STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, May 17, 2012

Messi wa Simba achekelewa kuitwa Taifa Stars

MSHAMBULIAJI nyota kinda la klabu ya Simba, Ramadhani Singano 'Messi' amesema hakuamini kirahisi alipolisikia jina lake likitajwa na kocha mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars, Kim Poulsen kujiunga na kikosi cha timu hiyo. Akizungumza na MICHARAZO nyumbani kwao, Keko Machungwa jijini Dar es Salaam, Messi, alisema mara alipojithibitisha kwamba ni kweli ni miongoni mwa wachezaji wa timu hiyo aliporomoka hadi chini kumsujudia Mola wake. Mchezaji huyo aliyetamba na timu za Ubatan na Bombom kabla ya kuonwa na Simba, alisema kifupi ni kwamba amefurahia uteuzi huo akiamini kocha Poulsen amekiona kipaji chake na wajibu wake kutomuangusha. "Kwa kweli sikuamini kama ni mimi niliyetajwa katika kikosi hicho, ila ndugu zangu waliponithibitishia cha kwanza nilichofanya ni kusujudu kumshukuru Mungu kwani nimefurahi kupata fursa hii na sitamuangusha kocha," alisema. Alisema mbali na kujitahidi kwa uwezo wake wote kuonyesha fadhila kwa kocha Kim, pia asingependa kuwaangusha Watanzania ambao wamekuwa na matumaini makubwa na timu yao licha ya kushindwa kuwapa raha. "Ninachoomba nipate nafasi ya kuonyesha uwezo wangu kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu ili kuweza kuisaidia timu ifanye vema na kusuuza roho za watanzania wenye wazimu wa soka," alisema Messi. Messi, aliyepandishwa kikosi cha kwanza cha Simba kitokea timu B ya klabu hiyo hiyo ni mara yake ya kwanza kuitwa Stars, ingawa tangu mwaka 2009 amekuwa akizichezea timu za taifa za vijana U17 na U20. Mchezaji huyo ni kati ya wachezaji 25 walioteuliwa na kocha Poulsen kwa ajili ya kujiandaa na mechi za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia na zile za Afrika zitakazofanyika kati ya mwaka kesho na 2014.

No comments:

Post a Comment