STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, September 22, 2013

Unyama! Watu watatu wa familia moja wauwawa kinyama

WATU watatu wa familia moja jijini Mwanza, akiwemo kichanga cha miezi saba, wameuawa kwa kunyongwa, kukatwa mapanga kichwani na kuchinjwa mithili ya kuku.

Mauaji hayo yamefanyika kati ya saa 9 na 10 usiku wa kuamkia jana, katika Kijiji cha Ihyila, Kata ya Buhongwa, jijini humo.

Waliofikwa na mauti hayo ni baba wa familia, Jones Elias Luhinga (44), mama wa familia, Lusia Elias Luhinga (35), na mtoto Eliud Elias Luhinga (mwaka mmoja).

Inadaiwa mauaji hayo yametekelezwa na mtu mmoja fundi wa kujenga nyumba (jina linahifadhiwa kwa sasa), aliyekaribishwa siku tisa zilizopita na Jones.

Kwa mujibu wa maelezo ya baadhi ya majirani na ndugu wa familia hiyo ya marehemu, mtu huyo alifanya unyama huo usiku wa manane, na kwamba alfajiri alioga kisha kuwafungia ndani watoto wengine waliokuwa wamelala na kutokomea kusikojulikana.

Mmoja wa ndugu wa marehemu Jones, aliyejitambulisha kwa jina la Benjamin Luhinga alinukuliwa akidai kuwa ndugu yake aliuawa kwa kuchinjwa kama kuku, kisha kukatwa panga katikati ya kichwa na upande mmoja wa juu ya sikio.

"Jones ni mjomba wangu, ameuawa kwa kuchinjwa hapa kwenye koromeo. Amekatwa na panga hapa kichwani na eneo hili la juu ya sikio. Lakini tumekuta mabegi yamefunguliwa, labda alikuwa akitafuta fedha.

"Binafsi nina shaka huenda mjomba wangu ameuawa kwa sababu za fitna au fedha aliyouza kiwanja huko Buswelu baada ya kulipwa na jiji na baadaye akaja kujenga huku Buhongwa," alisema.

Benjamin alisema fundi ujenzi anayetuhumiwa kutekeleza mauaji hayo aliitwa na Jones na tangu awasili nyumbani hapo alikuwa akilala kwenye chumba cha watoto.

Alibainisha kuwa familia hiyo ina watoto tisa na haijulikani kwanini mtuhumiwa hakuwadhuru wengine nane waliokuwamo kwenye chumba alichokuwa akilala.

Inadaiwa kuwa mtoto aliyeuawa alikuwa amelala na wenzake na muuaji aliamua kumpeleka kwa mama yake ili akanyonye na ndipo alipokwenda kumnyonga.

Musa Sayi, mkazi wa Buhongwa alisema walipata taarifa za mauaji hayo jana alfajiri na walipofika walihisi kuna mtu amemaliza kuoga lakini hawakumuona.

“Mazingira tuliyoyakuta pale tulihisi kuna mtu anaoga, lakini hatukuona. Tulihisi ndiye muuaji labda amefanya mitambiko ya kichawi,” alisema.

Jeshi la Polisi kupitia kwa Mkuu wa Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Mwanza, Joseph Konyo (RCO), alisema Jones aliuawa kwa kukatwa panga kichwani na upande mmoja wa juu ya sikio, na si kuchinjwa kama kuku.

"Huyu baba mwenye nyumba yeye ameuawa kwa kukatwa panga katikati ya kichwa na likaingia sana na huku upande wa karibu na sikio. Hajachinjwa kama baadhi ya watu wanavyodai," alisema.

Konyo alisema walifika eneo la tukio hilo na kushuhudia miili ya marehemu hao.

Akizungumzia tukio la jana, RCO Konyo alisema yawezekana chanzo cha mauaji hayo yanatokana na fitna, visa na uhasama wa muda mrefu baina ya mwenye nyumba na baadhi ya watu na kuna uwezekano muuaji hakuwa peke yake.

Kamanda Konyo alisema polisi itawasaka wauaji hao ili iwafikishe kwenye vyombo vya sheria.

Tukio kama hilo limewahi kutokea Februari 16, 2010 huko Musoma mkoani Mara, baada ya watu 17 wa familia tatu za koo moja kuuawa kinyama na wengine watatu kujeruhiwa vibaya pamoja na ng’ombe kadhaa kuchinjwa huko Buhare.

Mauaji hayo ya Musoma yalielezwa kwamba yalikuwa ya kulipiza kisasi, baada ya kutokea wizi wa mifugo kisha watu kadhaa kuuawa miaka ya nyuma kabla ya mwaka huo 2010.

No comments:

Post a Comment