STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, July 15, 2013

Rais JK awalilia wanajeshi waliokufa Darfur


Amir Jeshi Mkuu wa Tanzania, Rais Jakaya Kikwete
  Rais Jakaya Kikwete, ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ameeleza kushtushwa na kuhuzunishwa na mauaji ya wanajeshi saba wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliokuwa wanalinda amani Darfur, Sudan baada ya kushambuliwa na waasi wa Sudan.
Katika shambulizi hilo ambalo pia wanajeshi wengine 14 walijeruhiwa, pia ametuma salamu za rambirambi kwa JWTZ na kwa familia za wafiwa wote.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais iliyotolewa jijini Dar es Salaam jana ilisema kuwa Rais Kikwete anaungana na Watanzania wote na hasa maofisa na wapiganaji wa JWTZ na familia za wafiwa kuomboleza vifo vya askari hao na anawaombea walioumia katika tukio hilo wapone haraka na kuendelea na majukumu yao ya ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa.
Katika salamu zake za rambirambi kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange na familia za wafiwa, Rais Kikwete na Amiri Jeshi Mkuu amesema:
“Sina maneno ya kutosha ya kuelezea mshtuko, huzuni na masikitiko yangu makubwa kufuatia vifo vya vijana wetu hao ambao wamepoteza maisha yao katika shughuli muhimu sana ya utekelezaji wa majukumu ya Umoja wa Mataifa ya kulinda na kuleta amani katika eneo la dunia ambako maelfu kwa maelfu ya watu wamepoteza maisha yao kwa kushambuliwa na waasi.”

“Napenda kwa niaba ya Watanzania wenzangu niwahakikishieni kwamba hakuna shaka kuwa vijana wetu hao tokea walipokwenda  Darfur Februari mwaka huu, na kwa hakika tokea Tanzania ilipoanza kuchangia walinzi katika eneo hilo mwaka 2007, wamefanya kazi nzuri sana, kazi iliyoongozwa na weledi wa hali ya juu na kazi ambayo imeiletea nchi yetu heshima kubwa.
Tutaendelea kuwaenzi kwa kujivunia kazi yao,” amesisitiza katika salamu hizo. Kupitia kwa Jenerali Mwamunyange, ametuma salamu za rambirambi kwa maofisa wakuu na maofisa wadogo pamoja na wapigaji wote wa JWTZ kwa kupotelewa na wenzao.
“Aidha, kupitia kwako, nawatumia salamu zangu kwa wanafamilia za waliopotelewa na wapenzi wao na ndugu zao katika tukio hilo.
Wajulishe kuwa naungana nao katika kuomboleza. Wajue kuwa uchungu wao ni uchungu wangu pia na wa Watanzania wote na kuwa kwa pamoja tunamwomba Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu.
Vile vile kwa pamoja tunamwomba Mwenyezi Mungu azilaze peponi roho za marehemu,” alisema.
Wanajeshi waliouawa na kujeruhiwa walikuwa sehemu ya askari 37 na ofisa mmoja ambao walikuwa wanasindikiza msafara wa waangalizi wa kijeshi huko Darfur kutoka eneo la Khorabeche kwenda Nyara waliposhambuliwa na waasi kiasi cha kilomita 20 kutoka Khorabeche saa tatu asubuhi Jumamosi iliyopita.
JWTZ YAPELEKA KIKOSI KUCHUNGUZA
Wakati guo huo, JWTZ  limetuma kikosi maalum kwenda  nchini Sudan  kufanya uchunguzi kuhusu mazingira ya kuuawa kwa wanajeshi saba wa Tanzania huko  Darfur.

Vile vile, Jeshi hilo limesema linaendelea kufanya mawasiliano na Umoja wa Mataifa (UN),  kuangalia namna ya kuongeza uwezo wa kujilinda na mashambulizi pindi kikosi cha Tanzania cha kulinda amani kinapokabiliana na mashambulizi ya aina hiyo.

Akitoa taarifa ya awali kwa waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaama, Msemaji wa Jeshi hilo ambaye ni Mkurugenzi  wa Habari na Uhusiano,  Kanali Kapambala Mgawe, alisema tukio hilo lilitokea juzi asubuhi baada ya kikundi cha askari 36 kutoka Tanzania akiwamo ofisa wao mmoja kushambuliwa na kikundi cha waasi wa Sudan.

Mgawe alisema  msafara huo uliojumuisha maafisa na askari kutoka mataifa mengine ambao pia walijeruhiwa,  ulishambuliwa  umbali wa kilomita  20 kutoka  Makao Makuu ya Kikosi hicho.

Mgawe alisema tukio hilo lilitokea katika eneo la sheria ya ulinzi wa amani (chapter 6) ambayo hairuhusu mashambulizi ya silaha.

“Kwa kuwa mazingira ya sasa  Darfur hayapo katika sheria inayoruhusu mashambulizi, hivyo tunaendelea kuwasiliana na UN  na kuwaomba kubadili sheria hiyo ili kuruhusu kutumika ile ya chapter 7 kwa ajili ya kukiwezesha kikundi chetu kujilinda pindi kinapokabiliwa na  mashambulizi ya aina hiyo,” alisema Mgawe

Kadhalika,  Mgawe alisema mpaka sasa taratibu zilizokwishafanyika ni kuhamisha miili ya marehemu kutoka eneo la tukio na kupelekwa Nyara ambako kuna  Hospitali kuu ya eneo la Operesheni kwa ajili ya kuhifadhiwa na majeruhi kupatiwa matibabu.

Pia alisema wanawasiliana na familia za marehemu hao,  na kwamba utaratibu huo ukikamilika majina ya askari hao yatatangazwa.

“Wanajeshi wetu wamepatwa na mkasa huo wakiwa katika utekelezaji wa jukumu lao la Umoja wa Mataifa la kulinda amani nchini Sudan eneo la Darfur,  kwa utaratibu wa Kijeshi hatuwezi kutangaza majina yao mpaka tuwasiliane na familia zao kwanza,” alisema.

Mgawe alisema taarifa hiyo ni ya awali na kwamba taarifa zaidi juu ya tukio hilo  zitaendelea kutolewa.

Hii ni mara ya pili kwa wanajeshi wa Tanzania kuuawa katika Jimbo la Darfur, ambapo Agosti mwaka jana , Kanali Mgawe alinukuliwa na vyombo vya habari akithibitisha kutokea kwa vifo vya askari watatu ambao gari lao lilizolewa na maji walipokuwa wa kivuka mto uliokuwa umefurika maji, huku wakiwa katika utekelezaji wa jukumu lao la Umoja wa Mataifa la kulinda Amani nchini humo.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment