STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, September 4, 2014

Odemiwngie kupasuliwa, van Persie akwepa 'kisu'


WAKATI mshambuliaji nyota wa Manchester United anayetokea Uholanzi, Robin van Persie akinusurika kupigwa 'kisu', mshambuliaji was kimataifa wa Nigeria, Peter Odemwingie amebainisha kuwa sasa anahitaji kufanyiwa upasuaji kutokana na majeraha ya goti aliyonayo. 
Odemwingie sasa anategemewa kukosa sehemu ya msimu wa Ligi Kuu kufuatia kuumia katika mchezo ambao Stoke City waliitandika Manchester City kwa bao 1-0 Jumamosi iliyopita. 
Taarifa zinadai kuwa mchezaji huyo anaweza kuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha miezi 10 au zaidi. 
Odemwingie mwenye umri wa miaka 33 alithibitisha hayo jana katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kwa kudai kuwa atakosa mechi nyingi za ligi msimu huu. 
Nyota huyo aliendelea kudai kuwa atafanya kila awezalo kuhakikisha anarejea tena uwanjani akiwa fiti zaidi na kuendelea kuisaidia timu yake ya Stoke.
Majeruhi ya Odemwingie ambaye anachukuliwa kama mchezaji muhimu katika kikosi cha Stoke yamemlazimisha meneja Mark Hughes kumsajili winga wa kimataifa wa Morocco Oussama Assaidi kwa mkopo kutoka Liverpool katika siku ya mwisho kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili majira ya kiangazi.
Hali ikiwa hivyo kwa Odemwingie, Robin van Persie ameiambia Fox Sports NL kuwa hatafanyiwa upasuaji wa goti na kwamba kwa sasa anajipanga kuwania namba dhidi ya mshambuliaji mpya Radamel Falcao ambaye alijiunga na Manchester United Jumatatu.
Wakati United ikimsajili kwa mkopo mshambuliaji huyo raia wa Colombia akitokea klabu ya Monaco, iliripotiwa kuwa Mholanzi huyo atafanyiwa upasuaji hivyo kuwa nje kwa muda mrefu.
Lakini Van Persie, ambaye amekuwa akisumbuliwa na goti mapema katika wasifu wake kisoka, alipuuzia taarifa hizo: "Ninashangaa watu hao kutengeneza hisia kama hizo.
"Sijui yanatokea wapi na ninaweza kusema ukweli kutoka moyoni sitakuwapo hospitali kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji."
Falcao aliigharimu Monaco Euro milioni 60 miezi 12 iliyopita na amefunga mabao 155 katika mechi 200 za mwisho akiwa Porto, Atletico Madrid na klabu hiyo ya Ligue 1. 

No comments:

Post a Comment