STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, September 21, 2013

Simba, Mbeya City nini bwana, ngoma kesho Yanga vs Azam

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjPnNutozTJ6LUNDdmv05v7BvLNYLIQ6dp4CQ2ET3L3oazDgFevrgY8oyJQYiRwp0q85aEDxXie6rSVYqBOkl6hngu5QSM5xh24P58eJEep1bVkTQhE8P0a20N1ChhRt5YTQlf4pHuVo4dH/s1600/MWAIKIMBA.jpg
Wachezaji Azam wakishangilia mabao yao

WAKATI Mbeya City ikiwa na kibarua kigumu mbele ya vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, macho na masikio ya mashabiki yapo kwenye pambano la kesho kati ya mabingwa watetezi Yanga na makamu bingwa, Azam zitakazopepetana kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Yanga wakishangilia moja ya mabao yao
Simba na Mbeya zinaumana leo pia kwenye uwanja huo katika mfululizo wa ligi hiyo utakaoshuhudiwa pia mechi nyingine tatu katika miji tofauti.
Hata hivyo mashabiki wa soka watakuwa na hamu kubwa ya kushuhudia pambano la Yanga na Azama ambazo zote zimeshindwa kuonyesha makeke katika mechi zake mbili zilizopita.
baada ya kubanwa mbavu jijini Mbeya ikilazimishwa sare mbili mfululizo dhidi ya wenyeji wao Mbeya City na Prisons, Yanga kesho inarejea katika dimba lake la nyumbani kujaribu bahati yake tena kwa Azam.Azam nao kama ilivyo kwa Yanga imetoka kuambulia sare mbili dhidi ya Kagera Sugar na Ashanti na kujikusanyia pointi sita sawa na ilizonazo Yanga, Mbeya City na Coastal Union.
Pambano hilo la Yanga na Azam ni kati ya mechi tatu zitakazochezwa kesho katika ligi hiyo iliyoingia raundi ya tano, michezo mingine ikiwa ni maafande wa JKT Ruvu na Oljoro JKT zitakazopepetana kwenye dimba la Chamazi, Mbagala Dar es Salaam na ile ya 'Wagosi wa Kaya' Coastal Union itakyokuwa nyumbani uwanja wa Mkwakwani, Tanga kuumana na Ruvu Shooting.
Hata hivyo pamoja na mechi hizo nyingine kuwa na mvuto wake, pambano la Yanga na Azam ndilo linaloangaliwa kwa ukaribu na mashabiki wa soka nchini kutokana na upinzani uliopo baina ya timu hizo kila zinapokutana.
Timu hizo zenye pointi sita kila mmoja zikitofautiana uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa zitakutana katika pambano lao la 11 la Ligi Kuu tangu 'Wana Lambalamba' wapande daraja mnamo mwaka 2008.
Klabu hizo zimeshakutana katika michuano kadhaa ikiwamo ya Kombe la Mapinduzi, Kombe la Kagame na Ngao ya Hisani ambayo mara ya mwisho walivaana Agosti 17 na Yanga kuitambia Azam kwa bao 1-0, lakini katika mechi za ligi kuu huwa na matokeo mengi ya kushangaza.
Kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo tangu mwaka 2008 Yanga na Azam zimekutana mara 10 katika Ligi Kuu na Yanga kushinda mechi tano na Azam ikishinda mechi tatu huku michezo yao miwili ikiishia kwa sare.
Hivyo katika pambano hilo klabu hizo zitakuwa zikifukuzia nafasi ya kuvuna pointi tatu na wakati huo huo kulinda au kuboresha rekodi yao dhidi ya mwenzake, huku wadau wa soka wakitaka kuona kama wafungaji bora wa msimu uliopita nani anatayemfunika mwenzake.
Kipre Tchetche wa Azam ndiye aliyeongoza orodha ya wafungaji bora kwa kufunga mabao 17 na amezinduka majuzi baada ya kufunga bao lake la kwanza, huku aliyeyemfuata msimu uliopita, Didier Kavumbagu tayari akiwa na mabao mawili kibindoni mpaka sasa.
Kadhalika ni mechi itakayokuwa ikishindanisha makocha wawili wa kigeni wenye rekodi nzuri kwa msimu uliopita, Ernie Brandts wa Yanga aliyeiongoza Yanga kwa mechi zaidi ya 24 bila kufungwa tangu walipolala bao 1-0 toka kwa Kagera Sugar msimu uliopita.
Kocha wa Azam, Muingereza, Stewart John Hall, yeye naye atataka kulipa kisasi kwa mpinzani wake ambaye amemtambia kwa msimu uliopita katika mechi zote za ligi na majuzi kwenye ngao ya Hisani.
Je ni Yanga au Azam itakayocheka au Kipre Tchetche atakayemtambia Didier Kavumbagu ama ni kocha Brandts kuendelea kumfunika Stewart? Tusubuiri tuone.
Rekodi za Yanga na Azam katika Ligi tangu 2008:
Oktoba 15, 2008
Yanga 3-1 Azam
Aprili 8, 2009
Azam 3-2 Yanga
Oktoba 17, 2009
Azam 1-1 Yanga
Machi 7, 2010
Yanga 2-1 Azam
Oktoba 24, 2010
Yanga 0-0 Azam
Machi 30, 2011
Yanga 2-1 Azam
Septemba 18, 2011
Azam 1-0 Yanga
Machi 10, 2012
Azam 3-1 Yanga
Novemba 4, 2012
Yanga 2-0 Azam
Februari 23, 2013
Yanga 1-0 Azam
Sept 22, 2013?

No comments:

Post a Comment