STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, May 22, 2016

YANGA KWELI YA KIMATAIFA, RAIS FIFA AIPA TANO

http://www.dw.com/image/0,,19078335_303,00.jpg
Mmetwaa mara mbili? Hongereni sana. Rais wa FIFA, Gianni Infantino ameipongeza Yanga kwa kuwa mabingwa wa Tanzania.
SIKIA hii. Msemaji wa Yanga, Jerry Muro amekuwa akiwatania Simba kuwa wa Mchangani, huku akiipaisha timu yake kuwa ya Kimataifa, lakini leo Jumapili imethibitika ni kweli Yanga ni ya Kimataifa baada ya Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino kuipongeza.
Infantino ameipongeza Yanga kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara 2015/16.
Yanga imetwaa ubingwa huo kwa msimu wa pili mfululizo, lakini ikiwa ni mara ya 26 tangu kuanza kwa Ligi Kuu Bara mwaka 1965.

Katika salamu zake, kupitia barua yake ya Mei 18, 2016 kwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi, Infantino ameelezea ubingwa wa Yanga kwamba umetokana na kazi kubwa iliyofanywa na uongozi wa timu hiyo, makocha, wachezaji pamoja na mashabiki.

“Yanga ndiyo mabingwa wa Tanzania. Napenda kuchukua nafasi hii kuipongeza Young Africans na timu nzima isiyoshindika kwa mafanikio haya makubwa. Taji la Yanga ni matokeo ya mshikamano ulioko ndani ya Young Africans,” amesema Infantino katika barua hiyo yenye kichwa cha habari kinachosema: Salamu za Pongezi kwa Yanga.

Amesema pongezi zake ziende kwa uongozi wa klabu, makocha na benchi nzima la ufundi, wachezaji, madaktari pamoja na mashabiki wote wa Yanga.
“Kwa niaba ya familia ya soka, napenda kuchukua nafasi hii kuishukuru Yanga na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa jinsi mnavyopeleka ujumbe chanya wa soka kwa jamii ya michezo,” alisema Infantino katika barua hiyo iliyotua TFF Mei 21, mwaka huu.

Tayari Rais wa TFF, Jamal Malinzi alikwisha kuipongeza Yanga ambayo imepewa Kombe na medali kwa wachezaji 24, viongozi saba wa benchi la ufundi na viongozi wanne wa Kamati ya Utendaji na kwa sasa wanasubiri zawadi ya fedha Sh 81,345,723.
Klabu hiyo iliyotinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho leo ilikuwa Uwanja wa Majimaji Songea kukamilisha msimu wa 2015-2016 dhidi ya Majimaji.

No comments:

Post a Comment