STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, October 3, 2013

Beki Simba achekelea ushindani wa namba Msimbazi

Adeyum Saleh Ahmed
BEKI mpya wa klabu ya Simba Adeyum Saleh amekiri kuna ushindani mkubwa wa namba katika kikosi cha vinara hao wa Ligi Kuu ya Vodacom, lakini akidai anafurahia hali hiyo akiamini itasaidia kuinua kiwango chake na cha timu nzima.
Aidha beki huyo aliyesajiliwa Simba akitokea Miembeni ya Zanzibar, anasema Ligi Kuu ya Tanzania Bara ni ngumu na yenye ushindani huku wachezaji wake wakicheza kwa malengo kuliko ilivyo Ligi Kuu ya visiwani Zanzibar alitokea.
Akizungumza na MICHARAZO kwenye mahojiano maalum, Adeyum aliyewahi kuzichezea Malindi, Mafunzo na Oljoro JKT, alisema ndani ya Simba hakuna mchezaji wenye uhakika wa namba mpaka sasa kutokana na ushindani uliopo kitu kinachowafanya wachezaji wote kujifua vilivyo ili kuwavutia makocha.
"Hivi ndivyo inavyotakiwa kwa timu yoyote, kadri ushindani unapokuwa mkubwa ndivyo wachezaji wanaimarisha viwango vyao, naamini hata mimi kiwango changu kitapanda zaidi na kutimiza ndoto nilizojiwekea," alisema.
Beki huyo wa kushoto alisema moja ya ndoto zake ni kucheza soka la kulipwa nje ya nchi pamoja na kutamani aje kuitwa kuichezea timu ya taifa (Taifa Stars) kwani hajaridhika na kuichezea Zanzibar Heroes tu.
Pia mkali huyo aliyewavutia makocha na mashabiki mara alipojitokeza kwenye majaribio ya timu hiyo alisema Ligi ya Tanzania Bara ni tofauti kiushindani na ile ya visiwani Zanzibar.
Alisema Ligi ya Bara ni ngumu na wachezaji wanacheza kwa malengo kitu ambacho anatamani nyota wa visiwani wangepata fursa ya kuja kuicheza ligi hiyo ili kukuza viwango vyao na kuisaidia timu ya taifa ya visiwa hivyo.
Adeyum anayeisaidia timu ya taifa ya Zanzibar, kunyakua nafasi ya tatu katika michuano ya Kombe la Chalenji ya mwaka jana, alisema ugumu wa ligi hiyo unafanya awe mgumu kutabiri itakavyokuwa mbeleni japo anatamani kuibebesha Simba taji la ligi la Vodacom.

No comments:

Post a Comment