STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, March 20, 2014

TASWA yateua 12 Kamati Tuzo za Wanamichezo Bora

Katibu Mkuu wa TASWA. Amir Mhando ;Mgosi'
KAMATI ya Utendaji ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) iliyokutana jijini Dar es Salaam wiki iliyopita imeteua majina ya watu 12 kwa ajili ya kusimamia Tuzo za Wanamichezo Bora Tanzania zinazotolewa kila mwaka na chama hicho huku ikizifanyia mabadiliko makubwa tuzo hizo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kaimu Mwenyekiti TASWA, Egbert Mkoko, kamati hiyo ya tuzo ambayo itakuwa chini ya uenyekiti wa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TASWA, Rehure Nyaulawa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Redio 100.5 Times FM, ina wajumbe wengine 10 ambao si viongozi wa TASWA, lakini ni waandishi wazoefu wa habari za michezo.
"Jukumu la kamati hiyo pamoja na kuandaa mchakato wa upatikanaji wa Wanamichezo Bora wa Tanzania mwaka 2013 na kupanga tarehe ya kufanyika tuzo hiyo mwaka huu, lakini pia imepewa mamlaka ya kutazama mfumo wa tuzo ulivyo na ikiwezekana kuubadili kwa namna itakavyoona inafaa kwa maslahi ya chama na maendeleo ya michezo kwa ujumla," ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliongeza: "Ni nia ya Kamati ya Utendaji ya TASWA ni kuona tuzo inakuwa bora na ambayo wadau wa michezo wataendelea kuiheshimu kwa kila hatua. Ndiyo maana TASWA ikaamua kuipa kamati hiyo mamlaka ya kuamua mambo ya msingi katika kuiboresha kwa mipango ya muda mfupi na mrefu."
Pamoja na mwenyekiti Nyaulawa, wengine walioteuliwa kuunda kamati hiyo na vyombo vyao katika mabano ni Amour Hassan (Mhariri wa habari za Michezo - NIPASHE), Elizabeth Mayemba (Mwandishi wa Majira), Dominick Isiji (Mhariri wa michezo - The African) na Rais wa Chama cha Gofu Wanawake Tanzania (TLGU), ambaye pia ni mwandishi wa habari za michezo wa gazeti la Daily News, Mbonile Burton.
Wengine ni Mahmoud Zubeiyr (mmiliki bongostazblogspot), Athanas Kazige (Mwandishi Uhuru), Suleiman Jongo (Mwandishi-Citizens), Angela Msangi (Mwandishi TBC1) na Cosmas Mlekani (Mwandishi - Spotileo) na Tulo Chambo ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Riadha Tanzania (RT) na pia Mhariri wa habari za michezo wa gazeti la Tanzania Daima.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa katibu wa kamati hiyo atakuwa Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando na kwamba kikao cha kwanza cha kamati kitafanyika jijini Dar es Salaam Jumatatu Machi 24 na kitafunguliwa na Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto, ambaye kwa sasa yupo safarini.

No comments:

Post a Comment