STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, October 24, 2014

Mtibwa Sugar waenda Mbeya kulipa kisasi kwa Mbeya City

Kocha Mecky Mexime
Mtibwa Sugar
BENCHI la ufundi la Mtibwa Sugar limesema limeenda jijini Mbeya kwa lengo moja tu, la kuhakikisha timu yao inazoa pointi zote tatu mbele ya wenyeji wa Mbeya City katyika pambano la Ligi Kuu Tanzania Bara litakalochezwa Jumapili uwanja wa Sokoine jijini humo.
Mecky Mexime, kocha mkuu wa Mtibwa alisema kuwa, wanajua pambano hilo litakuwa gumu ila wamejiandaa kuhakikisha wanashinda ikiwa ni pamoja na kulipiza kisasi cha mabao 2-1 walichopewa katika mechi ya msimu uliopita kwenye uwanja huo.
Mexime alisema vijana wake wapo 'fiti' kwa mtanange huo ambao unasubiriwa kwa hamu kutokana na timu zote mbili kushindwa kufanya vema katika mechi zao zilizopita, Mtibwa ikisitishiwa wimbi lake la ushindi mfululizo kwa kulazimisha suluhu na timu iliyorejea ligi hiyo Polisi Moro wakati wapinzani wao Mbeya City wakilala 1-0 kwa mabingwa watetezi na kutibua rekodi yao ya kuwa timu isiyoruhusu bao.
"Tupo njiani kwa sasa, lakini tunaenda Mbeya kwa lengo moja ya kushinda, suluhu dhidi ya Polisi hatukuifurahia kwani imetunyima fursa ya kuendelea kubaki kileleni," alisema Mexime.
Aliongeza kuwa, anatarajia kupata upinzani mkali toka kwa wenyeji wao, lakini kwa namna walivyojiandaa anatarajia kuibuka na ushindi ili kuzoa pointi tatu na kulipa kisasi cha 2-1 walichopewa katika mechi ya marudiano ya msimu uliopita iliyochezwa jijini humo baada ya mchezo wao wa awali uliochezwa Manungu-Turiani kumalizika kwa kutoka suluhu.
Mabingwa hao wa zamani mpaka sasa wanalingana pointi 10 na watetezi Azam kila moja akiwa amecheza mechi nne na kushinda tatu na kutoka sare moja na ni kati ya timu tatu pekee ambazo hazijaonja vipigo msimu huu mpaka sasa, nyingine ikiwa ni Simba ambao wenyewe watacheza kesho na Prisons huku wakiwa hawajaonja ushindi wowote katika mechi zao nne walizoambulia sare.
Hata hivyo Azam wapo kileleni kwa faida ya herufi A, huku timu ya tatu inayowafukuzia ni Coastal Union ikifuatiwa na Yanga ambayo watakuwa na kibarua mjini Shinyanga dhidi ya wageni wa ligi hiyo Stand United. Coastal na Yanga kila moja ana pointi saba.

No comments:

Post a Comment