STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, October 3, 2013

Warundi kuwachezesha Twiga Stars, Msumbiji


SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Burundi kuchezesha mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kwa wanawake chini ya miaka 20 Kanda ya Afrika kati ya Tanzania na Msumbiji.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, Waamuzi hao watakaochezesha mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya Oktoba 26 na 27 mwaka huu wataongozwa na Ines Niyonsara.
Niyonsara atasaidiwa na Jacqueline Ndimurukundo na Axelle Shikana, huku Irene Namiburu kutoka Uganda ndiye atakayekuwa mwamuzi wa mezani wakati Kamishna wa mechi hiyo ni Evelyn Awuor wa Kenya.
Wambura alisema mechi ya marudiano itachezwa jijini Maputo kati ya Novemba 9 na 10 mwaka huu, na itachezeshwa na waamuzi kutoka Madagascar.
Fainali hizo za Kombe la Dunia zitafanyika mwakani nchini Canada, ambapo Tanzania inashiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo ya Kombe la Dunia kwa wasichana.
Timu ya Tanzania tayari imepiga kambi mkoani Pwani ikiwa chini ya Kocha wake Rogasian Kaijage.
Wachezaji walioko kambini ni Amina Ally, Amina Ramadhan, Amisa Athuman, Anastazia Anthony, Anna Hebron, Belina Julius, Donisia Daniel, Esther Mayala, Fatuma Issa, Gerwa Lugomba, Happiness Lazoni, Harriet Edward, Hellen Maduka, Irene Ndibalema, Jane Cloud, Khadija Hiza na Latifa Salum.
Wengine ni Maimuna Hamis, Mwanaidi Khamis, Najiati Abbas, Neema Paul, Niwael Khalfan, Rehema Abdul, Sabahi Hashim, Sada Ramadhan, Shamimo Hamis, Shelder Boniface, Stumai Abdallah, Tatu Idd, Therese Yona, Violet Nicholas, Vumilia Maarifa, Yulitha Kimbuya na Zena Said.

No comments:

Post a Comment