STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, February 11, 2014

MZEE KINGUNGE ATEMA CHECHE VITA YA DAWA ZA KLEVYA

* Adai bila kunaswa 'vigogo' ni kazi bure
* Asisitiza mfumo wa malezi, tamaa chanzo cha tatizo
Mzee Kingunge akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na blogu hii nyumbani kwake
WAKATI serikali ikitokwa povu la mdomo ikijigamba kuwa, itaongeza ukali dhidi ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya nchini, japo tatizo hilo linaloonekana kuzidi kuota mizizi, mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru ameibuka na kufichua sababu za biashara hiyo kushindwa kukomeshwa huku taifa likiendelea kushuhudia vijana ambao ni nguvu kazi ikiangamia kwa tamaa za utajiri wa watu wachache.
Mwanasiasa huyo amesema ni vigumu biashara hiyo kukoma nchini kama serikali na vyombo vyake vya dola havitawashughulikia na kuwakamata  'vigogo' wa biashara hiyo pamoja na kutengenezwa sheria kali itakayowafanya wahusika wajutie kujihusisha nayo na kuwatia woga watu wengine wanaoanza au kutamani kuifanya biashara hiyo.
Pia, amesema ni lazima serikali na jamii kwa ujumla ishirikiane katika kuwapa malezi na elimu bora watoto na vijana itakayowafanya wapende kufanya kazi na kujitegemea badala ya kuwa tegemezi, wavivu na wanaopenda anasa na tamaa ya kutamani vitu ambavyo hawana uwezo wa kuvipata.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi nyumbani kwake wiki iliyopita, Kingunge alisema tatizo la dawa za kulevya ni kubwa na linaloliangamiza taifa, na kwamba licha ya kuwepo kwa juhudi tatizo hilo limeshindwa kupatiwa ufumbuzi kwa sababu wanaonaswa ni watu wadogo tu, huku vigogo na wamiliki wakubwa wa mtandao huo wakiachwa mitaani bila kuguswa.
Kingunge alisema pia hata sheria zilizopo ni nyepesi na zisizowafanya watuhumiwa na biashara hiyo kuziogopa, japo alidai asingependa kupona sheria za kuwapiga risasi au kuwanyonga kama zinazofanywa na mataifa mengine ndizo zitumike nchini, lakini alitaka sheria ziwe kali na zitakazowafanya wanaonaswa wakijishughulisha na biashara hiyo kujuta wao na familia zao ambazo zimekuwa zikifahamu nyendo zao na kunyamaza.
"Juhudi za kudhibiti suala hili zipo,  ila hazizai matunda kwa sababu wanaokamatwa ni watu wadogo, vigogo je kwa nini hawaguswi? Ni vyema nguvu zikaelekezwa kwa vigogo na kuwekwa sheria kali ya kuwatisha wanaojihusisha na biashara hiyo. Dawa za kulevya ni janga na hatari kwa taifa.  Ni tatizo la dunia nzima hivyo tunapaswa kuonyesha ukali katika hili hapo tunaweza kudhibiti, ingawa kukomesha kabisa ni vigumu," alisema.
Alisema pia kuna haja ya kujipanga upya katika kuteua watu wa kushughulikia mapambano ya dawa za kulevya kwa kuhakikisha wanateuliwa watu waaminifu na wasiojihusisha na mtandao wa biashara hiyo vinginevyo vita dhidi ya dawa za kulevya zitakuwa kazi bure tu.
Kingunge aliyewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ukiwamo uwaziri katika awamu zote nne za uongozi tangu taifa lipate uhuru, alisema pia tatizo la biashara hiyo ya dawa za kulevya limekuwa sugu kutokana na mfumo wa maisha uliopo kwa sasa kuanzia kwenye malezi hadi katika elimu kwa watoto na vijana inayowafanya wakuwe wakiwa wavivu na kuthamini fedha na anasa kuliko kufanya kazi.
"Wazazi, walezi na hata serikali imekuwa ikikumbatia na kuthamini sana watu wenye fedha, pia jamii imekuwa inapenda anasa na njia za mkato za maisha badala ya mfumo wa malezi na elimu unaowafanya watu wapende kufanya kazi kama tulivyokuwa tukihimiza miaka ya nyuma. Hili liunafanya watu watafute kila njia kupata fedha hata kwa njia haramu," alisema.
Kuhusu wimbi la wanawake nao kujiingiza kwenye biashara hiyo na baadhi yao kunaswa katika mataifa ya nje, alisema wanalazimika kwa sababu nao wanatafuta fedha kw akutambua bila ya kuwa na fedha hawathaminiki wala kuonekana ni watu.
"Upo msemo kwamba mtu kitu asiyekuwa na kitu kinyama cha mwitu, tusiwalaumu wanawake na vijana kuingia kwenye biashara hii, wanatafuta fedha kwa sababu wamewaona wazazi na walezi wao na hata serikali ikithamini na kuwapa heshima watu wenye fedha," alisema.
Mwanasiasa huyo alisema hata hivyo kuna tatizo la jamii ya kitanzania kuangalia matokeo ya hali ya mambo badala ya kuangalia chanzo cha suala hilo, akidai biashara ya unga imeanza kitambo kirefu lakini iliwahusisha watu wachache lakini kutokana na mabadiliko ya utandawazi vijana wamekuwa wakijifunza mambo mengi ya upuuzi kupitia runinga na mitandao na kujikuta wakizama kwenye maovu.

No comments:

Post a Comment