STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, May 21, 2012

Ngumi nazo zikumbukwe kama ilivyo kwa soka

INGAWA soka linatajwa kama mchezo unaopendwa na wengi duniani na hata nchini Tanzania, hata hivyo mchezo wa ngumi nao haupo nyuma kwa kuwa na mashabiki wengi. Kwa hapa nchini ukiondoa miaka ya hivi karibuni ambapo soka kurejesha heshima yake, mchezo wa ngumi ndio uliokuwa ukiongoza kwa kushabikiwa na watu wengi kiasi cha vijana wengi kuota kuwa mabondia. Hii ilitokana na mafanikio makubwa waliyopata mabondia wetu hasa wa ngumi za kulipwa kama akina Rashid Matumla, Rodger Mtagwa, Joseph Marwa, Mbwana Matumla na wengineo. Kabla ya mabondia hao kutamba katika ngumi za kulipwa kuna wakali wengine waliong'ara katika ngumi za ridhaa na kuiletea Tanzania medali katika mashindano mbalimbali ya kimataifa. Iwapo nitataka kuiandika orodha ya nyota walioiletea sifa katika ngumi enzi hizo, huenda nafasi isitoshe lakini baadhi yao ni akina Titus Simba, Habib Kinyogoli, Emmanuel Mlundwa, Bakar Seleman 'Match Maker' na wengine. Hata baada ya kuondoka kwa wakali hao na kuja kizazi cha akina Matumla, bado ngumi zimekuwa zikiendelea kutamba kwa kushuhudia mabondia kama Francis Cheka , Karama Nyilawila na wengine wakiitangaza vema Tanzania. Mataji ya kimataifa waliyotwaa katika mchezo huo likiwemo la hivi karibuni ya IBF-Afrika anaoushikilia Cheka, au ubingwa wa Dunia wa WBF ulioachwa kutetewa na Nyilawila ni mifano ya mafanikio machache ya mchezo wa ngumi. Hata hivyo pamoja na mafanikio hayo, bado mchezo huo haujapewa kipaumbele kama ilivyo kwa soka ambapo licha ya kusuasua na kutokuwa na tija ya kutosha linapewa hadhi ya kipekee nchini. Mchezo huo umekuwa na viwanja vya kutosha vya kuzalisha nyota wa baadae vikiwemo vya kimataifa ambavyo vimezidi kuwatia wazimu mashabiki wake, hali ikiwa ni tofauti kwa michezo mingine hususani ngumi. Mafanikio pekee ya kujivunia katika soka ni kufika fainali za Afrika za mwaka 1980 kwa timu ya taifa na klabu za Simba kutinga fainali za CAF-1993 na kufika nusu fainali za Klabu Bingwa Afrika mwaka 1974 na kucheza hatua ya makundi kwa Simba na Yanga mwaka 1998 na 2003. Pengine kwa mafanikio makubwa iliyopata mchezo wa ngumi kimataifa nilidhani kuna haja ya kuwepo uwanja au ukumbi maalum wa kufanyikia mashindano ya michezo huo kama soka ilivyo na viwanja vyake. Kitambo kidogo watu wa ngumi walikuwa na hakika wakienda ukumbi wa Arnatoglo au Relwe Gerezani, wangesuuza mioyo yao kwa kuwaangalia mabondia wakipasha misuli na wakati mwingine wakichuana mashindanoni. Mabondia wetu kwa sasa wamekuwa wakitangatanga na kutumia ama 'gym' zao zilizopo uchochoroni katika mazingira mabaya kukuzia vipaji vyao wakati wenzao wa soka wanatanua katika viwanja kadhaa vilivyopo nchini. Hata wanapokuwa na mipambano yao, utasikia kama sio Diamond Jubilee, ambao hata hivyo kwa sasa hautumiwi sana, basi ni PTA, Friends Corner au DDC Keko. Yaani hakuna ukumbi maalum wa kufanyikia mapambano ya ngumi kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia katika mataifa mengine kama Marekani yenye kumbi za uhakika kama Madson Square Garden au MGM Grand. Ni vigumu kujilinganisha na Marekani, lakini nadhani kama kungekuwa na kumbi maalum au eneo maalum la kukutanishia mabondia ingesaidia kuwapoa uhakika mabondia na mapromota wao katika kukuza mchezo huo. Inawezekana Tanzania kuwa na kumbi za kisasa na zenye ubora zitakazotoa ushawishi kwa mapromota hata wa nje kuleta mapambano makubwa kucheza nchini kama uwanja wa Taifa ulivyozileta timu kubwa za soka nchini. Nani aliyekuwa akiota siku moja Brazil ingeweza kuja kucheza Tanzania? Lakini kwa kuwa na uwanja wa kisasa wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000 tuliwaona akina Robinho, Kaka na wengine kisha tukawaona akina Yaya Toure, Solomon Kalou, Didier Drogba na wengine wa Ivory Coast. Hivyo ni changamoto kwa serikali, vyama vinavyosimamia ngumi na wadau wote wa ngumi kupigania jambo hili la kuwepo kwa uwekezaji mzuri katika ngumi ili kuufanya mchezo huo uwe na hadhi kulingana na thamani yake. Nadhani kujengwa kwa kumbi au eneo litakalokuwa kama kitovu cha kuwakutanishia mabondia na la kufanyikia mapambano ya ngumi sio tu itawasaidia mabondia kufika mbali, lakini itawavuta watu wa nje kuja nchini. Kuja kwa kutasaidia kuitangaza Tanzania kimataifa katika sekta ya Utalii na hivyo kuliingizia taifa pato kubwa, kama ambavyo Brazil, New Zealand au Vancouver Whitecap ya Canada walivyokuja nchini kisoka. Mwisho

No comments:

Post a Comment