STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, November 11, 2013

Bunge lapata msiba, Rais Kikwete atuma salamu za rambirambi

Anselm Lyatonga Mrema enzi za uhai wake
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Anne Semamba Makinda kuomboleza kifo cha Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Shughuli za Bunge, Bwana Anselm Lyatonga Mrema kilichotokea usiku wa tarehe 10 Novemba, 2013 katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma alikokuwa amepelekwa kwa matibabu ya ugonjwa wa shinikizo la damu.

“Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mtumishi wa Ofisi yako ya Bunge, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Shughuli za Bunge, Bwana Anselm Lyatonga Mrema kilichotokea usiku wa tarehe 10 Novemba, 2013 katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma alikokuwa amepelekwa kwa matibabu akisumbuliwa na shinikizo la damu”, amesema kwa masikitiko Rais Kikwete katika Salamu zake za Rambirambi.

“Nilimfahamu Marehemu Anselm Lyatonga Mrema, enzi za uhai wake, kama Mtumishi Mwaminifu, Mwadilifu na Mchapakazi Hodari aliyejituma kikamilifu katika utekelezaji wa majukumu yake, sifa ambazo zilimfanya apande cheo kutoka kuwa Katibu Msaidizi Mwandamizi wa Bunge na kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Shughuli za Bunge”, ameongeza kusema Rais Kikwete.

“Kutokana na msiba huo mkubwa, ninakutumia wewe Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Anne Semamba Makinda pamoja na Watumishi wote wa Bunge Salamu zangu za Rambirambi kwa kuondokewa na Mtumishi muhimu ambaye mchango wake katika Utumishi wa Bunge na Taifa kwa ujumla ulikuwa bado unahitajika sana”, amesema Rais Kikwete.

Rais Kikwete amemuomba Spika wa Bunge kumfikishia Salamu zake za Rambirambi na pole nyingi kwa Familia ya Marehemu Anselm Lyatonga Mrema kwa kupotelewa na Kiongozi na mhimili muhimu wa familia. Amewahakikishia Wanafamilia kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba wa Mpendwa wao.

Amewaomba wawe na moyo wa uvumilivu na ujasiri katika kipindi chote cha maombolezo kwa kutambua kuwa yote ni mapenzi yake Mola.  Aidha Rais Kikwete amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza Mahala Pema Peponi Roho ya Marehemu Anselm Lyatonga Mrema, Amina.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu

No comments:

Post a Comment