STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, November 26, 2014

Coastal Union yaita nyota wake Tanga

UONGOZI wa mabingwa wa zamani wa soka nchini, Coastal Union walioanza mazoezi jijini Tanga kujiandaa na Ligi Kuu Tanzania Bara, imewachimba mkwara nyota wake kwa kuwapa muda wa wiki moja wawe wameripoti kambini kabla ya kuchukuliwa hatua.
Aidha klabu hiyo imesema haina mpango ya kufanya usajili wowote kwenye dirisha dogo la usajili linaloendelea kwa sababu kikosi chao kimekamilika kila idara.
Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Kassim El Siagi, aliliambia MICHARAZO kuwa, mapumziko ya wiki mbili waliyowapa wachezaji wao walishaisha na timu kuanza mazoezi chini ya makocha wao Wakenya Yusuf Chipo na Ben Mwalala, lakini ni idadi ndogo tu ya wachezaji walioripoti kwenye kambi ya mazoezi na kuufanya uongozi wao kutoa muda wa wiki moja kwa wachezaji hao kuripoti haraka.
"Tumeshanza mazoezi na tumetoa hadi wiki moja kwa nyota wote wawe wamesharipoti, kwa sababu timu inatarajiwa kucheza mechi kadhaa za kirafiki za kujipima nguvu kabla ya kuikabili ligi kuu," alisema.
El Siagi alisema kwa mujibu wa kocha wao, klabu hiyo haihitaji kufanya usajili wowote kwenye dirisha dogo kwa sababu wachezaji waliopo wanakidhi kila idara.
"Hatutaongeza mchezaji yeyote kwenye dirisha dogo, kwa sababu idara zote za wachezaji katika kikosi chetu zimekamilika," alisema.
Coastal waliotwaa ubingwa wa Tanzania mwaka 1988 inakamata nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ikiwa nyuma ya timu za Mtibwa Sugar, Yanga na Azam baada ya kukusanya pointi 11 kutokana na mechi saba ilizocheza.

No comments:

Post a Comment