STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, September 5, 2014

HALI YA HEWA YABASHIRI MAFURIKO NCHINI

Dkt. Agnes L. Kijazi

MWELEKEO WA MVUA KWA KIPINDI CHA OKTOBA - DISEMBA 2014 NCHINI
A:         UTANGULIZI                                      
Taarifa hii inatoa tathmini ya mvua za masika (Machi - Mei) 2014 na mwelekeo wa mifumo ya hali ya hewa na mvua kwa kipindi  cha mwezi Oktoba hadi Disemba, 2014(Vuli).
B:         TATHMINI YA MVUA KIPINDI CHA MACHI – MEI, 2014
Katika msimu uliopita wa mvua za Masika Machi hadi Mei, 2014. Maeneo mengi ya nchi yalipata mvua za wastani hadi juu ya wastani isipokuwa maeneo machache ya mikoa ya Mwanza, Singida na Dodoma ambayo yalipata mvua za chini ya wastani. Matukio ya vimbunga hususan Kimbunga ‘Hellen’ kilichotokea katika Rasi ya Msumbiji kusini magharibi mwa baharí ya Hindi kilisababisha ongezeko la mvua katika eneo la Pwani ya kaskazini.
Maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka:
Kanda ya Ziwa Victoria: Viwango vya mvua vilivyopimwa katika vituo vya Bukoba na Musoma vilikuwa juu ya wastani. Kituo cha Shinyanga kilipima mvua kiwango cha wastani wakati katika kituo cha Mwanza kiwango cha mvua kilikuwa chini ya wastani.
Nyanda za juu kaskazini mashariki: Vituo vya Arusha, Lyamungo na Kilimanjaro vilipima mvua juu ya wastani ilihali vituo vya Moshi na Same kiwango cha mvua kilikuwa cha wastani.
Pwani ya kaskazini na visiwa vya Unguja na Pemba: Vituo vya Dar es Salaam, Morogoro na Pemba vilipima mvua za juu ya wastani na vituo vya Zanzibar, Amani, Kizimbani pamoja na Tanga mvua zilikuwa wastani.

Dondoo muhimu

1. Mwelekeo wa mvua kwa kipindi cha Oktoba-Disemba, 2014 Vuli unaonyesha kuwa;
           Hali ya mvua inatarajiwa kuwa ya  kuridhisha katika maeneo mengi ya nchi hata hivyo mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa  katika baadhi ya maeneo ya kusini mwa nchi hususan mkoa wa Ruvuma.
           Msimu huu mvua zinatarajiwa kuanza mapema mwezi Septemba katika maeneo ya ziwa Viktoria, nyanda za juu kaskazini mashariki na pwani ya kasikazini
 2. Athari na Ushauri
           Mvua za kutosha zinatarajiwa kwa shughuli za  kilimo katika maeneo mengi ya nchi.
           Vina vya maji katika mito na mabwawa vinatarajiwa kuongezeka katika maeneo mengi ya nchi.
           Maji yatumike kwa uangalifu na kuzingatia taratibu za uvunaji, uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali maji
           Matukio ya migogoro inayosababishwa na mifugo, wanyamapori na shughuli za binadamu na kilimo hayatarajiwi kujitokeza kwa kiasi kikubwa.
           Vipindi vya mvua kubwa vinaweza kuongeza matukio ya mafuriko na uharibifu wa mali na miundombinu.
           Milipuko ya magonjwa yanayosababishwa  na kutuama kwa maji na utiririshaji wa majitaka usiodhibitiwa inaweza kujitokeza.
           Hatua stahiki katika utunzaji wa mazingira, upatikanaji wa maji safi na salama, na usambazaji wa madawa, maji na chakula ikiwa ni hatua za kujiandaa na kukabiliana na majanga yanayoweza kutokea

Maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka:
Nyanda za juu kusini magharibi: Vituo vya Mbeya, Tukuyu, na Mahenge vilipima mvua juu ya wastani na kituo cha Sumbawanga kiwango cha mvua kilikuwa cha wastani.
Kanda ya magharibi: Mvua juu ya wastani ilipimwa katika kituo cha Kigoma ilihali vituo vya Kibondo na Tabora mvua zilikuwa ni za wastani.
Pwani ya kusini: Kituo cha Kilwa kilipima mvua juu ya wastani na vituo vya Mtwara pamoja na  Naliendele mvua zilikuwa za wastani.
Kanda ya kati: Vituo vya Singida na Dodoma vilipima mvua chini ya wastani na kituo cha Hombolo mvua za wastani. 
Kanda ya kusini: Kituo cha Songea kiwango cha mvua kilichopimwa kilikuwa juu ya wastani.
C: MIFUMO YA HALI YA HEWA
Katika kipindi cha miezi ya Oktoba hadi Disemba, 2014 hali ya joto la bahari katika maeneo ya magharibi na kusini -magharibi mwa bahari ya Hindi inatarajiwa kuwa juu ya wastani, upande wa mashariki mwa bahari ya Hindi hali ya  joto la wastani inatarajiwa. Hali hii inatarajiwa kusababisha  upepo  wenye unyevunyevu  kutoka bahari ya Hindi kuelekea katika eneo la  Pwani ya Africa Mashariki. Aidha, hali ya joto la chini ya wastani katika eneo la mashariki mwa bahari ya Atlantiki (Pwani ya Angola) inatarajiwa kusababisha ongezeko la hewa yenye unyevunyevu kutoka katika misitu ya Kongo kuelekea katika maeneo ya magharibi na kusini Magharibi mwa nchi.
Hali ya joto la juu ya wastani katika eneo la Tropikali ya bahari ya Pasifiki linatarajiwa kuendelea kwa kipindi cha miezi ya Oktoba hadi Disemba, 2014. Hali hiyo inatarajiwa kuchangia ongezeko la mvua katika baadhi ya maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua. Hali ya joto la juu ya wastani katika eneo la kusini magharibi mwa Bahari ya Hindi linaashiria kuwepo kwa matukio ya vimbunga katika msimu wa mvua za Vuli kuanzia mwezi Novemba, 2014.
D:         MWELEKEO WA MVUA OKTOBA - DISEMBA 2014: 
Kutokana na mwelekeo wa mifumo ya hali ya hewa inayotarajiwa, mvua za kipindi cha Oktoba hadi Disemba, 2014 zinatarajiwa kuwa kama ifuatavyo:
(i)         Mvua za Vuli (kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua)
Msimu wa mvua wa Oktoba hadi Disemba (Vuli) ni mahususi katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki, pwani ya kaskazini, kanda ya Ziwa Viktoria na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.

Katika msimu huu mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo ya pwani ya kaskazini (mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba), nyanda za juu kaskazini mashariki (mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara) pamoja na mikoa ya Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
Msimu wa mvua za Vuli unatarajiwa kuanza mwezi Septemba, 2014 katika ukanda wa Ziwa Viktoria na kusambaa katika maeneo mengine. Hata hivyo, mvua hizo zinatarajiwa kuanza mapema katika maeneo ya ukanda wa pwani (Mkoa wa Tanga na kisiwa cha Pemba) na katika baadhi ya maeneo ya nyanda za juu kaskazini Mashariki.

Kanda ya Ziwa Victoria: (Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga): Mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Septemba, 2014 katika mkoa wa Kagera na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma na kuendelea kusambaa katika mikoa ya Mwanza,  Geita, Shinyanga, Simiyu na Mara. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani katika maeneo ya mikoa ya Kagera, Geita, Mara, Mwanza pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma. Maeneo mengi ya mkoa wa Shinyanga yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani.

Ukanda wa Pwani ya Kaskazini: (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro-kaskazini pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya mwezi Septemba, 2014 katika maeneo ya mikoa ya Tanga, Dar es Salaam pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba na kusambaa maeneo ya mkoa  wa Morogoro. Mvua hizi zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi.

Nyanda za juu Kaskazini Mashariki: (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara):
Mvua katika maeneo haya zinatarajiwa kuanza wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Septemba, 2014 na zinatarajiwa kuwa juu ya wastani katika maeneo mengi ya mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na kaskazini mwa mkoa wa Manyara. Hata hivyo, kusini mwa mkoa wa Manyara, mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani.
(ii)        Mvua za Msimu (Novemba – Aprili) kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua.
Msimu wa mvua za Novemba hadi Aprili ni mahususi kwa  maeneo ya  Magharibi mwa nchi, kanda ya  kati, nyanda za juu kusini-magharibi, kusini mwa nchi na pwani ya kusini. Katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba, 2014 maeneo mengi yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.

Kanda ya Magharibi (Mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya pili ya mwezi Novemba, 2014. Mvua hizi zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani katika maeneo ya mikoa ya Rukwa, Katavi pamoja na kusini mwa mkoa wa Kigoma. Hata hivyo, maeneo mengi ya mkoa wa Tabora yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani.
Kanda ya kati (Mikoa ya Singida na Dodoma):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya tatu ya mwezi Novemba, 2014 na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani.
Nyanda za juu Kusini Magharibi: (Mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe na kusini mwa Morogoro):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Novemba, 2014 na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi. Maeneo ya magharibi mwa mkoa wa Mbeya, mvua zinatarajiwa kuwa juu ya wastani.
Maeneo ya kusini na pwani ya kusini (mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara)
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Novemba, 2014 na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani isipokuwa maeneo mengi ya mkoa wa Ruvuma, yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi chini ya wastani katika baadhi ya maeneo.
Izingatiwe kuwa pamoja na kuwapo kwa uwezekano wa matukio mengi ya mvua kubwa katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua juu ya wastani, hali hiyo pia inaweza kujitokeza katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.
Matukio ya Vimbunga katika eneo la kusini magharibi mwa Bahari ya Hindi yanatarajiwa kuchangia katika mwenendo wa mvua nchini. Maeneo ambayo hali ya mvua inaweza kuathiriwa zaidi na vimbunga ni pamoja na kanda ya kati, Nyanda za juu Kusini Magharibi, Magharibi mwa nchi na maeneo ya ukanda wa Pwani.

E: ATHARI NA USHAURI
Maeneo mengi ya nchi yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani isipokua baadhi ya maeneo ya kusini mwa nchi yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani. Matarajio ya mvua hizo pamoja na ushauri kwa baadhi ya sekta za kiuchumi na kijamii zimeainishwa kama ifuatavyo;
Kilimo na Usalama wa Chakula
Katika  maeneo mengi ya nchi hali ya unyevunyevu  wa udongo inatarajiwa kuwa ya kutosheleza shughuli za kilimo. Hata hivyo, kwa maeneo machache ya kusini mwa nchi (hususan Mkoa wa Ruvuma) vipindi vya upungufu wa mvua vinatarajiwa mwanzoni mwa msimu na hivyo kuathiri kiwango cha unyevunyevu wa udongo. Hali ya unyevunyevu wa udongo kupita kiasi inayoambatana na vipindi vya mvua  kubwa inaweza kusababisha ongezeko la magugu, matumizi makubwa ya pembejeo, hivyo kuongeza gharama za uzalishaji. Wakulima wanashauriwa kuandaa mashamba  na pembejeo mapema  pamoja na kuzingatia ushauri wa wataalam wa kilimo kwa matumizi sahihi ya ardhi na mbegu.

Malisho  na maji kwa ajili ya mifugo na wanyama pori
Hali ya malisho na upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo na wanyama pori inatarajiwa kuwa nzuri katika maeneo mengi nchini. Hata hivyo, wafugaji  wanashauriwa kuzalisha malisho na  kuyahifadhi kwa matumizi wakati wa kiangazi. Aidha, wafugaji wanashauriwa kufuata maelekezo ya wataalam wa ugani katika maeneo yao hususan matumizi ya maji na malisho  na kukabiliana na  magonjwa ya mlipuko yanayoweza kujitokeza. Kutokana na hali ya mvua inayotarajiwa, matukio ya migogoro inayosababishwa na mifugo,  wanyamapori na shughuli za binadamu na kilimo hayatarajiwi kujitokeza kwa kiasi kikubwa.

Maliasili na Utalii
Mamlaka za usimamizi wa shughuli za utalii na hifadhi za wanyamapori zina shauriwa kuchukua hatua stahiki katika kuzuia uharibifu wa  miundombinu kama barabara na madaraja ndani ya hifadhi dhidi ya adhari za mvua kubwa na za juu ya wastani katika maeneo husika.  Aidha, wawindaji, wapiga picha za kitalii na makampuni ya kitalii yanashauriwa kuchukua tahadhari ya uwepo wa mafuriko kutokana na mvua zinazotarajiwa.
Maji na Nishati
Mtiririko wa maji katika mito na vina vya maji katika mabwawa vinatarajiwa kuongezeka katika maeneo mengi ya nchi kutokana na mvua za msimu wa Vuli. Pamoja na matarajio ya kuwepo kwa mvua za juu ya wastani inashauriwa kuwa maji yatumike kwa uangalifu na kuzingatia taratibu za uvunaji, uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali maji.
Mamlaka za Miji
Inashauriwa  kuchukua hatua  za kuhakikisha kuwa mifumo na njia za kupitisha maji  zinafanyakazi  katika kiwango cha kutosha kuhimili mvua zinazotarajiwa ili kuepusha maji kutuama na kusababisha mafuriko na uharibifu wa miundombinu, upotevu wa maisha na mali katika maeneo husika.
Sekta ya Afya
Ushauri unatolewa kwa jamii na sekta husika kuchukua hatua stahiki katika kuzuia  milipuko ya magonjwa yanayosababishwa  na kutuama kwa maji na utiririshaji wa maji taka usiodhibitiwa katika maeneo yao.
Menejimenti ya Maafa
Mamlaka za maafa na wadau wengine wanashauriwa kuchukua hatua stahiki katika utunzaji wa mazingira, upatikanaji wa maji safi na salama, na usambazaji wa madawa, maji na chakula ikiwa ni hatua za kujiandaa na kukabiliana na majanga yanayoweza kutokea kutokana na vipindi vya mvua  kubwa na mvua za juu ya wastani zinazotarajiwa.
Vyombo vya habari
Vyombo vya habari vinashauriwa kufuatilia, kupata na kusambaza taarifa sahihi za mienendo ya hali ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na kutumia wataalam wa sekta husika katika kuandaa na kufikisha taarifa za masuala mtambuka ya hali ya hewa kwa jamii. Aidha, jamii nayo inashauriwa kufuatilia na kuzingatia taarifa sahihi za hali ya hewa na mirejeo yake kupitia vyombo vya habari.

Angalizo: Mwelekeo wa mvua uliotolewa hapa umezingatia zaidi kipindi cha msimu (miezi mitatu) na hali ya mvua katika maeneo makubwa. Hivyo, viashiria vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya mvua na mabadiliko ya muda mfupi katika maeneo madogo utazingatiwa katika   uchambuzi wa utabiri wa muda wa kati na mfupi. Watumiaji wa taarifa za utabiri huu wanashauriwa pia kufuatilia tabiri za saa 24, siku 10 pamoja na wa mwezi kama zinavyotolewa na Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa taarifa za mwelekeo wa mvua nchini.


Dkt. Agnes L. Kijazi
MKURUGENZI MKUU

No comments:

Post a Comment