STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, September 9, 2016

Wanaume wa Manchester kumalizana mchana kweupe Jumamosi


Pep Guardiola
ACHANA na kelele zote ulizosikia kuelekea kwenye pambano la kukata na shoka baina ya Manchester United dhidi ya wapinzani wao Manchester City. Mwisho wa yote ni kesho Jumamosi wakati miamba hiyo itakapokwaruzana mchana kweupee.
Itakuwa vita ya makocha Jose Mourinho wa Man United dhidi ya Pep Guardiola ambao wote wametua katika timu zao hizo hivi karibuni na tayari wameshauwasha moto wa kutosha katika mechi tatu za Ligi Kuu ya England (EPL).
Macho na masikio ya wapenzi na mashabiki wa soka duniani kote mwishoni yataelekezwa kwenye mchezo huo mkali wa kumaliza ubishi kwa mahasimu hao wa jiji la Manchester.
Mchezo huo utakaokuwa ukipigwa kwenye Uwanja wa Old Trafford, nyumbani kwa Man United una ladha nyingi za kusisimua kuanzia thamani ya pambano lenyewe na hata nyota wanaotarajiwa kuonyeshana kazi majira ya saa 8:30 mchana.
Katika mchezo huo timu hizo  zitaingia uwanjani zikiwa na rekodi nzuri ya kuanza vyema msimu mpya wa ligi wakiwa wameshinda mechi zao tatu za mwanzo. Hata hivyo pamoja matokeo hayo, United wao watakwenda katika mchezo wa kesho wakiwa na rekodi nzuri zaidi dhidi ya City katika mechi 171 walizowahi kukutana huko nyuma, ambapo wameshinda 71 dhidi ya 49 za wapinzani wao. Mchezo wa mwisho United kuitambia City ulikuwa ni ule uliofanyika Machi mwaka huu katika Uwanja wa Etihad ambapo United walishinda bao 1-0. Mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa mgumu ni wa kwanza kukutana kwa mameneja wote wawili toka mwaka 2013 katika mchezo wa Super Cup ya Ulaya kati ya Chelsea na Bayern Munich ambapo Guardiola aliibuka kidedea kwa kushinda kwa matuta baada ya timu hizo kutoka sare ya mabao 2-2.
Mameneja hao wana historia ndefu kwani wameshawahi kukutana mara 16 wakiwa na timu tofauti katika kipindi cha miaka saba iliyopita. Kulinganisha na historia ya timu hizo, upande huu ni tofauti kidogo kwani katika mara hizo 16 walizokutana Guardiola ndio ameibuka kidedea kwa kushinda mechi saba, wakitoa sare mechi sita huku Mourinho yeye akishinda mechi tatu pekee.
Wakati Kocha Mourinho akiwa Inter Milan walikutana na Guadiola aliyekuwa Barcelona mara nne, mbili Guardiola akishinda, sare moja huku Mourinho naye akiambulia ushindi mara moja. Wakati Mourinho akiwa Real Madrid walikutana na Guardiola aliyekuwa Barcelona tena mara 11, tano kati ya hizo Guardiola akiibuka kidedea, sare nne na Mourinho akiambulia ushindi mara mbili katika kipindi chote alichokuwa Hispania. Mara ya mwisho mameneja hao kukutana ilikuwa Agosti 30 mwaka 2013, ambapo Guardiola akiwa na Bayern Munich aliibuka kidedea kwa changamoto ya mikwaju ya penati baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Chelsea ya Mourinho.
Klabu zote zitawategemea nyota wao wanaokimbiza kwenye orodha ya ufungaji, Man United ikiwa na Zlatan Ibrahimovic wakati wenzao wakitambia Raheem Starling na Duran Nolito wenye mabao mawili kila moja, kinara, Kun Aguero hatacheza pambano hilo kwa vile kafungiwa na FA kwa utovu wa nidhamu.
Kadhalika Man City itawakosa wakali wake kadhaa kwa sabau nyingine ikiwamo kuwa majeruhi akiwamo nahodha, Vincent Kompany, Bacary Sagna, Leroy Sane, Ilkay Gundogan, huku Man United ikimkosa Henrikh Mkhitaryan  aliye majeruhi na kuna uwezekano mkubwa wa Marcus Rashford kulianza pambano hilo kama Mourinho ataamua kusikiliza maombi ya mashabiki wengi wa klabu hiyo iliyopo nafasi tatu.
Katika mechi zao za mwisho, Manchester United ilipata ushindi mwembamba ugenini dhidi ya Hull City, bao likitupiwa kambani na kinda hilo, wakati wapinzani wao walishinda nyumbani kwa mabao 3-1 dhidi ya West Ham na kukaa kileleni.


Ratiba kamili ya EPL kwa wikiendi hii ipo hivi;

Kesho Jumamosi
14:30 Man United    v Manchester City
17:00 Arsenal          v Southampton
17:00 Bournemouth v West Brom
17:00 Burnley          v Hull
17:00 Middlesbroughv Crystal Palace
17:00 Stoke City      v Tottenham
17:00 West Ham      v Watford
19:30 Liverpool        v Leicester City
 

Jumapili
18:00 Swansea        v Chelsea
 

Jumatatu Septemba 12
22:00 Sunderland    v Everton

 

No comments:

Post a Comment