STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, March 26, 2014

Yanga yaiua Prisons Taifa, Azam haishikiki

Yanga
Azam wanaozidi kuukomalia ubingwa unaoshikiliwa na Yanga
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga imezidi kufufua matumaini ya kutetea taji hilo baada ya jioni hii kuibugiza Prisons-Mbeya kwa mabao 5-0.
Pambano hilo lililochezwa kwenye uwanja wa Taifa, lilishuhudia Yanga wakienda mapumziko wakiongoza kwa mabao 2-0.
Bao la kwanza la Yanga liliwekwa kimiani na Mganda Emmanuel Okwi kwa mkwaju wa faulo katika dakika ya 21 kabla ya Mrisho Ngassa kuongeza la pili dakika ya 38 akimalizia krosi ya Husseni Javu.
Kipindi cha pili Yanga ilicharuka na hasa baada ya kufanya mabadiliko ya wachezaji na kuweza kujiandikia bao la tatu lililofungwa dakika 68 na mtokea benchi, Hamis Kiiza 'Diego'.
Kiiza alifunga bao hilo akiuwahi mpira uliotemwa na kipa wa Prisons baada ya Simon Msuva kumimina krosi murua langoni mwa 'Wajelajela' na Mganda huyo kufunga kilaini.
Nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro' aliiandikia Yanga bao la nne katika dakika ya 78 kwa mkwaju wa penati baada ya mabeki wa Prisons kumuangusha Husseni Javu, aliyeng'ara katika mchezo huo aliyoingia kipindi cha kwanza kuchukua nafasi ya Jerryson Tegete.
Dakika chache kabla ya kumalizika kwa pambano hilo, Kiiza kwa mara nyingine aliiongezea Yanga bao la tano baada ya Hussen Javu kufanya kazi nzuri kwa kufumua shuti langoni mwa wapinzani wao.
Kwa ushindi huo Yanga wamefikisha pointi 46 kutokana na kucheza mechi 21, wakiendelea kusalia nafasi ya pili nyuma ya Azam ambao jioni hii wameibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mgambo JKT katika pambano lililochezwa jijini Tanga.
taarifa toka Tanga zinasema kuwa Azam walipata mabao yake kupitia kwa John Bocco na Brian Umony na kuifanya timu hiyo kuendeleza rekodi yao ya kutopoteza mchezo wowote katika ligi ya msimu huu na kukaa kileleni wakiwa na pointi 51 licha ya kucheza mchezo 22.

No comments:

Post a Comment