STRIKA
USILIKOSE
Monday, May 21, 2012
Twiga Stars yakiona cha moto kwa Banyana Banyana
WIKI moja tangu iangushiwe kipigo cha mabao 4-1 na madada wenzao wa Zimbabwe, kwa mara nyingine tena timu ya taifa ya soka ya wanawake ya Tanzania, Twiga Stars jana ilikumbana na kipigo kingine kizito toka kwa 'wababe' wa Afrika Kusini, Banyana Banyana.
Katika mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa, Twiga Stars ilicharazwa mabao 5-2 na wageni wao katika mechi zao za kujiandaa na michezo yao ya kufuzu fainali za Afrika.
Twiga itacheza mechi yake ya kufuzu dhidi ya Ethiopia mjini Addis Ababa Mei 26, wakati Banyana itakuwa ugenini Zambia siku hiyo hiyo.
Katika mechi ya jana iliyochezwa kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Banyana walipata goli la kwanza katika dakika ya 23 kupitia kwa Patricia Modise aliyeuwahi mpira uliorudishwa nyuma na beki wa Twiga, Mwanaidi Tamba, na kufanya matokeo ya 1-0 hadi wakati wa mapumziko.
Banyana Banyana iliongeza bao la pili kupitia tena kwa Modise tena aliyepachika wavuni kwa kichwa akiunganisha krosi ya Gabisile Hlumbane,
Twiga ilizinduka na kujipatia bao la kwanza kupitia kwa Fatuma Bushiri aliifungia Twiga Stars kwa mkwaju wa penalti iliyotolewa na mwamuzi wa FIFA, Judith Gamba, baada ya Mwanahamis Omary 'Gaucho' kuangushwa na Janine van Wyk katika dakika ya 63.
Wageni walipata goli la tatu katika dakika ya 73 kupitia kwa Sanah Mollo aliyeingia kuchukua nafasi ya Andiswe Mgloyi baada ya mabeki wa Twiga kujichanganya.
Asha Rashid 'Mwalala' alifanya matokeo yawe 3-2 katika dakika ya 77 kufuatia pasi ya Fatuma Mustapha, lakini dakika mbili baadaye Banyana walipata goli la nne lililofungwa na Sanah tena. Na dakika nne kabla ya mechi kumalizika beki Janine van Wyk aliwafungia Banyana goli la tano kwa mpira wa 'fri-kiki' iliyokwenda moja kwa moja wavuni. Mara ya mwisho wakati timu hizo zilipokutana katika fainali za Mataifa ya Afrika nchini Afrika Kusuni, Twiga ililala 2-1.
Kikosi cha Twiga Stars jana kilikuwa: Fatuma Omary, Fatuma Khatibu, Mwajuma Abdallah, Fatuma Bushiri, Mwanaidi Tamba, Everine Sekikobo, Esther Chabruma 'Lunyamila', Mwanahamisi Omary 'Gaucho', Asha Rashid 'Mwalala', Mwapewa Mtumwa na Fatuma Mustapha.
Banyana: Roxanne Barker, Nodhano Vilakazi, Amanda Sister, Janine van Wyk, Zamandosi Cele, Amanda Dlamini, Mary Ntsweg, Patricia Modise, Gabisile Hlumbane, Rafilde Jane, Andiswe Mgloyi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment