STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, December 25, 2013

Awadh Juma alitoa bao lake kwa familia, amtetea Kaseja

Awadh Juma alipomtesa Kaseja katika mechi ya Simba na Yanga

KIUNGO mpya klabu ya Simba, Awadh Juma amesema anajisikia furaha kubwa kuitungua Yanga katika ushindi wa 3-1 wa mechi yao ya kirafiki ya Nani Mtani Jembe na kwamba amelitoa bao hilo kama zawadi kwa familia yake.
Awadh alifunga goli hilo katika nyavu tupu baada ya kumpa 'presha' kipa Juma Kaseja aliyejikanganya na kuanguka nje ya boksi wakati akijaribu kuurudisha mpira kwenye eneo lake la kujidai ili audake na kumruhusu mfungaji kumtungua kiulaini.
Akizungumza na MICHARAZO, Juma alisema analitoa bao hilo lililomletea matatizo kipa anayeaminiwa kuwa bora zaidi nchini, Juma Kaseja, kama zawadi kwa familia yake inayomuunga mkono katika kila kitu chake katika soka.
Mkali huyo anayeichezea pia timu ya taifa ya Zanzibar, alisema bao lake lililokuja baada ya kumzidi ujanja Kaseja na kumnyang'anya mpira ulioonekana hauna madhara kwa Yanga ni mwanzo nzuri kwake ndani ya Simba na kudai amefurahi mno kuitungua Yanga na kupata bahati ya kuanza kwenye mechi kubwa kama hiyo.
"Siku zote nilikuwa naota kucheza pambano la watani za jadi na nimefurahia Simba kunisajili na kubahatika kupangwa katika pambano hilo na kufunga bao ambalo nalitoa kwa familia yangu kama zawadi kwao," alisema.
Aidha, mchezaji huyo amewaahidi wanachama na mashabiki wa Msimbazi kusubiri raha zaidi wakati mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakapoanza akisema alichokionyesha uwanjani siku ya Jumamosi ni sehemu tu ya ujuzi wake.
Awadh aliyesajiliwa akitokea Mtibwa Sugar alisema pamoja na watu kumsifia kwa kuonyesha kiwango kizuri katika pambano hilo lililochezwa uwanja wa Taifa, yeye anajiona kama amecheza kiwango cha chini na kuwaomba mashabiki na wanachama wa Simba kusubiri kuona ujuzi wake duru la pili litakapoanza.
"Tuombe uzima ligi ianze watu waone kiwango changu halisi, ila kwa kweli nashukuru na nimefurahi kutua Simba na kuanza kuitumikia kwenye mechi ya watani wa jadi," alisema.
Aidha Awadh alisema kosa lililofanywa na Kaseja linaweza kufanywa na yeyote hivyo asibebeshwe lawama kwani ni tukio la kwaida la mchezo.
"Sidhani kama kuna sababu ya Kaseja kusakamwa ni mmoja wa makipa hodari na lililomtokea huweza kumtokea yeyote asisakamwe," alisema Awadh aliyepo visiwani Zanzibar kwa sasa kwa mapumziko mafupi.

No comments:

Post a Comment