataba wa mchezaji, ili kamati ya katiba, sheria na hadhi za wachezaji iweze kupitia na TFF iweze kuidhinisha mikataba hiyo. Baada ya hapo timu na mchezaji, watakuja kuchukulia mikataba hiyo hapa TFF. Ni matarajio yetu kuwa kila klabu itatimiza wajibu wake ili kuondoa migogoro kati ya timu na mchezaji na mchezaji na timu. Tunategemea kupata ushirikiano.

No comments:

Post a Comment