STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, June 16, 2013

Safari ya Tanzania kwenda Brazili yafikia mwisho yalala 4-2 kwa Ivory Coast Taifa

Thomas Ulimwengu akimtoka Bamba Seleman katika pambano lililoisha jioni hii (Picha:Bin Zubeiry)

SAFARI ya Tanzania katika mbio za kuwania kucheza Fainali za Kombe la Dunia 2014, zimefikia ukingoni baada ya jioni hii timu ya taifa, Taifa Stars kukubali kipigo cha mabao 4-2 mbele ya Ivory Coast katika pambano kali la kundi C.
Stars ilikuwa ikihitaji ushindi ili kuweka hai matumaini yake ya kuingia hatua ya mtoano wa Top 10, pamoja na kuonyesha kiwango kikubwa, ilishindwa kufurukuta kwa vinara hao wa ubora wa soka Afrika na kulala.
Ushindi huo uliopatikana kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam umeifanya Ivory Coast kufuzu hatua hiyo ya mtoano wa timu bora 10 kwa kufikisha pointi 13 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote ya kundi hilo.
Stars ilianza pambano hilo kwa bao lilitupiwa kambani na kiungo Amri Kiemba dakika ya kwanza ya mchezo kabla ya Ivory Coast kusawazisha dakika ya 13 kupitia Lacina  Troure.
Kiungo mahiri wa Manchester City Yaya Toure aliifungia Ivory Coast bao la pili kwa mpira wa adhabu ndogo katika dakika ya 23 ambalo lilirudishwa na Thomas Ulimwengu dakika ya 34 akiunganisha krosi ya Shomar Kapombe iliyoguswa na Amri Kiemba.
Dakika moja kabla ya mapumziko, Yaya Toure aliiandikia tena Ivory Coast bao la tatu kwa mkwaju wa penati baada ya beki Erasto Nyoni kumwangusha Gervinho na kufanya hadi mapumziko matokeo kuwa mabao 3-2.
Kipindi cha pili, Tanzania ilionyesha kama ingeweza kurudisha bao kwa kasi iliyoingia nayo na kufanya kosa kosa kadhaa kabla ya mtokea benchi, Wilfred Bony kuiandikia wageni bao la nne dakika ya 74.
Bao hilo liliwakatisha tamaa mashabiki waliojitokeza kwa wingi uwanja wa Taifa na kuanza kutoka uwanjani kwa kuamini safari ya timu yao imefikia mwisho licha ya kusaliwa na mechi ya kukamilisha ratiba dhidi ya 'vibonde' Gambia ambao jana walilala mabao 2-0 mbele ya Morocco.

No comments:

Post a Comment