Michael Wambura |
Rais Mpya wa Simba, Evance Aveva (kulia) akiwa na Mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, Hassan Dalali |
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Wambura amesema hakuna haja ya kupeleka suala lake kwenye mkutano huo kwasababu sakata lake lilimalizwa na kamati ya Rufani ya uchaguzi ya TFF chini ya mwenyekiti wake, Jaji Julius Mutabazi Lugaziya.
Wambura ameyasema hayo ikiwa ni siku moja baada ya Aveva alitangaza kuwasimamishwa wanachama 69 kwa kosa la kwenda mahakama ya kawaida kujaribu kuzuia uchaguzi huo wa Simba na kudai suala lao litajadiliwa kwenye mkutano mkuu wa mwezi agosti, sawia na suala linalomhusu Wambura aliyewahi kuipeleka Simba mahakamani katika uchaguzi wa mwaka 2010 kosa lililomfanya ajikute matatani Msimbazi.
Hata hivyo Wambura amekuja juu na kusema yeye alishasafishwa na kamati ya Lugaziya na kitendo cha Aveva kuwapiga `Stop` wanachama ni kuendelea kuchochea migogoro isiyokuwa ya lazima.
“Mimi nilisafishwa kwenye kamati ya Rufani ya Lugaziya na ndio maana nilirudishwa kwenye mchakato wa uchaguzi, na niliondolewa kwa kosa la kupiga kampeni kabla ya muda, hivyo sina haja na mkutano huo”. Alisema Wambura.
Wambura aligusia Ibara ya 41(d) ya klabu ya Simba ambapo alifafanua kuwa kuwanyima wanachama fursa ya kujitetea na kusikilizwa kabla ya kuchukua hatua ni uvunjifu wa haki za msingi za binadamu.
Aidha, Wambura alisema wanachama waliokwenda mahakamani wasipuuzwe kwasababu wana hoja za msingi.
“Wangekuwa hawana hoja, hata mahakama kuu isingewapa haki ya kufungua shauri lao. Wasipuuzwe, wapewe fursa ya kujitetea na kusikilizwa”. Aliongeza Wambura.
Alisisitiza kuwa Ibara ya 54(3) ya klabu ya Simba inafafanua kuwa uamuzi wowote wa kufukuza wanachama lazima upigiwe kura za siri na wajumbe theluthi mbili waunge mkono, huku akitolea mfano wa Hassani Dalali alipofanya jaribio la kumpinuda Mwina Kaduguda, lakini alikwama kwasababu wanachama walikataa pendekezo lake.
Aliongeza kuwa uongozi wa Aveva hauwezi kupambana na wanachama zaidi ya 500 na kama utaendelea kufanya hivyo basi utaingia katika mgogoro mkubwa, lakini akashauri uongozi utafute suluhusho la mapema.
Wambura alisema ushauri wake atauwasilisha kwa maandishi kwa uongozi wa Simba sc kama sehemu kutunza kumbukumbu kuwa aliyaongea hayo.
No comments:
Post a Comment