STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, May 21, 2012

Boban azuiwa Airport akimsafirisha Mafisango, kisa...!

Michael Momburi, Kinshasa SAFARI ya mwisho ya kiungo wa Simba, Patrick Mafisango kuonekana duniani, inakamilishwa leo wakati sanduku lenye mwili wake litakapoteremshwa kaburini baadaye jioni. Mafisango alifariki alfajii ya Alhamisi iliyopita baada ya gai lake kuacha njia na kuingia mtaroni. Alikuwa akitoka Maisha Club kurudi nyumbani. Kiungo huyo aliyeacha mke na watoto watatu, aliagwa juzi kwenye Viwanja vya Klabu ya Sigara, Chang'ombe Dar es Salaam. Msafara wa uliosindikiza mwili wa Mafisango ulitua jijini hapa jana saa 6.10 mchana na kulakiwana mashabiki wengi wa kike huku askari wa usalama ndani ya Uwanja wa Ndege wahapa wakishindwa kujizuia na kumwaga machozi. Mafisango atazikwa leo kwenye makaburi ya Kinkole yaliyoko karibu na Uwanja wa Ndege wa Kinshasa. Baada ya mwili wa mchezaji huyo kutua, askari wa uhamiaji pamoja na wahudumu wa afya wanaokagua kadi za chanjo kwa wasafiri ndani ya uwanja wa ndege walianza kuuliza kwamba ni nani huyo lakini walipoelezwa bado hawakuelewa kwa vile mchezaji huyo hakuwahi kutamba na timu yoyote ya Kinshasa. Kiungo wa DC Motema Pembe, Mussa Hassan Mgosi alikuwa miongoni mwa waombolezaji. Mkuu wa msafara wa Simba, Itang'are alipotoa nakala za magazeti ya Tanzania na kuwaonyesha waliacha kazi zao na kuuzingira mwili huo huku wanawake wakishindwa kujizuia nakuanza kumwaga machozi kwa jinsi walivyoona gari lake lilivyochakaa baada ya ajali hiyo. Askari hao walitumia takribani dakika 10 kuangalia jeneza la mchezaji huyo huku wengine wakikimbia ofisi zao na kwenda kuliangalia na walisaidia kulitoa nje kuwakabidhi ndugu ingawa walizuia kabisa kupiga picha eneo la uwanja. Licha ya barabara nyingi kuwa chakavu kwenda Lemba nje ya kidogo ya jiji alikokuwa akiishi marehemu, mwili wake ulibebwa kwa gari ndogo ukiongozwa na ving’ora ingawa msafara huo uliingiliwa na 'daladala'. Msafara mzima ulikuwa na magari manane. Nyumbani kwa marehemu, kulikuwa na wanawake wengi waliokuwa wakimlilia mchezaji huyo wa Rwanda na ilitumia karibu saa nzima kuwatuliza kabla ya Mzee Kinesi kumkabidhi baba mlezi wa Mafisango, Papaa Pierre mwili wa mchezaji huyo kisha kumwelezea tukio zima la ajali na hali ilivyokuwa Tanzania. Pierre alishindwa kujizuia na kuanza kulia kwa sauti ya juu. Mwili huo wa mchezaji huyo ambaye hapa anafahamika kwa jina la Patrick Tabu Ete ambayo ndiyo majina halisi ya wazazi wake, haukukaa sana nyumbani hapo kutokana na nafasi kuwa ndogo na waliuhamishia kwenye Uwanja wa mpira wa Terrain ambao Mafisango alianzia kucheza soka ili kutoa nafasi ya mashabiki kumuaga zoezi linaloendelea hadi leo mchana. Ingawa anaonekana si maarufu sana jijini hapa kama ilivyo Lubumbashi na Rwanda, mchezaji huyo picha zake zilikuwa zimebandikwa kwenye magari mbalimbali ya vijana na hadi jana jioni hakuna mke wake aliyekuwa amewasili wala mtoto. Pierre alisema; “Msibahuu unauma sana, hakuna jinsi ninavyoweza kuelezea lakini nashukuru Wanasimbana Tanzania kwa kumpa heshima stahili mwanangu, hii ni kazi ya Mungu, tumpumzishe aende kwa amani.” Ujumbe wa Shirikisho la Soka la Rwanda, Ferwafa pamoja na familia na wageni mbalimbali mashuhuri walitarajiwa kuwasili usiku wa kuamkia leo kwa shughuli hiyo. Katika hatua nyingine, nguo za Mafisango zimeyeyuka kiaina huku Haruna Moshi ‘Boban’ akionja joto ya jiwe kwenye Uwanja wa Ndege wa hapa. Ndugu wa Mafisango waliokuwa wakiishi naye jijini Dar es Salaam walidai kupakia nguo hizo kwenye ndege na walipofika Kinshasa hazikuonekana huku wahudumu wakidai zitakuwa zimesahaulika Nairobi. “Sisi tuliziweka sehemu ya mizigo lakini tunashangaa hapa hazionekani wanasema labda zimebaki Nairobi, kule ndani ya begi lake vilikuwa vitu vyake vyote mpaka zile nguo alizopatia ajali yaani sijui itakuwaje,” ndugu mmoja alimueleza Papaa Pierre ambaye ni baba mlezi wa Mafisango. Lakini wahudumu wa ndege iliyosafirisha mizigo hiyo wameahidi kwamba leo Jumapili huenda nguo hizo zikapatikana kama kweli zilikwama Nairobi. Wakati huo huo, Haruna Moshi aliyesindikiza mwili wa marehemu, alizuiwa kwa zaidi ya nusu saa na maofisa wa uhamiaji ndani ya Uwanja wa Ndege wa Kinshasa kwa madai kuwa pasi yake ya kusafiria si halali. Maafisa hao walikuwa wakidai pasi hiyo ya dharura anayotumia Boban hairuhusu kuingia nchini Congo bali kwenye nchi za Afrika Mashariki lakini baadaye wakalainika na kumruhusu. “Huyu anarudi Dar es Salaam hawezi kuingia Congo na hii karatasi nyie ondokeni, huyu gari lile pale anarudi nalo mpeni kila kilicho chake,”alisema Afisa mmoja akimwambia mkuu wa msafara wa Simba Mzee Kinesi. Lakini baadaye maafisa hao walipoona picha za Boban kwenye magazeti ya Tanzania yaliyoripoti ajali ya Mafisango walilainika na kuamua kumruhusu Boban aingie ingawa alishachanganyikiwa na kutaka kulia huku akigoma kwenda licha ya kwamba askari hao haswa wa kiume walimsukuma mara kadhaa. “Sasa mimi niende wapi wakati ubalozi wenu umenipa visa na kuniruhusu nije kuwawakilisha wachezaji wenzangu kwenye mazishi ya ndugu yetu,”alisikika Boban akimwambia askari mmoja. Hata hivyo baadhiya askari walisikika waziwazi wakiomba kitu kidogo ili wamuachie Boban apite kwani alisahau hata karatasi yake ya chanjo jijini Dar es Salaam. Habari hii kwa hisani ya Michael Momburi kupitia ShafiiDauda.Blogspot.com

No comments:

Post a Comment