LONDON, Uingereza
LIVERPOOL haifungwi kimkataba
kumuuza Luis Suarez, kwa mujibu wa mwenyekiti wa chama cha wachezaji wa kulipwa
(PFA), Gordon Taylor.
Suarez anaamini kwamba ana
makubaliano na klabu hiyo ambayo yatamruhusu kujiunga na klabu inayoshiriki
Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, kama wataletewa ofa inayozidi paundi milioni 40.
Klabu hiyo ya Anfield
imekataa ofa ya paundi milioni 40 na ziada ya paundi 1 kutoka kwa Arsenal, na
Taylor amesema Liverpool walichoafiki ni kwamba watafanya tu mazungumzo na
klabu husika kama ofa hiyo italetwa.
Taylor aliiambia Press
Association: "Kama una kipengele cha kuvunjia mkataba ni lazima kieleze
wazi, lakini hapa (kwa Suarez) ni tofauti kwa sababu kinasema kama Liverpool
itashindwa kufuzu Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya na kama kuna ofa ya angalau paundi
milioni 40 pande husika zitakaa mezani kujadili mambo lakini hakisemi kama
klabu ni lazima imuuze.
"Iko wazi kwamba ofa ya
paundi milioni 40 ndiyo kiwango awali cha kuanza mazungumzo, lakini inakuwa
ngumu sana kwenye vipengele kama hivyo.
"Kuna kipengele cha
'maelewano ya kiungwana' katika suala 'siriasi' la mazungumzo ya uhamisho
lakini siwezi kusema kinaibana Liverpool kwamba ni lazima imuuze.
"Luis ni mmoja wa memba
wetu na tunataka kutoa sapoti yetu, hata hivyo, huenda anadhani kwamba ofa kama
hiyo inaweza kulazimisha uhamisho."
Taylor pia alisema kwamba PFA
itazungumza na Suarez na Liverpool katika jaribio la kulimaliza tatizo hilo.
Aliongeza: "Kwa sasa
mambo hayako poa na sidhani kama ni hali nzuri kwa kila upande mchezaji au
klabu zinazohusika.
"Hamna manufaa na ndiyo
maana naona kwamba ni lazima tufanya kila tuwezalo tukae mezani na kuona kama
kuna mazingira ya kufikiria uhamisho lakini kipengele kilichopo hakielezi wazi
kwa asilimia 100.
"Tunawasiliana na pande
zote kujaribu kuona kama suluhu itapatikana ambayo itazinufaisha pande
zote."
No comments:
Post a Comment