STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, August 9, 2013

Ashanti Utd yatambaa Yanga kitu gani bwana watatuona Taifa!

Kocha wa Ashanti United, Mbaraka Hassani akiwa na wachezaji wake jijini Dar kabla ya kwenda Kigoma kuweka kambi
KLABU ya soka ya Ashanti United imetamba kuwa licha ya kupangwa kuanza mechi zake za Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya watetezi Yanga. bado hawana mchecheto na kutamba kuwa wapinzani wao wajiandae kuaibika uwanja wa Taifa.
Ashanti iliyorejea katika ligi hiyo toka Daraja la Kwanza, imepangwa kuanza na Yanga katika mechi ya fungua dimba mechi itakayochezwa kwenye uwanja wa Taifa, kabla ya kuwafuata 'Maafande' wa Mgambo JKT Mkwakwani Tanga mechi inayofuata.
Akizungumza kwa njia ya simu toka Kigoma walipoweka kambi ya timu yao, Kocha Mkuu wa Ashanti Mbaraka Hassan alisema ingawa Yanga ni timu kubwa na iliyosheheni wachezaji wenye majina makubwa nchini na Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati bado hawana hofu nao katika pambano lao la kufungua dimba kwa vile wanajiamini wanaweza soka.
Hassan alisema anawaamini vijana wake wenye vipaji na kiu ya mafanikio wataidhibiti Yanga katika mechi hiyo na hata nyingine za ligi kuu dhidi ya wapinzani wao wengine.
"Tunaendelea vyema na kambi yetu kwa lengo la kuhakikisha tunaianza vyema ligi na hasa mechi yetu dhidi ya Yanga. Wapinzani wetu ni timu kubwa na yenye wachezaji nyota Afrika Mashariki, lakini hatuna mchecheto nikitegemea vijana wangu kufanya kweli katika mechi hiyo na nyingine za ligi," alisema.
Kocha huyo alisema kikosi chao kinaundwa na wachezaji mchanganyiko kwa maana ya vijana na wazoefu hata kama hawana majina makubwa, lakini wenye kiu ya kufika mbali kisoka na wanaamini kwamba wataipigania Ashanti kuweza kurejesha makali yake ya nyuma ilipozitia tumbo joto vigogo walipoipanda daraja kwa mara ya kwanza mwaka 2004 kabla ya kushuka 2007.
Aliongea kuwa, kupelekwa kwa kambi ya mazoezi mjini Kigoma kwao benchi la ufundi ni faraja kubwa kwa vile inawapa nafasi wachezaji kuwa pamoja kwa muda mrefu bila kusumbuliwa na familia zao kama kambi hiyo ingekuwa Dar au miji ya karibu.
Alisema mpaka sasa hakuna majeruhi yeyote katika kikosi chao na kwamba kwa sasa wanajipanga kwa mechi mbili watakazocheza wiki ijayo kabla ya kuanza safari ya kurejea Dar kukabiliana na Yanga.

No comments:

Post a Comment