Julio kwenye kijitabu akiwa na makocha wenzake kwenye mazoezi ya Simba uwanja wa Kines hivi karibuni |
Kwa mujibu wa habari zilizochapishwa na gazeti la NIPASHE ni kwamba maamuzi ya kutimuliwa kwa Julio kunatokana na kumaliza mkataba wake wa muda mfupi na tayari maamuzi yameshapitishwa na Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo ili nafasi yake ichukuliwe na Seleman Matola.
Mmoja wa vigogo wa Simba aliyenukuliwa na gazeti hilo alisema kuwa tayari maamuzi ya kuachana na Julio yameshatolewa na nafasi yake itachukuliwa na kiungo na nahodha wa zamani wa timu hiyo, Matola.
Kigogo huyo alisema vilevile kuwa katika kikao hicho, watajadili maandalizi na kupanga siku ya kufanyika kwa mkutano mkuu wa mwaka wa klabu hiyo unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao.
"Sasa presha imehamia kwa Julio ambaye hatma yake haijulikani ndani ya Simba, lakini kilichopo ni kama ilivyokuwa kwa Kaseja," alisema kigogo huyo.
Julio alipotafutwa kuelezea hatma yake, alisema yuko kwenye kelele na atafutwe baadaye ambapo hakupatikana tena kupitia simu yake ya mkononi.
Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, aliliambia gazeti hilo kuwa ni kweli kesho kamati ya utendaji itakutana lakini kubwa watakalojadili ni kupanga maandalizi ya wiki ya Simba.
Mtawala alisema kuwa kikao hicho kitabariki shughuli zote za kijamii zilizopangwa kufanyika na kumalizika kwa tukio la kutambulishwa kwa wachezaji wapya wa Simba katika siku ijulikanayo kama 'Simba Day'.
Alieleza pia zoezi la usajili wa wachezaji wapya limeenda kwa umakini na kwa zaidi ya asilimia 80 wamekamilisha mchakato huo.
Alisema kabla ya kuanza kwa msimu mpya, timu hiyo inatarajia kuweka kambi nje ya jiji la kucheza mechi za kirafiki zaidi ya tatu kwa ajili ya kuwaandaa na kuwaweka tayari kukabiliana na ushindani katika msimu ujao wa ligi.
Simba sasa inaendelea na mazoezi chini ya kocha wake mkuu, Abdallah Kibaden 'King' wakati Matola akiendelea kuisimamia timu ya vijana (Simba B).
No comments:
Post a Comment