STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, January 6, 2018

Yanga hiyooo, Simba, Azam mechi ya kisasi

Azam FC itakayovaana na Simba usiku wa leo
Simba watakaokuwa na kibarua mbele ya watetezi wa Mapinduzi, Azam FC

Yanga waliotangulia nusu fainali ya Mapinduzi usiku wa jana
RAHIM JUNIOR
WAKATI Simba usiku huu ikishuka uwanjani katika mechi ya kisasi dhidi ya Azam, watani zao usiku wa kuamkia leo wametangulia nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi wakiungana na Singida United.
Singida inayoongoza Kundi A ikiwa na alama 9 sawa na Yanga ila ikiwa na faida ya mabao ya kufungwa na kufungwa, itashuka tena uwanjani jioni ya leo kuvaana na JKU katika pambano jingine linalotarajiwa kuwa kali itakayochezwa Uwanja wa Amaan mjini Unguja.
Maafande wa JKU wataivaa Singida ikiwa inauguza kidonda cha kutunguliwa bao 1-0 na Yanga katika mechi yao iliyopita na itakuwa ikikamilisha ratiba tu kwani hata kama itaifunga Singida itafikisha pointi 7 ambazo zimeshapitwa na wapinzani wao.
Yanga ilitinga nusu fainali baada ya kuifunga Taifa Jang'ombe kwa mabao 2-0, mabao yaliyowekwa kimiani katika vipindi vyote. La kwanza likifungwa na Ibrahim Ajib dakika chache kabla ya mapumziko na jingine la Yohana Mkomola kwenye dakika ya 60 na kuifanya Yanga kukata tiketi ya kucheza nusu fainali ikiwa na michezo miwili mkononi dhidi ya Zimamoto na Singida United zitakazopigwa kati ya kesho Jumapili na Jumatatu mtawalia.
Hata hivyo Yanga na Singida zikitangulia mapema nusu fainali, wapinzani wao Simba watakuwa na kibarua kizito usiku wa leo kwa kuvaana na Azam katika mechi ya kisasi na inayorejesha kumbukumbu ya fainali ya michuano iliyopita.
Simba ilicharazwa na Azam kwa bao 1-0 katika fainali ya mwaka jana ya michuano hiyo na kuwaacha matajiri hao wa Chamazi wakibeba taji kwa mara ya tatu wakifikia rekodi ya Wekundu wa Msimbazi.
Mchezo wa leo ni vita baada ya Azam jana kulala 1-0 mbele ya URA wanaoongoza kundi lao la B na ushindi pekee ndio utakawanusuru wasiliteme taji hilo la sivyo itawaacha Simba wakiungana na Waganda kucheza hatua hiyo itakayoanza Januari 10.
Simba kupitia Kocha wake, Masudi Djuma imetamba kukata tiketi hiyo kwa sababu imepanga mwaka huu kubeba kila taji baada ya kutemeshwa taji lao la Kombe la FA na timu ya Green Warriors iliyopo Ligi Daraja la Pili (SDL).
Simba ipo nafasi ya tatu nyuma ya URA na Azam ikiwa na alama nne baada ya kupata sare moja na kushinda mchezo mwingine wa mwisho na kama itaichapa Azam, licha ya kulipa kisasi cha mwaka jana, lakini itafuzu nusu fainali.
Watetezi ambao walipoteza mchezo wao wa kwanza msimu huu na kufungwa bao la kwanza katika Mapinduzi tangu mwaka jana walipobeba taji bila kupoteza wala kufungwa bao, imetamba tiketi yao ya nusu fainali wanayo Simba na lazima wawape. Ngoja tuone itakavyokuwa baada ya kipyenga cha mwisho usiku wa leo.

No comments:

Post a Comment