TIMU ya soka ya Masoko Veterani imefanikiwa kutinga fainali za michuano ya kuwania Ubingwa wa Jimbo la Kilwa Kusini 'Mbunge Cup' kwa kuidonyoa Kilwa Kisiwani kwa bao 1-0 katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa jioni ya jana kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari, Kilwa mkoani Lindi.
Bao hilo lililotimiza ahadi ya kocha wa Masoko Veterani, Abdallah Ahmad kwamba wangeilaza timu hiyo ya nyumbani kwao, lilitupiwa kimiani kwa kichwa na Said Mohammed aiyemalizia kazi nzuri iliyofanywa na Salum Teru.
Kocha huyo aliahidi mara baada ya timu yake kutinga hatua ya nusu fainali kwamba wangeinyuka Kisiwan anakotokea yeye na kutinga fainali ili kutimiza lengo la kuibuka mabingwa wa michuano hiyo iliyoandaliwa na kudhaminiwa na Mbunge wa Kilwa Kusini maarufu kama Bwege.
Katika pambano hilo la jana lililokuwa lenye upinzani na kosa kosa karibu muda wote, Masoko Veterani iliwakosa nyota wake kadhaa kama Shaaban Kassali na Yusuph Polisi waliopumzishwa na kocha wao ili kuwa tayari kwa mechi ya fainali itakayochezwa Jumamosi kati yao na mshindi wa mechi ya leo ya nusu fainali ya pili.
Nusu fainali hiyo ya pili itazikutanisha timu za Fresh Nigger dhidi ya Transpoters ambapo wadau wa soka wanaofuatilia michuano hiyo wametabiri litakuwa pambano kali zaidi ya lile la jana.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, kocha msaidizi wa Masoko, Cool Mudi, aliwaomba mashabiki wa timu yao kujitokeza kwa wingi kwenye mchezo wa fainali akiamini kwamba hakuna cha kuwazuia kutawazwa kuwa mabingwa wa michuano hiyo iliyoshirikia timu zaidi ya 10 kabla ya kufika hapo ilipo.
No comments:
Post a Comment