STRIKA

USILIKOSE

Monday, June 25, 2012
Ngassa atamani kucheza Simba
ACHANA na Mrisho Ngassa. Mshambuliaji nyota wa timu ya Moro United iliyoshuka kwenye ligi kuu ya Bara, Benedict Ngassa, amesema anatamani kuichezea Simba.
Kama hatopata nafasi ya kucheza Simba, mabingwa wa mwaka jana, Ngassa amesema anatamani kusajiliwa Yanga.
Akizungumza na MICHARAZO, Ngassa, alisema kati ya ndoto anazoota kila siku ni ile ya kuja kuichezea ama Simba au Yanga, klabu anazozihusudu na anazoamini zitaweza kumfikisha mbali kisoka.
Ngassa, alisema yeye hatakuwa mchezaji wa kwanza nchini kuziota timu hizo kubwa, ingawa alisema ni vigumu kupata fursa hiyo kirahisi kama hufanyi vitu vya kuzivutia.
"Kwa kweli natamani kuichezea timu moja kati ya Simba au Yanga, ni klabu kubwa na zenye mafanikio makubwa nchini na zinazoweza kumfikisha mbali mchezaji kama ana malengo na kila kijana anatamani kuzichezea," alisema.
Ngassa, alisema mpaka sasa wakati usajili ukiendelea bado hajasaini kokote licha ya kufuatwa na timu kadhaa.
Ngassa ni mmoja wa nyota wa timu ya Moro iliyokuwa imerejea ligi kuu na kushuka msimu uliopita sambamba na Villa Squad na Polisi Dodoma.
Nafasi za timu hizo tatu, mbili zikiwa za uraiani, zimechukuliwa na Mgambo Shooting, Polisi Moro na Mbeya Prisons.
Niombeeni kwa Mungu, naumwa-Omar Kapera 'Mwamba'
Kapera (wa tatu kushoto waliochuchumaa) akiwa na wachezaji wenzake wa Yanga |
Hassani Kumbi: Kiungo mkabaji anayetesa na miondoko ya Mduara



Kingwendu ajipanga kuachana na soka, kisa...!
MSHAMBULIAJI nyota wa timu ya African Lyon aliyewahi kutamba na timu za Ashanti Utd na Simba, Adam Kingwande amesema anatarajiwa kupumzika kwa muda kucheza soka ili arejee darasani kusoma.
Kingwande, aliiambia MICHARAZO kama mipango yake ya kwenda darasani itatimia hivi karibuni, basi huenda asionekane tena dimbani hadi atakapomaliza masomo yake baada yaa miaka mitatu.
Mchezaji huyo aliyekuwa msaada mkubwa kwa Lyon kabla ya kuumia na kuwa nje ya dimba hadi aliporejea mwishoni mwa msimu uliopita, alisema ameona ni bora arejee darasani kusoma kisha ndipo aendelee kucheza soka.
Kingwande alisema anatarajia kwenda kusomea Sheria katika Chuo kimoja kilichopo hapa nchini na hivyo itamuwia vigumu kwake kuchanganya mambo mawili kwa wakati mmoja.
"Kaka huenda nisionekane tena dimbani kwa muda kidogo kwani natarajia kurudi darasani kusoma, si unajua soka la Bongo lilivyo kama mtu hujiwekei mipango mizuri unaweza kuumbuka mbeleni," alisema.
Mkali huyo, aliyeibuliwa na kituo cha kukuza soka la vijana cha DYOC, alisema masomo yake yatachukua muda wa miaka mitatu na hivyo kipindi chote cha masomo hayo hataweza kucheza timu yoyote labda ya chuoni tu.
Kingwande alisema mbali na chuo hicho, pia ameomba nafasi ya kusoma pia katika chuo kimoja kilichopo nje ya nchi hivyo anasikilizia kama akikubaliwa anaweza kuamua kujiunga na chuo kimojawapo kati ya hivyo.
"Nimeomba pia katika chuo kimoja nje ya nchi, lakini ningependa kusoma hapa nchini, mradi tu nitimize ndoto zangu za kuwa mwanasheria," alisema.
Mchezaji huyo anayemudu nafasi zote za mbele ikiwemo kiungo alisema anaamini kusoma kutamwezesha kulicheza soka lake kwa uhakika sambamba na kuwa na uhakika wa maisha baada ya kutundika daluga zake.
Mwisho
Theresia Ojade, mshindi wa tuzo ya TASWA anaizimia Simba



Tuesday, June 19, 2012
Waislam wadai hawahitaji upendeleo serikali, ila...!
AMIRI wa Vijana wa Dini ya Kiislam Tanzania, Sheikh Shaaban Mapeyo, amesema malalamiko wanayotoa waumini wa dini hiyo dhidi ya serikali haina maana ya waislam kutaka upendeleo bali kutaka haki na uadilifu utendwe kwa raia wote nchini.
Aidha alisisitiza kuwa msimamo wa viongozi wa dini hiyo juu ya Sensa ya mwaka huu ni ule ule wa kuigomea mpaka kipengele cha dini kilichoondolewa kirejeshwe ili kuondoa utata uliopo na kusaidia kujua idadi ya wanadini nchini.
Akiwahutubia waumini wa msikiti wa Mwenge, jijini Dar es Salaam, Sheikh Mapeyo ambye pi ni Imamu Mkuu wa msikiti huo, alisema waislam hawahitaji upendeleo wa aina yoyote, isipokuwa wanapenda kuona haki na uadilifu unatendwa kwa raia wote.
Sheikh Mapeyo alisema madai wanayoyatoa kila mara dhidi ya dhuluma na hujuma wanaofanyiwa ni kama njia ya kuikumbusha serikali ifanye shughuli zake kwa uadilifu ikiwatendea haki raia wake wote badala ya kupendelea kundi fulani na kuwapuuza wengine.
"Waislam tunapolalamika na kupiga kelele kila mara hatuna maana ya kutaka upendeleo, tunachotaka ni kuona serikali inaendesha shughuli zake za usawa, haki na uadilifu kwa vile taifa hili ni la watanzania wote," alisema.
Aliongeza, waislam wamekuwa wavumilivu kwa muda mrefu nchini licha ya kutambua kuna baadhi ya mambo hawatendewi haki, lakini kwa kupuuzwa kwao imewafanya wafikie kikomo na kuitahadharisha serikali iwe makini.
"Kwa mfano kwa muda mrefu tumekuwa tukilalamika hujuma tunayofanyiwa katika elimu, ila majuzi imebainika hatulii ovyo baada ya kubainika madudu ya matokeo ya Baraza la Taifa la Mitihani, ambapo wenyewe wamekiri makosa."
Alisema ni vema serikali ikazinduka na kuliona tatizo lililopo nchini ni kubwa kuliko wanavyofikiria, huku akisisitiza kuwa bila kuyrejeshwa kwa kipengele cha dini kwenye zoezi la Sensa waislam hawatashiriki.
"Huu ni msimamo wetu na tumeanza kuwahimiza waumini wetu kuwa kama kipengele hicho hakirejeshwi basi wasishiriki Sensa na tumeshaiandikia barua serikali juu ya msimamo huo," alisema Sheikh Mapeyo.
Alisema serikali iliwaita viongozi wa kidini mjini Dodoma kuzungumzia jambo hilo na kusisitiza hawaterejesha kipengele hicho na wao kuieleza wazi kwamba kama ni hivyo basi wapo radhi wahesabiwe watu wengine na sio waislam.
Mwisho

Mcheza filamu wa Marekani kukimbia Mount Kilimanjaro
MCHEZA sinema maarufu duniani kutoka nchini Marekani Deidre Lorenz, anatarajiwa kushiriki mbio za kila mwaka za Mount Kilimanjaro Marathon zitakazofanyika Jumapili ijayo mjini Moshi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na waratibu wa mbio hizo zilizoanzishwa na Marie France wa mji wa Bethesda, Maryland nchini Marekani mwaka 1991 na zitakazojulikana kama 7 Continental Races, muigizaji huyo wa filamu naye atakimbia katika mbio hizo.
Taarifa hiyo iliyotumwa MICHARAZO na Afisa Habari Uhusiano wa mbio hizo, Grace Soka ni kwamba mcheza sinema huyu aliyecheza sinema kama Santorini Blue, Perfect Strangers, The Great Fight, ujio wake utaitangaza Tanzania katika macho ya dunia na kuwavutia watalii.
Lorenz aliyewahi kuteuliwa mara tatu kuwania tuzo za Grammy, ataambana na wamarekani wengine na anatarajiwa kutua nchini Juni 21.
Mbio hizo za Mount Kilimanajaro zitawashirikisha wakimbiaji wengine wa kimataifa pamoja na wa nyumbani na zitakuwa za umbali wa Kilomita 42 na washindi wake wakiwemo watoto watazawadiwa zawadi mbalimbali.
Pia mbizo zitahusisha mbio za umabli wa kilometa 21, kilometa 10 na kilometa 5 kwa watoto na kwamba washiriki wake hawahitaji ujuzi wa kukimbia bali mradi mtu anayeweza kufanya hivyo.
Deidre Lorenz alizaliwa katika jiji la Oregon nchini Marekani lakini alihamia katika jiji la New York City linalijulikana kama "The Big Apple" nchini Marekani akiwa na kampuni yake ya kutengeneza sinema inayoitwa Thira Films LLS.
Lorenz alipatikana kushiriki mbio hizo katika bahati nasibu iliyochezwa wakati wa mbio za New York Marathon za mwaka jana.

Coastal Union yanasa vifaa vipya yumo Atupele
KLABU ya soka ya Coastal Union ya Tanga, imetangaza kuwanyakua wachezaji kadhaa wapya akiwemo kipa wa zamani wa Yanga na Azam, Jackson Chove.
Afisa Habari wa Coastal, Eddo Kumwembe, aliiambia MICHARAZO,
Chove ni miongoni mwa makipa wawili wapya iliyowasajili kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kumwembe alimtaja kipa mwingine iliyomnyakua ni Juma Mpongo aliyekuwa akiidakia Kiyovu Sports ya Rwanda.
Afisa Habari huyo aliwataja wachezaji wengine iliyowanasa mpaka sasa kuwa ni mshambuliaji Nsa Job toka Villa Squad, mlinzi wa kushoto wa JKT Oljoro, Othman Omary, Atupele Green aliyekuwa Yanga na nyota wa timu ya taifa ya U20.
Kumwembe aliwatraja wachezaji wengine kuwa ni Soud Mohamed kutoka Toto Afrika, Seleman Kassim 'Selembi' na Raraq Khalfan waliokuwa African Lyon.
"Hao ni baadhi ya wachezaji tuliowanyakua na tunaendelea na usajili wetu kwa ajili ya kuziba nafasi za wachezaji tisa tuliowatema katika kikosi cha msimu uliopita," alisema Kumwembe.
Aliongeza kuwa, mbali na wachezaji hao pia timu yao imeshamalizana na kocha wao wa zamani Rashid Shedu kutoka Kenya ambaye amechukua nafasi ya Jamhuri Kihwelu 'Julio' waliyeachana nae mara baada ya kuiwesha Coastal kumaliza ligi ikiwa nafasi ya tano.
"Pia tumeimarisha benchi letu la ufundi kwa kumnyakua Rashid Shedu kuziba nafasi ya Julio tuliyeachana nae," alisema.
Kumwembe alisema pia kwa sasa wanafanya mazungumzo na kiungo wa zamani wa Simba, Jerry Santo ili zweze kuichezea timu yao kwa msimu ujao.
Mwisho
Friday, June 8, 2012
Zuri Chuchu: Muimbaji wa zamani Double M anayeishi na VVU







Thursday, June 7, 2012
Mchumiatumbo atamba hana mpinzani Bongo
BONDIA wa ngumi za kulipwa wa uzito wa juu, Alphonce Joseph 'Mchumiatumbo' ametamba kuwa, haoni bondia wa kupigana nae nchini kutokana na karibu mabondia wote wa uzito wake kuwachapa na wengine kuingia mitini kukacha kupigana nae.
Aidha, amewaomba mapromota na wafadhili wa ngumi nchini kumsaidia kumtafutia mapambano ya kimataifa na mabondia wa nje ili awe kutimiza ndoto za kutwaa na kulitangaza jina lake katika anga hizo.
Akizungumza na MICHARAZO
kwenye mahojiano maalum, Mchumiatumbo alisema kutokana na kuwapiga karibu mabondia wote wa uzani wake na wengine kumkacha ulingoni anahisi hana bondia wa kupigana nchini hivyo kuwataka mabondia wa nje.
Bondia huyo aliyepigana mapambano sita na kushinda matano, manne kati ya haayo kwa KO na kupata sare moja dhidi ya Ashraf Suleiman, alisema bondia aliyekuwa akidhani angeweza kumpa upinzani Amur Zungu alishaawahi kumkacha ulingoni.
"Kwa kweli kama kila bondia ninayepigana nae naamshinda na wengine kunikacha ulingoni, sidhani kama kuna wa kupigana nami kwa sasa, hivyo nilikuwa naomba nitafutiwe michezo ya kimataifa kujitangaza zaidi na kuwania mikanda," alisema.
Bingwa huyo wa zamani wa Mkoa wa Dar es Salaam wa ngumi za ridhaa, alisema mabondia wengi wa Tanzania wanaishia kutamba nchini tu kwa vile mapromota na waandaaji wa michezo ya ngumi hawawatafutii michezo ya kimataifa kama nchi nyingine.
Mara ya mwisho Mchumiatumbo kupata ushindi ni wiki mbili zilizopita alipomtwanga kwa KO Bahati Mwafyale katika pambano lililofanyika kwenye ukumbi wa DDC Keko.
Madega awaonya Yanga kuhusu uchaguzi

Bingwa wa karate aililia serikali
BINGWA wa mchezo wa Karate kwa nchi za Afrika Mashariki ngazi ya klabu, Sensei Mikidadi Kilindo, ameiomba serikali iutupie macho mchezo huo na kuupa sapoti kama ilivyo kwa michezo mingine ili kuuhamasisha nchini.
Aidha, Kilindo amedai kuwa kutopewa kipaumbele kwa mchezo huo ndio kilichomfanya mara zote awe anaenda na kurudi na medali bila hata kutangazwa au kufahamika kwa wananchi kitu kinachomsikitisha.
Akizungumza na MICHARAZO
, Sensei Kilindo alisema licha ya mchezo huo kuwa na manufaa makubwa kwa taifa na jamii kwa ujumla umekuwa haupewi kipaumbele kama michezo mingine.
Alisema kutokana na hali hiyo ni vema serikali na wadau wa michezo kuutupia macho na kuusaidia ili utangazike na kutumiwa kuiletea sifa Tanzania baada ya michezo mingine kushindwa kufanya hivyo.
Bingwa huyo wa miaka minne mfululizo wa Afrika Mashariki tangu 2008 alisema, kutopewa kipaumbele kwa karate ndiko kunakofanya hata wachezaji wanaoenda kuitangaza nchi wasifahamike warudipo na ushindi.
"Mimi nimerudi hivi karibuni na medali ya dhahabu baada ya kuwa mshindi wa kwanza Afrika Mashariki, hii ni mara ya nne mfululizo, ila hakuna anayejua wala kiongozi aliyewahi kunipokea na kunipongeza inauma sana," alisema.
Pia Kilindo alisema ukimya unaofanywa na viongozi wa Chama cha Karate nchini, TASHOKA katika kuutangaza mchezo huo ni tatizo linalofanya usisikike licha ya mafanikio yake kwa ngazi ya klabu.
Alisema ni vema TASHOKA ikafanya utaratibu wa kuandaa michuano ya taifa angalau mara mbili kwa mwaka itakayoshirikisha klabu mbalimbali nchini kwa lengo la kuuhamasisha na kuutangaza mchezo huo.
Zuri Chuchu Anapenda Kuishi bwana!
Yanga, Simba 'jino kwa jino' kisa Kelvin Yondani


Wednesday, June 6, 2012
Mwenyekiti Villa Squad ajiuzulu, kisa...!
MAKAMU Mwenyekiti wa klabu ya Villa Sqaud aliyekuwa pia akikaimu nafasi ya Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ramadhani Uledi ametangaza kujiuzulu kuiongoza klabu hiyo kwa kile alichodai kutaka kulinda heshima yake.
Habari za kuaminika toka katika klabu hiyo iliyoshuka daraja toka Ligi Kuu na yenye maskani yake eneo la Magomeni Mapipa, jijini Dar na kuthibitishwa na Uledi mwenyewe zinasema mwenyekiti huyo ameamua kubwaga manyanga tangu jana.
Sababu zilizomfanya Uledi ajiondoe uongozini ni kutokana na kusakamwa na wanachama na kutengwa na viongozi wenzake baada ya kushindwa kushindwa kuinusuru Villa Squad isishuke daraja.
Chanzo cha habari cha awali kilisema kutokana na shinikizo kubwa la wanachama hao, Uledi aliamua kubwaga manyanga akiandika barua ya kujitoa madarakani.
Hata hivyo MICHARAZO lilipowasiliana na Uledi kutaka kuthibitisha taarifa hizo, alikiri juu ya kujiuzulu kwake, akidai amefanya hivyo ili kulinda heshima yake kutokana na kuona hali si shwari ndani ya klabu yao.
Uledi, alisema tangu alipochaguliwa hakuwahi kupata ushirikiano wa kutosha kwa viongozi na wanachama, ila aliichukulia hali hiyo kama changamoto wake, lakini kwa hali inavyozidi kwenda mrama klabu kwao ameona bora ajiengue ili Villa itulie.
"Ni kweli nimejiuzulu kutokana na hali ya mambo iliyopo klabuni, pia nahofia kuvunjiwa heshima, hivyo nimewaachia wanachama klabu yao, ingawa bado nitaendelea kuwa ndani ya timu hiyo kwa hali na mali kama mwanachama hai," alisema.
Uledi, aliongeza anadhani chokochoko zote zilizopo Villa Squad kwa sasa zimetokana na timu hiyo kushindwa kubaki ligi kuu, japo alidai yapo mambo mengi yaliyochangia timu hiyo kutohimili ushindani hasa kutokana na hali mbaya ya kifedha iliyokuwa nayo.
Mwenyekiti huyo na wenzake walichaguliwa kwenye uchaguzi mkuu uliokuwa umejaa mizengwe Juni 25 mwaka jana, huku nafasi ya Mwenyekiti na wajumbe watatu zikiwa wazi baada ya Kamati ya Uchaguzi wa TFF, kuwaengua waliokuwa wagombea wake kwa kukosa sifa za kuwania nafasi hizo ikiwemo suala la elimu zao.
Muziki wa Dansi walilia nafasi redioni, runingani


Uchaguzi Mkuu Yanga kumekucha, wanawake waitwa Jangwani
WAKATI zoezi la uchukuaji na urudishaji fomu kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa klabu ya Yanga ukitarajiwa kufungwa rasmi leo saa 10:00 jioni, wanachama vibopa wa klabu hiyo wamejitokeza kuwania uongozi na kuonyesha namna gani Jangwani walivyopania kufanya mabadiliko ya kuondokana na viongozi 'ombaomba'.
Miongoni mwa waliojitokeza kwa jana kuchukua fomu za kuwania madarakani katika uchaguzi huo utakaofanyika Julai 15 ni pamoja na Yono Kevella wa Yono Auction Mart, Muzzammil Katunzi na Mussa Katabalo wanaowania nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo.
Wanachama wengine waliochukua fomu jana kuwania ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni Eliakim Mmaswi, Lameck Nyambaya, Ahmed Gao na wachezaji nyota wa zamani wa klabu hiyo ambao ni Edgar Fongo, Ramadhani Kampira, Ally Mayai na Aaron Nyanda.
Uchaguzi mdogo wa Yanga unatarajiwa kufanyika Julai 15, hatua inayotokana na idadi kubwa ya viongozi waliokuwa madarakani hapo awali kutangaza kujizulu hivi karibuni, akiwemo Lloyd Nchunga aliyekuwa akishikilia nafasi ya uenyekiti.
Tofauti na wagombea wengine, Katunzi na Katabalo wao walichukuliwa fomu na wazee wa klabu hiyo ambao wako chini ya mwenyekiti wao Jabir Katundu na katibu, Ibrahim Akilimali.
Akimkabidhi fomu Katunzi, Akilimali alisema kuwa lengo la kumtaka mwanachama huyo wa Yanga kugombea ni kuimarisha safu yao ya uongozi ambayo itakuja na jukumu moja tu la kuiendeleza Yanga na kuokoa jahazi lao ambalo anaamini kwamba lilikuwa likizama.
Akilimali alisema kuwa Yanga inahitaji wanachama wenye uwezo wa kuisaidia timu wakati wowote ili ifanye vizuri na kurejesha furaha kwa wanachama wao.
"Hatuhitaji waomba dagaa, tunataka kiongozi mwenye uwezo ambapo inapohitajika Sh. 300,000, yeye atatoa Sh. 600,000," alisema Akilimali.
Hadi kufikia jana, waliochukua fomu kuwania kutwaa mikoba ya Nchunga ni pamoja na John Lambele, huku Ayuob Nyenzi ambaye katika uchaguzi uliopita alijitoa kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti, akichukua fomu ya kuomba kuchaguliwa kwenye cheo hicho.
Wengine waliochukua fomu wakiwania nafasi za ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga ni Jumanne Mwamwenya, Peter Haule, Gaudecius Ishengoma, Abdallah Sheria, Saleh Abdallah, Abdallah Binkleb na Muhingo Rweyemamu.
Isack Chanzi amejitokeza kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti ambayo Davis Mosha alijiuzulu mapema mwaka jana baada ya kudai kwamba ameshindwa kutimiza malengo yake kwa kukosa ushirikiano kutoka kwa viongozi wenzake.
Uchaguzi huo unasimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo iliyoko chini ya Jaji Mstaafu John Mkwawa.
Hata hivyo mpaka sasa hakuna mwanachama yeyote wa kike wa klabu hiyo aliyejitokeza kuwania uongozi, hali iliyofanya kamati hiyo kutoa wito kwa wanachama hao kujitokeza kwani milango i wazi kwa wote.

John Kitime ajitosa kwenye utunzi wa vitabu, aja na 'vunja mbavu'
MWANAMUZIKI mkongwe wa muziki wa dansi nchini, John Kitime, amejitosa kwenye utunzi wa vitabu, ambapo kwa sasa yuko hatua za mwisho kukamilisha kitabu chake cha kwanza cha 'vunja mbavu' kiitwacho 'Kucheka ni Muhimu'.
Akizungumza na MICHARAZO
jana, Kitime ambaye ni mwanamuziki wa bendi ya Kilimanjaro 'Wana Njenje na pia ni mmoja wa wanakamati ya kutetea muziki wa dansi nchini, alisema amepata wazo la kuandika kitabu hicho kutokana na kipaji cha uchekeshaji alichonacho.
Kitime ambaye wakati mwingine huwa jaji wa shindano la kusaka vipaji vya kuimba la Bongo Star Search, alisema kitabu hicho kwa sasa kipo katika hatua ya uhariri kabla ya kuanza mipango ya kukichapisha na kukisambaza ili kuwapa burudani wapenzi wa vunja mbavu.
"Nipo katika hatua ya mwisho ya kumalizia kitabu changu cha kwanza kiitwacho 'Kucheka ni Muhimu', nadhani muda si mrefu mhakato wake wa kukitoa utafanyika na kuwapa burudani Watanzania," alisema.
Aliongeza mbali na kitabu hicho pia ameshaandika vitabu vingine viwili kimoja kiitwacho 'Kilimanjaro Band' ambacho kitakuwa maalum kwa ajili ya kuzungumzia historia ya bendi hiyo ilitoka, ilipo na inapoenda pamoja na wasifu wa wanamuziki wake.
"Kitabu kingine cha tatu ni cha 'Haki Miliki'. Nimeamua kuandika hiki kwa nia ya kuwazindua wasanii kufahamu haki zao katika miliki ya kazi zao," alisema mkongwe huo.
Kitime anakuwa mwanamuziki wa pili mkongwe kujitosa kwenye fani ya uandishi vitabu, baada ya Tshimanga Kalala Assosa, aliyetunga kitabu cha 'Jifunze Lingala' ambacho kinaendelea kutamba sokoni kwa sasa huku akiandaa kingine cha wasifu wake.

Nassib, Majia kuwania ubingwa wa TPBO
MABONDIA machachari wa ngumi za kulipwa nchini, Nassib Ramadhani na Fadhili Majia wanatarajiwa kupanda ulingoni Juni 9 kuwania taji la taifa la Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO).
Pambano hilo la uzani wa Super Fly (kilo 52) litafanyika kwenye ukumbi wa Friend's Corner, Manzese na litasindikizwa na michezo kadhaa ya utangulizi.
Rais wa TPBO, Yasin Abdallah 'Ustaadh', aliiambia MICHARAZO jana kuwa pambano hilo limeandaliwa na promota Kaike Siraju na kwamba maandalizi yanaendelea vema.
Ustaadh alisema tayari mabondia wote wanaendelea kujifua tayari kwa pambano hilo litakalokuwa la raundi 10 ambapo siku moja ya kupanda ulingoni watapimwa afya na uzito wao.
"Mabondia wetu mahiri kabisa nchini, Nassib Ramadhani na Fadhili Majia wanatarajiwa kupigana kuwania ubingwa wa TPBO uzani wa Super Fly, litakalofanyika siku ya Jumamosi kwenye ukumbi wa Friend's Corner," alisema.
Katika kuzuia vitendo vyovyote vya kihuni, Ustaadh alisema TPBO imejipanga kuhakikisha ulinzi madhubuti katika pambano hilo kwa kuanza kuwasiliana na mkuu wa polisi kituo cha urafiki ili kuwasaidia siku hiyo.
"Tayari tumeshamuandikia barua mkuu wa kituo cha Polisi cha Urafiki, Afande Paparika, ili kutupa ulinzi wa kutosha siku ya pambano," alisema.
Ustaadh alisema imani yake pambano hilo litawasisimua wengi kutokana na upinzani mkali uliopo baina ya mabondia hao na wale watakapambana katika michezo ya utangulizi siku hiyo na kuwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi.
Bibi Cheka, Dogo Aslay kutambulishwa Kanda ya Ziwa
WASANII wanaokuja juu katika muziki wa kizazi kipya nchini, Asilahi Is'haka 'Dogo Aslay' na Cheka Hija a.k.a 'Bibi Cheka' wanatarajiwa kwenda kutambulishwa rasmi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa wakisindikizwa na wasanii kibao nyota.
Meneja wa wasanii hao, Said Hassani 'Mkubwa Fella' aliiambia MICHARAZO
kwamba wasanii hao wataenda kutambuliwa katika mikoa ya Mwanza na Mara katika maonyesho yatakayofanyika mwishoni mwa wiki hii.
Fella alisema wasanii watakaoenda kuwasindikiza Bibi Cheka anayetamba na wimbo wake wa 'Ni Wewe' alioimba na Mheshimiwa Temba, na Dogo Aslay aliyeachia ngoma mpya ya 'Umbea', ni pamoja na Ferooz, Easy Man, kundi la TMK Wanaume Family na wengine.
"Mkubwa tunatarajia kwenda mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa ajili ya maonyesho maalum ya kuwatambulisha Dogo Aslay na Bibi Cheka, shoo hizo zitakuwa tatu mfululizo zikianza Juni 8 mpaka 10 na watasindikizwa na 'vichwa' kibao," alisema Fella.
Aliongeza kuwa maonyesho yao mawili ya awali yatafanyika jijini Mwanza kabla ya kumalizia burudani yao mkoani Mara na iwapo watapata fursa zaidi wanaweza kuhamishia utambulisho huo mkoani Shinyanga kabla ya kurejea Dar es Salaam.
Alisema mbali na 'Ni Wewe', Bibi Cheka msanii wa muziki wa kizazi kipya mwenye umri mkubwa kuliko wote nchini, atatambulisha wimbo wake mwingine mpya aliouimba kwa kushirikiana tena na Mheshimiwa Temba uitwao 'Mario'.

Warembo Miss Bagamoyo kusaka vipaji J'pili Dar
WAREMBO tisa wanaojiandaa na shindano la urembo la 'Redd's Miss Bagamoyo 2012' wanatarajiwa kuonyeshana kazi katika mchuano wa kusaka kipaji 'Miss Talent' Jumapili ijayo.
Mratibu wa shindano hilo, Awetu Salim, alisema shindano hilo la vipaji litafanyika kwenye ukumbi wa Club Masai, Kinondoni kabla ya warembo hao kuelekea mjini Bagamoyo kuwania taji la urembo la mji huo litakalofanyika Juni 15.
Alisema warembo hao wanaoendelea na mazoezi kwenye ukumbi wa Club Masai chini ya mkufunzi wao, Sadah Salim wameanza kutambiana kila mmoja akidai ana kipaji kitakachompa ushindi kabla ya kwenda kutwaa taji la urembo.
"Warembo wetu wanaendelea vizuri na mazoezi yetu na Jumapili wanatarajia kuchuana kwenye shindano la vipaji, litakalofanyikia kwenye ukumbi wa Club Masai na siku chache baadae wataelekea Bagamoyo kuwania taji la urembo litakalofanyika Juni 15 kwenye ukumbi wa TaSUBA," alisema.
Awetu aliwataja warembo hao kuwa ni Zuhura Abdallah, Veronica James, Rose Lucas, Beatrice Bahaya, Diana Exavery, Nancy, Flora, Yvonne Steven na Celline Wangusu.
Aidha, Awetu alishukuru kuongezeka kwa wadhamini zaidi katika shindano lao ambapo aliitaja kiwanda cha mvinyo cha Dodoma Wines kuwa ni miongoni mwa wadhamini wapya waliojitosa kuwapiga tafu.
Mratibu huyo aliongeza kuwa upande wa burudani katika shindano lao watapambwa na bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' na mshehereshaji wa shughuli hiyo anatarajiwa kuwa Khadija Shaibu 'Dida wa G'.
Aurora afariki, azikwa Dar atakumbukwa kwa mengi

Monday, June 4, 2012
Kitale: 'Teja' la kwenye runinga lisiloujua 'unga'





Drogba aimwagia sifa Taifa Stars, achekelea kuwatungua


Wazee wa Ngwasuma kutumbuiza Miss Kigamboni


Masai Nyota Mbofu aachia Rungu na Mukuki
MCHEKESHAJI maarufu nchini, Gilliad Severine 'Masai Nyota Mbofu', ameachia wimbo mpya uitwao 'Rungu na Mukuki' sambamba na video yake akishirikiana na wasanii wa kundi la Vichwa la Zambia, Simple K na G4.
Tayari wimbo na video hiyo imeshaanza kurushwa hewani wakati mwenyewe akijiandaa kupakua kazi nyingine mpya.
Akizungumza na MICHARAZO, Masai Nyota Mbofu, alisema wimbo huo ameurekodia nchini Zambia katika studio za Hez Sound chini ya Prodyuza, Acknex na video yake amefyatulia nchini humo na kuja kuimalizia Tanzania.
Msanii huyo, alisema kazi hiyo mpya ni salamu kwa mashabiki wake waliomzoea kumuona katika filamu na komedi tu, kwamba kwenye muziki naye yumo.
Masai Nyota Mbofu, alisema wakati wimbo na video hiyo ikiendelea kutamba ameanza kuandaa wimbo mipango ya kutoa kazi nyingine kwa lengo la kuja kufyatua albamu hapo baadae.
"Wakati Rungu na Mukuki, ikiendelea kukimbiza kwa fideo na radio, tayari nimenza kuandaa kazi nyingine nataka onyesha mashabiki angu kwamba mi nawesa," alisema Masai kwa kiswahili kibovu cha kikomedi.
Mkali huyo aliyeanza kutamba kwenye michezo ya runinga akiwa na kikundi cha Jakaya Theatre kabla ya kuibukia kwenye filamu chini ya kampuni ya Al Riyamy Production.
Baadhi ya kazi zilizowahi kumpa ujiko msanii huyo ni Iny'e Plus, 'Iny'e Gwedegwede', 'Vumba Vimejaa', 'Pedeshee' na sasa anatamba na kipindi cha Vituko Show.

Mosha awachomolea wazee Yanga, fomu zachangamkiwa

Simba noma, yabebe mzigo wa matibabu ya akina Boban

Noela ndiye Miss Tabata 2012
Subscribe to:
Posts (Atom)