STRIKA
USILIKOSE
Monday, May 21, 2012
Matibabu ya Sajuki nchini India shakani, kisa...!
IMEELEZWA kwamba upungufu wa damu na kudhoofika mwili kupita kiasi kumemfanya mtayarishaji na mcheza filamu mashuhuri nchini, Salum Juma Kilowoko ‘Sajuki’, kushindwa kufanyiwa upasuaji mapema nchini India alikokwenda kwa matibabu.
Sajuki ambaye aliondoka nchini Jumapili iliyopita na kufikia katika Hospitali ya Saifee iliyopo Mumbai, nchini India, anakopatiwa matibabu, ameanza kuongezewa damu na kupewa vyakula ambavyo vitaweza kuupa mwili wake nguvu ili kukabiliana na zoezi la upasuaji.
Kwa mujibu wa rafiki wa karibu wa Sajuki, Denis Sweya ’Dino’ ambaye alizungumza na gazeti hili muda mfupi baada ya kuwasiliana na mke wa Sajuki, Wastara, alisema hali ya msanii huyo imezidi kutengemaa kila kukicha na kuwaomba Watanzania kumuombea zaidi kwa Mungu aweze kurudi haraka katika hali yake.
Sajuki anasumbuliwa na tatizo la uvimbe pembeni ya ini, ambapo wataalamu wa afya wanadai kuwa ni dalili za ugonjwa wa Hepatoma (kansa ya ini).
Taarifa za awali zinaeleza kwamba Sajuki alianza kwa kupata uvimbe sehemu tofauti katika mkono wake mmoja, lakini baadaye tatizo hilo lilihamia ndani na kuanza kupata maumivu makali pembeni ya ini.
Katika mahojiano yake na gazeti moja la wiki, Sajuki alikaririwa akisema madaktari walibaini ana uvimbe pembeni ya ini tatizo ambalo limekuwa likinisumbua kwa muda mrefu.
Kutokana na hali hiyo, wadau mbalimbali wa filamu wakiwemo wasanii waliweza kumchangia nyota huyo kiasi cha fedha ambacho alitakiwa kukipata ili kuweza kufanyiwa matibabu nje ya Tanzania. Tanzania Daima inamtakia kila la kheri Sajuki.
CHANZO:TANZANIA DAIMA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment