STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, May 17, 2012

KIPA nyota wa zamani wa timu za Simba na Yanga, Doyo Moke, amesema umefika wakati wa wadau wa soka nchini kuwapa nafasi wachezaji wa zamani kuziongoza klabu za soka badala ya kuwaachia 'wavamizi' wanaziyumbisha. Moke, aliyewahi kung'ara pia na timu za Majimaji-Songea, Rayon Sports ya Rwanda na Vital'O ya Burundi, alisema watu wasio na uchungu waliovamia mchezo huo ndio wanaolifanya soka la Tanzania kushindwa kusonga mbele. Alisema, dhana kwamba lazima kiongozi wa soka awe na elimu ya Chuo Kikuu, imechangia kudumaza soka la Bongo kwa vile wengi wa wasomi hao wamekuwa akizitumia klabu wa masilahi yao ikiwemo kupata umaarufu. "Lazima watanzania wabadilike kwa kutoa nafasi kwa wachezaji wa zamani kuweza kuongoza soka la Tanzania, mataifa mengine yamefanya hivyo na kufanikiwa, kwa kuwa wachezaji huwa na uchungu wa kweli na soka," alisema. "Wengi wanaojitokeza sasa kuongoza klabu ni wavamizi wasiokuwa na uchungu na mchezo huo zaidi ya kujitafutia umaarufu ili waende kugombea nafasi za uongozi wa kisiasa na kujinufaisha kimasilahi wenyewe," aliongeza. Alisema, ingawa elimu ni kitu cha muhimu katika uongozi, lakini basi nafasi hizo wapewe wachezaji wenye elimu za kutosha kuweza kuongoza gurudumu la soka kama ilivyotokea kwa akina Leodger Tenga, Mtemi Ramadhani na wengineo ambao wameonyesha uwezo mkubwa na ufanisi wa hali ya juu. Kuhusu kinachoendelea kwenye klabu yake ya zamani ya Yanga, Moke mwenye asili ya Jamhuri wa KIdemokrasia ya Kongo, alisema ni lazima pande zinazolumbana zikae chini na kumaliza tofauti zao ili kuinusuru klabu yao. "Kulumbana hakuwezi kukusaidia wakati wana kibarua kigumu katika utetezi wao wa Kombe la Kagame, wakizembea hata taji hilo litapotea hivihivi," alisema. Tangu wafungwe mabao 5-0 na watani zao Simba na kulipoteza taji la Ligi Kuu Tanzania Bara, hali ndani ya klabu ya Yanga imekuwa si shwari ambapo wanachama na wazee wakilumbana na uongozi wao chini ya Mwenyekiti Llyod Nchunga. Mwisho

No comments:

Post a Comment