STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, August 9, 2013

Twanga Pepeta kumtambulisha Ige Moyaba, warembo wa Miss Ilala kesho


BENDI ya muziki wa dansi ya African Stars 'Twanga Pepeta' kesho itawatambulisha wanamuziki wake wapya akiwemo muimbaji wao wa zamani Ige Moyaba na warembo watakaoshiriki Miss Ilala 2013.
Utambulisho huo ambao  ni sehemu ya shamrashamra za sikukuu ya Idd el Fitri utafanyika katika ukumbi  wa Mango Garden, Kinondoni.
Mratibu wa onyesho hilo, Joseph Kapinga alisema maandalizi yote ya onyesho hilo yamekamilika.
"Ige Moyaba aliyekuwa Ufaransa amewasili nchini tangu juzi usiku na alishajiunga na wanamuziki wenzake," Kapinga alisema.
Kapinga alisema warembo watakaoshiriki shindano la kumtafuta Miss Ilala pia watatambulishwa kwenye onyesho hilo linaloandaliwa na Bob Entertainment na Keen Arts chini ya udhamini wa Konyagi, Freddito Entertainment, Saluti5 na Twitter Pub.
Pia bendi hiyo itaambulisha wanenguaji wake wapya wa kike kwenye onyesho hilo maalum ya kusherekea Idd Pili.
 "Tumeamua kuleta wanenguaji wapya kabisa, wenye damu changa ili kuleta mapinduzi kwenye muziki wa dansi. Madansa wetu ni mabinti warembo, pia tuna  wanenguaji watanashati," alisema Mkurugenzi wa bendi hiyo Asha Baraka  na kuongeza kuwa;
"Tumebadilisha na kuongeza safu mpya ya unenguaji ili kwenda na wakati pamoja na soko la muziki linavyotaka."
Kwa upande wa Ige Moyaba aliyetamba kwenye albamu ya 'Mtu Pesa' ya mwaka wa 2004, Asha alisema ameandaa vitu vipya kuwapa mashabiki wa bendi hiyo inayotamba kwa staili ya 'Kisigino'.
"Kwa kweli hi siyo onyesho la kukosa kwani itakuwa ni zawadi yetu ya Idd kwa mashabiki wetu," mkurugenzi huyo alisema.
Mwezi uliyopita Twanga Pepeta walizindua albamu yao ya 10 iitwayo 'Nyumbani ni Nyumbani', ambapo nyimbo zake zitapigwa katika onyesho hilo la leo.
Nyimbo nyingine zitakazopigwa katika onyesho hilo ni zila za albamu za nyuma kama 'Jirani', 'Fainali Uzeeni', 'Chuki Binafsi', 'Ukubwa Jiwe', 'Mtu Pesa', 'Safari', 'Password', 'Mtaa wa Kwanza', 'Mwana Dar es Salaam' na 'Dunia Daraja'.

No comments:

Post a Comment