STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, November 30, 2013

Samatta, Ulimwengu kuweka rekodi leo Afrika na Tp Mazembe?

http://millardayo.com/wp-content/uploads/2013/09/B12CXSM0063.jpg
TP Mazembe watavuna nini leo kwa Watunisia Kombe la Shirikisho?
Na Nurat Mahmoud, Lubumbashi 
WASHAMBULIAJI Mbwana Ally Samatta na Thomas Emanuel Ulimwengu leo watakuwa wanawania kuwa Watanzania wa kwanza kuvaa Medali za Dhahabu za michuano ya Afrika wakati klabu yao, Tout Puissant Mazembe itakapokuwa inamenyana na CS Sfaxien ya Tunisia, katika fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi.
Mazembe inatakiwa kushinda mabao 3-0 leo nyumbani ili kutwaa taji hilo, baada ya awali kufungwa mabao 2-0 na Watunisia hao Uwanja Olympique de Rades mjini Tunis katika Fainali ya kwanza.
Mbwana Samatta kushoto akiwa ameinua Kombe la Super la DRC miezi miwili iliyopita,je leo atainua Kombe la Shirikisho?

Siku hiyo, mabao yaliyoizamisha Mazembe yalifungwa na washambuliaji wa kimataifa wa Gabon, Ibrahim Didier Ndong aliyefunga bao la kwanza dakika ya 16 na mshambuliaji Taha Yassine Khenissi aliyefunga la pili dakika ya 90 na ushei wakimtungua kipa mahiri, Robert Muteba Kidiaba.
Washambuliaji wote wa Tanzania, Samatta na Ulimwengu walianza katika kikosi cha Mazembe pamoja na Tressor Mputu Mabi, lakini hawakuweza kuwanusuru mabingwa mara nne Afrika na kipigo hicho.
Sfaxien, timu pekee iliyoshinda Kombe la Shirikisho mara mbili tangu kutambulishwa kwa mfumo mpya mwaka 2004, yenye maskani yake katika mji uliozungukwa na bahari ya Mediterranean, Sfax itahitaji sare katika mchezo wa marudiano au kufungwa kwa tofauti isiyozidi bao 1-0, mjini Lubumbashi ili kujinyakulia taji.
Bingwa wa Kombe hilo atazawadiwa kitita cha dola za Kimarekani, 625 000, wakati mshindi wa pili atapata dola 432 000.
Mshindi pia atamenyana na mabingwa wa Ligi ya Mabingwa, Al Ahly ya Misri kuwania taji la Super Cup mechi itakayopigwa nchini Misri Februari 2014.
Wachezaji waliokuwa wakiunda kikosi cha Simba SC mwaka 1993 walivalishwa Medali za Fedha na Rais mstafu wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi baada ya kufungwa mabao 2-0 na Stellah Abidjan ya Ivory Coast mwaka 1993 katika fainali ya pili ya Kombe la CAF Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Awali, Simba ilitoa sare ugenini na kuwapa matumaini Watanzania kwamba taji la kwanza kubwa Afrika lingetua nchini mwaka 1993.
Washambuliaji hao, Samatta na Ulimwengu baada ya fainali hiyo ya mwisho leo, kesho watapanda ndege kuelekea Nairobi, Kenya kuungana na kikosi cha Bara, Kilimanjaro Stars kinachoshiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge.

No comments:

Post a Comment