STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, November 26, 2014

Messi ndiye baba lao Ulaya, apiga hat trick ya 31

MSHAMBULIAJI nyota wa Argentina, Leonel Messi amevunja rekodi ya mabao katika Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuiongoza Barcelona kupata ushindi mnono wa mabao 4-0 ugenini mjini Nicosia, Cyprus katika mfululizo wa michuano hiyo.
Messi ambaye amekuwa gwiji wa kuvunja rekodi zilizowekwa na wanasoka wenzake, alifunga 'hat trick' iliyomfanya kufikisha mabao 74 katika michuano hiyo na kumpita aliyekuwa akishikilia rekodi ya mabao mengi katika michuano hiyo Raul aliyekuwa na mabao 71.
Nyota huyo wa Barcelona alikuwa akilingana na Raul baada ya kufunga mabao mawili dhidi ya Ajax mapema Novemba, lakini 'hat trick' hiyo ya 30 katika maisha yake ya soka yalimfanya awapiku wachezaji wote.
Messi alifunga mabao hayo katika dakika ya 38 akimalizia kazi nzuri ya Rafinha, ambalo lilikuwa bao la pili la timu yake baada ya mapema kwenye dakika ya 27 Luis Suarez kufungua akaunti yake ya mabao katika klabu hiyo aliyojiunga nayo msimu huu akitokea Liverpool, alipofunga bao la kuongoza akimalizia kazi nzuri ya Jordi Alba.
Nyota huyo anayeshikilia rekodi kibao katika ulimwengu wa soka ikiwamo wa kuwa Mfungaji Bora wa La Liga akiwa na mabao 253, alifunga mabao mengine mawili katika dakika za 58' na 87 kwa kumalizia pasi za wachezaji wenzake, Dani Alves na Pedro.
Ushindi huo umeifanya Barcelona kushika nafasi ya pili katika kundi lake la F wakiwa na pointi 12, moja pungufu na vinara wa kundi hilo PSG ambayo ilipata ushindi mnono nyumbani dhidi ya Ajax katika mfululizo wa michuano hiyo ya Ulaya.
Akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya mechi Messi amesema: "Nina furaha sana kuvunja rekodi hususan katika mashindano muhimu kama haya, lakini huu ulikuwa mchezo mkubwa kwetu mbali na rekodi zote," amesema.
Mshindi huyo mara nne wa tuzo ya Mwanasoka Bora Duniani, mwenye umri wa miaka 27, kwa mabao yake dhidi ya APOEL yamemfanya afikishe jumla ya mabao 371 akiwa na kikosi cha Barcelona, mbali na mabao 45 aliyonayo akiifungia timu yake ya taifa ya Argentina.
Naye Suarez aliyefunga bao lake la kwanza kwa Barcelona tangu aliposajiliwa kwa kitita cha pauni Mil. 75 alinukuliwa baada ya pambano hilo akisema kuwa anajisikia vizuri kufunga bao hilo.
"Kawaida ni muhimu kwa mshambuliaji kufunga mabao pamoja na kwamba kipaumbele ni kucheza vizuri kwa ajili ya timu. Lakini unajisikia vizuri kupiga bao,"amesema nyota huyo wa Uruguay.
Katika michezo mingine iliyochezwa juzi, Chelsea walipata ushindi mnono ugenini baada ya kuifumua Schalke 04 ya Ujerumani kwa mabao 5-0, huku mkongwe Didier Drogba alifunga bao moja kuthibitisha kuwa bado wamo.
Mabao mengine ya vinara hao wa Uingereza, ambayo imeendeleza rekodi yao ya kucheza mechi mfululuizo bila kupoteza msimu huu yaliwekwa kimiani na nahodha John Terry, Willian, Jan Kirchhoff aliyejifunga, na Ramires.
Ushindi huo wa Chelsea inayofundishwa na Mreno Jose Mourinho, umeihakikishia timu hiyo kwenda hatua ya mtoano kutoka kundi G baada ya kufikka pointi 11, ikifuatiwa na Spoting Lisbon ya Ureno ikijiweka pazuri katika nafasi ya pili baada ya kuinyuka Maribor 3-1.
Matokeo Kamili:
CSKA Moscow     1-1 Roma
BATE  0-3     Porto
Manchester City     3-2 Bayern Munich
APOEL  0-4 Barcelona
PSG     3-1 Ajax
Schalke 04 0-5 Chelsea
Sporting 3-1 Maribor
Shakhtar Donetsk 0-1 Athletic Bilbao
=======

No comments:

Post a Comment